MBIO za kuwania nafasi katika Shirikisho la Riadha Tanzania (RT) zinazidi kushika kasi kwa kujitokeza wagombea 20 hadi sasa wakiwamo watano wanaowania urais akiwamo nyota wa zamani wa kimataifa, Juma Ikangaa anayechuana na mtoto wa mkongwe wa mchezo huo, John Akhwari.
Uchaguzi Mkuu wa RT unatarajiwa kufanyika Agosti 16 jijini Mwanza na nafasi zinazowaniwa ni pamoja na urais, makamu wa rais, mjumbe wa viti maalum wanawake na wajumbe wanne wa kamati ya utendaji.
Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi wa RT, Leonard Thadeo mchakato wa uchukuaji na urejeshaji wa fomu ulifunguliwa Juni 16 na ulikamilika Julai 18 na idadi ya wagombea waliojitokeza kuwania nafasi ya uongozi ni 20, mchuano mkali ukiwa katika urais.
Nafasi hiyo inayovuta hisia za wadau wengi kutokana na umuhimu wake katika kuliongoza shirikisho hilo kuelekea mabadiliko ya kimfumo na kiutendaji imepata wagombea watano akiwamo gwiji wa zamani wa riadha, Juma Ikangaa na mshindi wa pili mfululizo mbio za Boston marathon mwaka 1988 na 1989 akimaliza mara zote nyuma ya bingwa wa Kenya, Ibrahim Hussein.
Wengine ni rais ambaye anatetea kiti hicho, Silas Isangi, Rogath John Stephen Akhwari ambaye pia ni mtoto wa nyota wa zamani wa mchezo huo, John Stephen Akhwari.
Yupo pia William Kalaghe ambaye ni Makamu wa Rais wa RT anayemaliza muda wake, sambamba na mdau mkubwa wa riadha nchini, Angelus Likwembe .
Kwa upande wa Makamu wa Rais, wamejitokeza wagombea wawili ambao ni Baraka Sulus na Wakili Jackson Ndaweka ambaye ni katibu wa RT anayemaliza muda, huku nafasi ya mwakilishi wa Wanawake ikiwaniwa na wagombea wawili pekee, Noela Mafuru na gwiji wa zamani Lwiza John.
Katika nafasi za Ujumbe wa Kamati ya Utendaji, wamejitokeza wagombea 10 ambao ni; Christina Paga, Sylivia Rushokana, Shenya Imori, Alfredo Shahanga, Tullo Chambo, Michael Washa, Ibrahim Adam, Andrew Rhobi, Tabu Mwandu na Joshua Kayombo.
Usahili wa wagombea hao utafanyika Julai kesho Ijumaa kisha Agosti Mosi majina ya waliopitishwa yatatangazwa baada ya hapo Agosti 2-8 itakuwa ni kipindi cha pingamizi na uamuzi kabla ya Agosti 9-16 kuwa muda rasmi cha kampeni na uchaguzi mkuu utafanyika Agosti 16 kupata mabosi wapya.