Kinondoni yaongoza kwa uhalifu, polisi wataja mikakati

Dar es Salaam. Mkoa wa Kipolisi wa Kinondoni jijini Dar es Salaam umetajwa kuongoza katika aina zote nne za uhalifu zilizobainishwa katika ripoti mpya ya Jeshi la Polisi.

Ripoti ya Uhalifu na Usalama Barabarani Jan–Des 2024 (Crime and Traffic Incidence Statistics) iliyochapishwa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), imeonyesha kuwa mkoa huo unaongoza katika uhalifu dhidi ya mali (wizi, uporaji), uhalifu dhidi ya mtu (kujeruhi, kubaka au kuua), na uvunjifu wa amani (ghasia, vurugu au fujo).

Katika matukio 564,477 yaliyoripotiwa, Kinondoni ilihusika katika asilimia 11 ya matukio yote, ikiwa ni mengi zaidi, ikifuatiwa na asilimia 9 kwa Mkoa wa Mwanza na asilimia 7 kwa Ilala.

Kwa matukio ya uhalifu wa mali, Kinondoni iliripoti kesi 31,523; uhalifu dhidi ya mtu, kesi 18,081; na uvunjaji wa amani, kesi 14,103.

Akizungumza na gazeti dada la The Citizen, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro amesema sababu ya Kinondoni kuongoza katika matukio hayo ni kutokana na kuwa lango la watu mbalimbali kupita ndani ya mkoa huo, hivyo ni kawaida kuwepo kwa matukio ya uhalifu.

“Wahalifu wamekuwa wakijaribu kwa njia mbalimbali kuingia na kutekeleza shughuli zao haramu hapa,” amesema Kamanda Muliro.

Amesema idadi kubwa ya kesi zilizoripotiwa inaonyesha kuwa wananchi wanajua haki zao na huchukua hatua kwa kutoa taarifa wanapoona uhalifu, jambo ambalo husaidia polisi kuhakikisha haki inatendeka kwa mujibu wa sheria.

Kamanda Muliro amesema Jeshi la Polisi linaendelea kushirikiana kwa karibu na jamii katika maeneo yote ya Dar es Salaam, na amewahimiza wananchi kuendelea kutoa taarifa za uhalifu kwani jeshi hilo litachukua hatua kali kwa wahusika.

“Tumeimarisha ulinzi katika maeneo hatarishi na tunafanya operesheni mara kwa mara kupunguza kwa kiasi kikubwa matukio ya uhalifu na kuwachukulia hatua wanaohusika,” amesema.

Akidokeza namna ya kukabiliana na uhalifu huo, mtaalamu wa ustawi wa jamii, Dk Zena Mnasi amesema Kinondoni inaonekana kuwa na matukio mengi ya uhalifu kutokana na kuwa na idadi kubwa ya watu wenye uwezo na wasio na uwezo.

Amesema watu wasio na uwezo huvutiwa kuiba mali za wenye uwezo, kwani ni vigumu mtu mwenye kazi rasmi kutenda uhalifu.

“Jambo la kwanza ni kufahamu kuwa tuna vijana wengi ambao hawana ajira. Ili kujikimu, wanatafuta njia zisizo halali, kwa hiyo tutatue tatizo hilo. Lakini ukiangalia wilaya hiyo ina nyumba nyingi za starehe na vijana wanajihusisha na dawa za kulevya tunapaswa kudhibiti hayo pia,” amesema.

Mbali na hayo, Dk Zena amesema Serikali inapaswa kuboresha mifumo ya usalama, kwani baadhi ya maeneo ndani ya mkoa huo wa kipolisi yana vichochoro vingi ambavyo hushawishi watu kutenda uhalifu.

Mkoa wa kipolisi Kinondoni ulirekodi matukio 31,523 ya uhalifu wa mali, ukishika nafasi ya kwanza; ukifuatiwa na Mkoa wa Mwanza (22,983), Ilala (18,569), Temeke (15,141), na Morogoro (14,508).

Kwa upande wa uhalifu dhidi ya watu, Kinondoni pia ilirekodi matukio 18,081; Mwanza (15,738), Temeke (13,603), Mbeya (9,732), na Morogoro (8,942).

Kwa makosa mengine madogo madogo ya jinai, Kinondoni ilirekodi matukio 63,707; Mwanza (51,437), Ilala (36,931), Temeke (36,448), na Morogoro (29,927).

Kwa matukio yanayohatarisha utulivu wa wananchi na usalama wa Taifa, Kinondoni ilirekodi matukio 14,103; ikifuatiwa na Mwanza (12,716), Kilimanjaro (9,925), Ilala (9,867), na Temeke (7,704).

Pia kwa matukio makubwa ya uhalifu, Kinondoni iliongoza kwa matukio 814; ikifuatiwa na Dodoma (772), Mjini Magharibi (700), Arusha (699), na Tanga (660).