KLABU ya Yanga imethibitisha kumuongezea mkataba wa miaka miwili kiungo wake, Pacome Zouzoua baada ya ule wa awali kumalizika mwisho wa msimu uliopita 2024-2025.
Kiungo huyo raia wa Ivory Coast, alitua Yanga msimu wa 2023-2024 akitokea ASEC Mimosas ambapo alikuwa Mchezaji Bora (MVP) wa Ligi Kuu ya Ivory Coast.
Katika msimu uliopita 2024-2025, Pacome alikuwa na mchango mkubwa wa Yanga kubeba mataji matano ambayo ni Kombe la Toyota, Ngao ya Jamii, Kombe la Muungano, Ligi Kuu Bara na Kombe la FA.
Msimu huo uliokuwa wa pili kwake ndani ya Ligi Kuu Bara, Pacome alicheza mechi 26 kati ya 30 kwa dakika 1,614, huku akihusika kwenye jumla ya mabao 22 kutokana na kufunga 12 na kuasisti mara 10.
Katika msimu wake wa kwanza 2023-2024, Pacome alicheza mechi 23 za ligi kati ya 30 kwa dakika 1430, akihusika kwenye mabao 11 kufuatia kufunga 7 na kuasisti 4.
Ndani ya misimu hiyo miwili kwenye ligi, Pacome amecheza jumla ya mechi 49, akihusika kwenye mabao 33 ambapo amefunga 19 na kuasisti mara 14.
Pacome amemaliza msimu wa 2024-2025 akiwa kinara katika kuchaguliwa kuwa mchezaji bora wa mechi za ligi akifanya hivyo mara nane. Pia ana tuzo moja ya Mchezaji Bora wa Ligi aliyoshinda Juni 2025.
Hadi sasa, Yanga imetangaza kuwaongezea mikataba wachezaji wake wawili ambao ni Mudathir Yahya na Pacome ambao wote wanacheza eneo la kiungo, huku pia ikitambulisha wachezaji wapya watatu ambao ni Moussa Balla Conte (kiungo), Offen Chikola (winga) na Abdulnassir Mohamed (kiungo).
Mbali na wachezaji, pia imemtambulisha Romain Folz raia wa Ufaransa kuwa Kocha Mkuu wa kikosi hicho akichukua nafasi iliyoachwa na Miloud Hamdi aliyemaliza mkataba mwisho wa msimu wa 2024-2025.