Samia mgeni rasmi maadhimisho ya mashujaa

Dodoma. Rais Samia Suluhu Hassan atakuwa mgeni rasmi kwenye maadhimisho ya siku ya kumbukumbu ya mashujaa itakayofanyika kesho Julai 25,2025 Mtumba, jijini Dodoma.

Hayo yamesemwa leo Julai 24, 2025 na Naibu Waziri Mkuu, Dk Doto Biteko baada ya kukagua mazoezi ya mwisho kabla ya maadhimisho hayo.

“Ni kuwakumbuka, kuwaenzi na kuwaheshimu mashujaa waliotoa maisha yao, nguvu zao sadaka zao kwa ajili ya uhuru amani na maendeleo ya Taifa letu.”

“Kwa sababu hiyo tutawakumbuka mashujaa wote waliopoteza maisha yao katika uwanja wa vita, waliostaafu baada ya kulitumikia Taifa kwa uaminifu. Na wale waliopata majeraha katika kulinda nchi yetu kwa nguvu zao zote,”amesema Dk Biteko.

Amesema ikifika saa 6:00 usiku leo, mwenge wa kumbukumbu ya mashujaa utawashwa rasmi na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule kwa niaba ya Rais Samia kuashiria kuanza kwa maombolezo ya mashujaa.

Amesema siku ya maadhimisho yenyewe Julai 25,2025 kuanzia saa 3:00 asubuhi kutakuwa na gwaride rasmi la heshima litakalofanywa na vikosi vya ulinzi na usalama ambalo litafanyika kwenye viwanja vya Mashujaa Mtumba jijini Dodoma.

Aidha, Dk Biteko amesema saa 6:00 usiku kesho Julai 25,2025 mwenge wa mashujaa utazimwa kuashiria hitimisho la maombolezo ya kumbukumbu ya mashujaa kwa mwaka 2025.

“Kwa niaba ya kamati ya maandalizi ya maadhimisho ya siku ya mashujaa, naomba kutoa wito kwa wananchi wote walioko Dodoma na wengine kutoka nje ya Dodoma kushiriki kwa wingi katika tukio hili muhimu ili iwe siku yetu sote,”amesema.

Pia amevitaka vyombo vya habari kushirikiana na Serikali katika kuielimisha jamii juu ya historia ya mashujaa, thamani ya mchango wao na sababu ya kuendelea kuwakumbuka kila mwaka.

Maadhimisho hayo hufanyika kila ifikapo Julai 25,2025, ambapo hupambwa na gwaride rasmi na uwekaji wa vifaa mbalimbali kama ngao, mkuki, shada la maua na sime katika mnara wa kumbukumbu za mashujaa.

Rais Samia ndiye atakayeweka mkuki na ngao katika mnara wa mashujaa, akifuatiwa na Mkuu wa Majeshi Jenerali Jacob Mkunda ambaye ataweka sime.

Pia kiongozi wa mabalozi ataweka shada la maua huku mishale ikiwekwa na shujaa wa Taifa.