BOLT YAZINDUA HUDUMA YA “FAMILY PROFILE” KURAHISISHA SAFARI ZA FAMILIA NCHINI


 ::::::::

Dar es Salaam, 24Julai 2025 – 

Kampuni ya usafiri wa mtandaoni ya Bolt imezindua rasmi huduma mpya ya Family Profile nchini Tanzania, inayowawezesha wateja kupanga na kulipia safari za hadi watu tisa kwa kutumia akaunti moja tu ya Bolt.

Kwa mujibu wa Bolt, huduma hiyo inalenga kurahisisha safari kwa familia, marafiki na mitandao ya msaada wa kijamii, kwa kuwezesha mmiliki wa akaunti ya familia kuwaalika wanafamilia au marafiki kujiunga, kuweka kikomo cha matumizi ya kila mwezi na kufuatilia safari kupitia arifa za moja kwa moja.

Akizungumza katika uzinduzi huo, Dimmy Kanyankole, Meneja Mkuu wa Bolt kwa Kenya na Tanzania, alisema kipengele hicho ni suluhisho la changamoto zinazowakabili wateja wanaoandalia safari kwa niaba ya wengine. “Kupitia Family Profile, tunawawezesha wateja kuwapatia wapendwa wao usafiri wa uhakika, wa kisasa na salama, huku wakibaki na udhibiti na uwazi wa matumizi,” alisema Kanyankole.

Bolt imeeleza kuwa kila anayeshirikishwa kwenye akaunti ya familia anapaswa kuwa na akaunti yake ya Bolt na umri wa angalau miaka 18, na malipo ya safari yatalipwa moja kwa moja na mmiliki wa akaunti kwa kutumia kadi za benki kama Visa. Huduma hiyo inalenga pia kusaidia wazazi, walezi na wale wanaosaidia jamaa wazee au watu wasioweza kutumia programu za usafiri mara kwa mara.

Kwa sasa huduma ya Family Profile inapatikana jijini Dar es Salaam na inatarajiwa kupanuliwa kwenye mikoa mingine ikiwemo Kilimanjaro, Mwanza na Kahama, ili kuongeza usalama na urahisi wa usafiri kwa familia na mitandao ya kijamii kote nchini.