Wenye umri huu hatarini kupata homa ya ini

Dodoma. Watu wenye umri wa miaka 15 hadi 60 wapo hatarini kuugua homa ya ini huku takwimu zikionyesha asilimia 3.5 ya kundi hilo huathiriwa na ugonjwa huo.

Hayo yamebainishwa leo Julai 24, 2025 na Meneja mpango wa Taifa wa kudhibiti Ukimwi, magonjwa ya ngono na homa ya ini, Dk Prosper Njau wakati wa mkutano na waandishi wa habari kuelekea maadhimisho ya siku ya homa ya ini duniani yatakayofanyika Julai 28, 2025 jijini Dodoma.

Dk Njau amesema makundi hayo mara nyingi yamekuwa kwenye hatari kutokana na mchanganyiko wa vyakula wanavyokula na mzunguko wa kimaisha kwa kadri inavyotokea.

Mbali na kundi hilo, watu wanaojidunga dawa za kulevya wamekuwa waathiriwa wakubwa wa ugonjwa huo na kwa sehemu kubwa ndiyo wanaongeza idadi ya asilimia za waathirika.

Ametoa tahadhari kwa wananchi kuchukua tahadhari katika kujilinda na ugonjwa huo ambapo utafiti uliofanyika mwaka 2022 ndiyo uliobaini kuwa asilimia 3.5 ya watu wenye umri wa miaka 15 hadi 60 ndiyo waathiriwa na ugonjwa huo.

“Hili ni tatizo kubwa ambalo linatuumiza, huu ugonjwa una kinga kwa maana ya chanjo lakini mtu akipata maambukizi, suala la uponyaji bado ni tatizo, hivyo tunasisitiza kuhusu elimu ya kujikinga na maambukizi ya ugonjwa huo na tunaamini kuwa tutafanikisha,” amesema Dk Njau.

Akizungumzia siku ya maadhimisho hayo, amesema yanalenga kutoa elimu na kufikisha ujumbe kwa wananchi juu ya namna bora ya kuishi ili kujilinda na homa ya ini na kwa mwaka huu yanafanyika kwa mara ya pili Julai 28, 2025 jijini Dodoma, na mgeni rasmi atakuwa Waziri wa Afya, Jenista Mhagama.

Kwa upande wake, Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Dodoma, Dk Nelson Bukuru amesema kuwa maadhimisho hayo yataanza Julai 26, 2025 katika viwanja vya mashujaa jijini hapa na kuwataka wananchi kujitokeza kwa wingi ili wapate elimu kwani madaktari bingwa watakuwepo kwa ajili ya kutoa elimu na huduma za ushauri kwa wenye matatizo hayo ili kuwapa unafuu.

Amesema kutakuwa na upimaji wa bure na chanjo ya homa ya ini itatolewa kwa wenye uhitaji, hivyo makundi yote yanasisitizwa kujitokeza.

Dk Bukuru amewataka wananchi wenye dalili za magonjwa kama kisukari na shinikizo la damu nao kujitokeza ili wapate huduma, ikiwemo upimaji wa virusi vya Ukimwi na kutakuwa na uchangiaji wa damu.