Dar es Salaam. Ingawa baadhi ya watu huchukulia kwa mzaha usafi wa taulo linalotumika kujifutia maji au unyevu mwilini baada ya kuoga, wataalamu wa afya wamebainisha kuwa usafi wa kifaa hicho ni muhimu sana, hata kama hutumika mwili ukiwa tayari umesafishwa.
Wameeleza kuwa taulo lina uwezo wa kuhifadhi bakteria wanaoweza kusababisha magonjwa mbalimbali ya ngozi kama vile upele na fangasi.
Kwa mujibu wa ujumbe wa watu 10 wa mwanzo kati ya 170 waliochangia kwenye chapisho lililowekwa kwenye ukurasa wa Instagram wa Mwananchi, likiuliza “unafua taulo lako kila baada ya muda gani?” umeonuesha watu saba hawana utaratibu wa kulifua kila mara.
Mmoja kati ya hao 10 hatumii kabisa taulo,. mwingine hufua mara moja kila baada ya wiki mbili na mwingine hufua mara moja kwa mwaka.
Mbali na wachangiaji hao, utafiti uliofanywa na ‘Showers to You’ kampuni ya kuuza na kusambaza bidhaa mbalimbali za bafuni na vyooni nchini Uingereza, umebaini asilimia 5 ya wanaume hufua taulo zao mara moja tu kwa mwaka.
Utafiti huo pia uligundua karibu mtu mmoja kati ya 10 hufua taulo mara mbili tu kwa mwaka. Huku asilimia 33 ya waliohojiwa hufanya hivyo mara moja kila baada ya miezi mitatu wakati asilimia 38 hufua taulo zao mara moja kwa mwezi.
Asilimia 24 hufua mara moja kwa wiki na mmoja kati ya 20 (asilimia 5) hufua kila siku.
Akizungumza na Mwananchi, Modesta Ires amesema licha ya kuwa anapendelea kutumia taulo, hana utaratibu wa kulifua mara kwa mara.
“Mimi natumia taulo, ninayo mawili, lakini sina utaratibu wa kilifua kila wiki. Mara nyingi nalifua nikiona limeanza kubadilika rangi au kutoa harufu ile ya uvundo, hapo najua litakuwa limechafuka kwa hiyo nalazimika kulifua,” amesema mkazi huyo wa Magomeni Dar es Salaam.
Aidha, Roda William mkazi wa Ilala jijini humo amesema anamiliki mataulo matatu kati ya hayo, lipo linalofuliwa baada ya mwezi mmoja
“Binafsi nina mataulo matatu ya kijivu, buluu na pink. Bluu huwa nalitumia mara moja moja. Kwa hiyo ufuaji wake ni mara moja kwa mwezi. Kijivu nalitumia mara kwa mara hivyo kila baada ya wiki mbili nalifua,” amesema Roda.
Kwa upande wake Juma Ismail, amesimulia kuwa alikaa na taulo kwa miaka zaidi ya miaka minne bila ya kulifua
“Nilianza form one na taulo mpaka form four bila kufua, pia nikarudi nalo form five na six,” ameeleza.
Sambamba na hayo Baraka Shonze amesema anazingatia usafi kwa taulo jeupe tu, lakini ya rangi nyingine hana utaratibu wa kuyafua
“Jeupe ndio linafuliwa. Ila haya ya rangi nyingine ukimaliza kujifuta unalianika halinaga shida kama jeupe,” amesema Baraka.
Akizungumza na Mwananchi, Daktari bingwa wa ngozi Venant Mboneko amesema mtu asipozingatia usafi wa taulo, ni rahisi kupata magonjwa kama upele na fangasi
“Taulo unatakiwa kulitumia siku mbili tu ya tatu unatakiwa kulifua. Usikae nalo wiki nzima, ukilitumia leo na kesho anika, kesho kutwa badilisha. Unajua taulo hata hotelini tunashauri mtu mmoja akiingia, akikaa siku moja unatakiwa kubadilisha. Kwa ajili ya kuepuka magonjwa ya kuambukiza kama fangasi, upele na mengine.
“Katika kuyasafisha fua kwa maji safi na sabuni kisha anika juani inatosha. Lakini kuna wengine ni lazima uweke dawa za kufulia na maji ya moto sehemu kama hotelini kwa sababu wanaingia watu tofauti,” amesema Mboneko.
Naye, Dk Sadam Kimanga anayehudumu katika Hospitali ya Ilembula Lutheran mkoani Njombe, amesema si lazima kila sehemu ya mwili kuwa na taulo lake kama ilivyouriwa na baadhi ya wadau.
“Siyo lazima kuwa na taulo la kila sehemu kwa sababu ngozi ina wadudu tunawaita ‘normal flora’ ikimaanisha wapo ila hawana madhara. Ila wataleta madhara ikiwa watatoka sehemu ambayo ni kawaida wao kuwepo, wakaingia sehemu ambayo si kawaida kuwepo.
“Kila sehemu ina ‘normal flora’ wake. Kwa upande wa fangasi ukitumia taulo mbichi ambayo imeanikwa ndani ni rahisi kupata. Ndiyo maana haturuhusu kuanika ndani, labda uwe na sababu ya msingi ya kufanya hivyo na siyo taulo tu hadi nguo za ndani ni vyema kuanikwa juani,” amesema Kimanga.
Kutokana na tabia ya baadhi ya watu hasa wanawake kutumia khanga kama mbadala wa taulo kujifutia maji wakimaliza kuoga, Kimanga anafafanua kuwa hawashauri kufanya hivyo hasa kwa kanga mpya.
“Kanga hatushauri kuitumia kujifutia maji kwa sababu hata ukaushaji wake si mzuri. Kanga ina asili ya ukavu, inachubua. Mara nyingi kama unataka kutumia basi iwe ile iliyowahi kutumika kiasi ambacho imepoteza sifa ya kuchubua,” amesema na kuongeza;
“Khanga au kitenge kilichotumika kikipoteza upya wake hakiwi chenye kuchubua. Hatutumii nguo mpya kujifuta maji hata wamama wakijifungua tunawaambia wasitumie nguo mpya kwa ajili ya watoto kwa sababu ya kuchubua,” amefafanua Kimanga.
Umuhimu wa kusafisha taulo zao mara kwa mara, unasisitizwa na Daktari bingwa wa ngozi kutoka hospitali ya Taifa Muhimbili, Said Mwemba akisema kutofua taulo kunaweza kusababisha magonjwa mengi kama ya kuwasha.
“Ikiwa mtu ana mzio inakuwa rahisi kupata magonjwa hayo. Pia baada ya kulisafisha taulo ni muhimu kulianika katika sehemu yenye jua,” amesisitiza Mwemba
Vilevile, Dk Warles Lwabukuna kutoka hospitali ya Hubert Kairuki Memorial (HKMH), aliwahi kunukuliwa na gazeti hili akisema kuna magonjwa mengi yanayoweza kuenezwa kwa kutumia taulo chafu.
“Hatuwezi kusema eti tuache kutumia taulo, la hasha! Tunatakiwa tutumie taulo vizuri kwa kuzingatia usafi,” alisema.
Dk Lwabukuna ameeleza ili taulo litumike kwa usalama zaidi, kuna mambo yanatakiwa kufanyika kwa mtu anayetumia.
Mtaalamu huyo ambaye amebobea katika magonjwa yasiyoambukiza amesema suala la usafi ni muhumu kuzingatiwa, kwa sababu taulo inaweza kueneza magonjwa.
“Magonjwa hayo yanaenea kutoka katika taulo ambalo mtu amejifutia mwenye ugonjwa fulani labda wa ngozi, viini vyake vitabaki katika taulo hilo na muda mwingine akijifutia anaweza kupata ugonjwa huo,” amefafanua.
Amesema kutokana na taulo lenyewe na sehemu linapowekwa, inawezekana viini vya magonjwa vikazaliana katika taulo hilo.
Dk Lwabukuna ambaye pia ni mhadhiri wa chuo kikuu cha Hubert Kairuki Memorial amesema taulo linatakiwa kufuliwa na maji ya moto kila baada ya siku tatu au siku tatu kwa wiki.
“Tunasisitiza utumiaji wa taulo lazima uendane na usafi na ni vizuri taulo liwe linafuliwa kwa maji ya moto walau kila baada vya siku tatu, kwa sababu kuna watu wengine wanafua taulo kwa wiki mara moja, lakini kila siku analitumia kwa kujifutia na kuliweka bafuni likiwa bichi hivyo hivyo.
“Mtu anajifutia taulo asubuhi analiacha bafuni likiwa bichi, akirudi tena jioni akioga anajifutia. Hii ni hatari kwa afya,” amesema.
Ameeleza kuwa taulo linapofuliwa na kukaushwa vizuri juani, linapokauka linapaswa kupigwa pasi ili kuua vijidudu mbalimbali, ikiwemo hao bakteria.
“Ubichibichi wa taulo unavutia vimelea vya vijidudu vya magonjwa, mfano bakteria na fangasi ambao ndio viini vya magonjwa ambayo yamekuwa ni sababu ya kutokea kwa matatizo ya kiafya, ikiwemo ugonjwa wa UTI,” amefafanua.
Pia amesema jambo la msingi ni kuhakikisha taulo halina unyevunyevu kabla ya kutumika na baada ya kutumika lianike juani.
Mtaalamu huyo wa magonjwa ya ndani amesema mfano wa bakteria na fangasi wanaoleta madhara kwa binadamu ni staphylococcus aureus, streptococcus na E.coli.
“Fangasi aina staphylococcus wanapoathiri sehemu ya ngozi, huifanya ngozi kubadilika rangi na kuwa nyekundu, kuwa na vipele, malengelenge, kuwashwa na wakati mwingine ngozi ya mgonjwa inakuwa imelika kwa sababu ya ugonjwa huo.
“Ili kuepuka na ugonjwa huu wa staphylococcus, unatakiwa kufua taulo yako kwa maji ya moto, halafu ikishakauka unaipiga pasi,” amesema.
Bakteria mwingine anayeeneza magonjwa ni streptococcus ambaye husababisha ugonjwa wa ngozi na mara nyingi ugonjwa huo unafanana na majipu kwenye ngozi.