UONGOZI wa Mbeya City uko katika hatua nzuri za kumsajili aliyekuwa beki wa kushoto wa maafande wa Mashujaa FC, Yahya Mbegu kwa ajili ya kuongezea nguvu kikosi hicho, huku mazungumzo yakienda vizuri baina ya upande wa mchezaji na klabu.
Beki huyo alijiunga na Mashujaa Januari 12, 2025 kwa mkopo akitokea Singida Black Stars na sasa yupo katika mazungumzo ya kuichezea Mbeya City msimu ujao, huku ikielezwa dili huenda likakamilika baada ya mchezaji kuridhia ofa aliyowekewa.
Akizungumza na Mwanaspoti, Ofisa Habari na Mawasiliano wa Mbeya City, Gwamaka Mwankota alisema wamekamilisha baadhi ya sajili kwa lengo la kuongezea nguvu kikosi hicho msimu ujao, japo wameandaa sapraizi kwa mashabiki katika kuwatangaza.
“Tutawatangaza muda muafaka utakapofika kwa sababu tunachokifanya kwa sasa ni kuhakikisha mapendekezo yote ya benchi la ufundi tunayakamilisha kimyakimya, lengo ni kuepuka vurugu zinazoendelea sokoni katika dirisha hili,” alisema Gwamaka.
Mbegu aliyewahi kucheza timu mbalimbali zikiwamo za Geita Gold na Polisi Tanzania, alishindwa kupenya kikosi cha kwanza cha Singida kutokana na uwepo wa beki raia wa Ghana, Ibrahim Imoro aliyejiunga na timu hiyo akitokea Al Hilal ya Sudan.
Timu hiyo inayonolewa na Malale Hamsini aliyerithi mikoba ya Salum Mayanga aliyetua Mashujaa FC, ameirejesha tena Ligi Kuu baada ya kushuka msimu wa 2022-2023, ikianza mawindo ya nyota wapya.