New York, Marekani. Bilionea namba moja duniani Elon Musk amepoteza zaidi ya Dola za Marekani bilioni 12 (zaidi ya Sh29 trilioni za Kitanzania) ndani ya saa 24, baada ya kampuni yake ya magari ya umeme, Tesla, kutangaza kushuka kwa mapato yake kwa kiwango cha kihistoria.
Ripoti ya fedha ya robo ya pili ya mwaka 2025 iliyotolewa na Tesla imeonesha kuwa kampuni hiyo imepata mapato ya Dola bilioni 19.6, kiwango ambacho ni pungufu kwa zaidi ya asilimia 15 ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka jana na ni mara ya kwanza kwa mapato ya Tesla kushuka kwa kiwango kikubwa hivyo tangu mwaka 2020.
Kuporomoka huko kumeibua wasiwasi mkubwa miongoni mwa wawekezaji, na kusababisha thamani ya hisa za kampuni hiyo kushuka kwa zaidi ya asilimia 12 kwenye Soko la Hisa la Nasdaq, hali iliyochangia kuporomoka kwa utajiri wa Musk.

Kwa mujibu wa jarida la Forbes, utajiri wa Musk sasa umeshuka hadi kufikia takriban Dola bilioni 193, ingawa bado anaongoza kwenye orodha ya matajiri duniani, akifuatiwa na Bernard Arnault wa kampuni ya LVMH.
Musk ambaye pia ni mmiliki wa kampuni za SpaceX na X (zamani Twitter), amekuwa akikabiliwa na changamoto mbalimbali za soko na ushindani mkali kutoka kwa wazalishaji wapya wa magari ya umeme hasa kutoka China, kama vile BYD.
Wachambuzi wa masuala ya uchumi wanasema kushuka kwa mapato ya Tesla kunaweza kuashiria mabadiliko katika mahitaji ya soko la magari ya umeme, hasa kutokana na kuongezeka kwa gharama za uzalishaji na ushindani mkali wa bei.

Hata hivyo, katika taarifa yake kwa wawekezaji, Musk amesema kampuni hiyo itaendelea kuwekeza kwenye teknolojia mpya na kupanua uzalishaji wake duniani kote, hasa katika masoko yanayoibukia kama Asia na Afrika.
“Tunaamini njia ya kuelekea katika ufanisi wa muda mrefu bado ipo wazi, na tutazidi kuwekeza kwenye ubunifu,” amesema Musk.
Panda shuka za Tesla kwa miaka mitano
Kampuni ya Tesla imepitia mabadiliko makubwa ya mapato kati ya mwaka 2020 na 2025, ikiwa na kipindi cha ukuaji mkubwa kabla ya kuanza kushuka. Mwaka 2020, Tesla ilipata faida ya mwaka mzima kwa mara ya kwanza, ikikusanya Dola bilioni 31.5 kutokana na ongezeko la mahitaji ya magari ya Model 3 na upanuzi wa viwanda vyake.

Mwaka 2021, mapato yalipanda hadi Dola bilioni 53.8 huku ukuaji huo ukichangiwa na mafanikio ya Model Y na kupanuka kwa masoko ya Ulaya na China. Tesla iliendelea kuvuna zaidi mwaka 2022 baada ya mapato kufikia Dola bilioni 81.5, hasa baada ya kuanzishwa kwa viwanda vya Giga Berlin na Texas, pamoja na kupanda kwa bei ya magari duniani.
Hata hivyo, mwaka 2023 ulileta dalili za kuyumba kwa kampuni hiyo baada ya mapato kuongezeka kidogo hadi Dola bilioni 96.8, lakini yakapungua tena mwaka 2024 hadi Dola bilioni 94 kutokana na ushindani mkali, gharama kubwa na kushuka kwa mahitaji ya magari ya umeme.
Mpaka robo ya pili ya mwaka huu, Tesla ilikuwa imepata mapato ya Dola bilioni 19.6, punguzo la asilimia 15 kutoka mwaka jana