Dar es Salaam. Inaweza ikawa sio taarifa njema sana kwa wale jamaa wa ‘ kujibusti’ yaani wanaotumia dawa za kuongeza nguvu za kiume.
Watu hawa wengi wao wakiwa vijana wamekuwa wakikimbilia kutumia dawa za asili za kuongeza nguvu wakiamini zina ufanisi mkubwa.
Hata hivyo, utafiti mpya umebaini dawa nyingi za asili huchanganywa na dawa nyingine za kisasa kama vile sildenafil na tadalafil (Viagra)
Utafiti huo uliofanywa na Chuo kikuu cha Kikatoliki cha Afya na Sayansi Shirikishi Bugando (Cuhas-Bugando), ulitumia sampuli 40 za za asili zilizopimwa maabara, sampuli 25 sawa na asilimia 62.5 zikigundulika kuwa zimechanganywa na dawa za kisasa.
Utafiti huo uliofanyika katika wilaya za Nyamagana na Ilemela jijini Mwanza, ulibaini dawa hizo zimekuwa zikichanganywa kwa siri huku watumiaji wakijua ni dawa za kiasili.
Utafiti huo ulilenga kuchunguza uchafuzi wa bidhaa za asili zinazodai kuongeza nguvu za kiume zinazouzwa katika Jiji la Mwanza.
Akizungumzia utafiti huo, Kiongozi mkuu wa utafiti kutoka Shule ya Famasia ya CUHAS, Flora Mchallah anasema jumla ya sampuli 40 za bidhaa za asili zilikusanywa kutoka kwa wauzaji wa mitaani na kuchambuliwa kwa kutumia mbinu ya kisayansi ya ‘High-Performance Thin Layer Chromatography (HPTLC)’. Sampuli 25 (sawa na 62.5) zilionekana kuwa zimechanganywa na dawa za kisasa.
“Miongoni mwa hizi, mbili (asilimia nane ) zilikuwa na sildenafil, tisa (asilimia 36) zilikuwa na tadalafil, na 14 (asilimia 56) zilikuwa na mchanganyiko wa sildenafil na tadalafil,” anasema.
Anasema uchambuzi wa kiasi ulibaini kuwa sampuli mbili (asilimia 12.5) kati ya zile zenye sildenafil zilikuwa na kiasi kikubwa cha sildenafil kinachozidi kiwango cha juu kinachopendekezwa cha miligramu 100 kwa siku.
Msimamizi wa utafiti huo, Emmanuel Kimaro anasema:
“Cha kusikitisha, baadhi ya bidhaa hizo zina viwango vya juu vya dawa hizi vinavyopitiliza kipimo cha juu kinachoruhusiwa kwa siku. Kiasi kilichotumika kuchanganya ni kingi na mtu anaweza kupata madhara ya kushuka kwa presha au kifo cha ghafla.’’
Kimaro anasisitiza kuwa ni muhimu kufanya uchunguzi wa dawa hizo mara kwa mara ili kuondoa athari zinazoweza kutokea kwa jamii.
Kwa upande wake, Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba Tanzania (TMDA) kupitia Meneja kitengo cha uhusiano Gaudensia Simwanza, ilisema chombo hicho hakihusiki moja kwa moja na dawa hizo na kueleza kuwa Wizara ya Afya ndiyo mhusika zaidi.
Baraza la Tiba asili latoa kauli
Mfamasia wa Baraza la Tiba Asili na Tiba Mbadala, Ndahani Msigwa, anasema watachukua hatua kwani huenda kuna dawa nyingi anazosema zimechakachuliwa kwenye tiba asili.
“Tunapenda kuielimisha jamii itumie dawa zilizosajiliwa na baraza kwa kuwa zimepitiwa na pia kuwa makini na matumizi holela ya dawa hizi kwani hata za kisasa mara nyingi haziuzwi kwa utaratibu rasmi. Tunaelimisha jamii itumie dawa zilizosajiliwa,” anasema.
Anasema watachukua hatua dhidi ya dawa hizo na kuelimisha jamii juu ya kinachoendelea.
Daktari kutoka kitengo cha mama na mtoto katika Hospitali ya CCBRT, Justin Nkulu anataja athari zinazoweza kujitokeza kwa wanaume wanaotumia dawa za kuongeza nguvu za kiume bila ushauri wa daktari.
“Dawa hizi kazi yake ni kutibu shinikizo la juu la damu, hutanua mishipa na kushusha presha, hivyo ni rahisi kusababisha matatizo ya presha na hatari zaidi kwa wenye presha ya kushuka, hatushauri kabisa kuzitumia,”anaeleza.
Anashauri mamlaka inayodhibiti dawa na tiba asili kuingilia kati matumizi holela, akisema kuchanganya dawa asili ambazo hazijapimwa na zile za kisasa kunaweza kuwa na madhara kwa watumiaji wake.
“Kutokana na changamoto hizi, dawa za kuongeza nguvu za kiume zipatikane kwa kibali maalumu. Mwanaume anapoenda duka la dawa, aonyeshe cheti cha daktari ndipo aweze kutumia, kwa kufanya hivyo tunaweza kuwasaidia wanaume wengi wanaotuma dawa hizo pasipo ushauri wa daktari,” anasema.
Dk Nkulu anasema kuna dozi za kutumia kutokana na umri, lakini wapo vijana wanaotumia viwango vya dozi vilivyowekwa kwa ajili ya watu wazima, jambo linalowaweka kwenye hatari za muda mfupi na mrefu.
Mwaka 2022 bidhaa maarufu ya asili iitwayo Hensha, inayojulikana kama “Vumbi la Kongo”, inayotolewa na ilipigwa marufuku sokoni na Baraza la Tiba Asili na Tiba Mbadala Tanzania, baada ya kugundulika kuwa imechanganywa na sildenafil (viagra).