Dosari zamwokoa kwenye adhabu ya kifo

Arusha. Mahakama ya Rufaa imebatilisha mwenendo wa kesi na kufuta adhabu ya kunyongwa hadi kufa aliyohukumiwa Ludan Lyimo, aliyetiwa hatiani kwa mauaji.

Uamuzi huo unatokana na kubainika dosari za kisheria zilizojitokeza wakati wa usikilizwaji wa kesi.

Ludan na Abelly Lyimo, walishtakiwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Moshi, wakidaiwa kumuua Florid Lyimo katika Kijiji cha Mbomai Juu, wilayani Rombo Desemba 17, 2019.

Mwili wa Florid ulikutwa katika Msitu wa KDF, wilayani Rombo mkoani Kilimanjaro ukiwa umefungwa kwenye mfuko wa salfeti.

Jopo la majaji Stella Mugasha, Rehema Kerefu na Paul Ngwembe limetoa hukumu iliyomuachia huru Lyimo, Julai 22, 2025 na nakala yake kupatikana kwenye mtandao wa Mahakama.

Uamuzi wa jopo hilo umefikiwa baada ya kupitia mwenendo wa kumbukumbu za Mahakama na kukubaliana na hoja za pande zote, kuwa mahakama iliyosikiliza kesi hiyo ilikosea kisheria kwa kumtia hatiani mrufani, bila ushahidi uliojitosheleza pamoja na amri ya kuhamisha kesi kutompa mamlaka ya nyongeza hakimu aliyeisikiliza kesi hiyo ya mauaji.

Lyimo alipandishwa kizimbani na mwenzake (siyo mrufani katika rufaa hiyo), waliosomewa shtaka la mauaji kinyume cha kifungu cha 196 cha Kanuni ya Adhabu.

Mrufani alikana kutenda kosa, upande wa mashtaka ulikuwa na mashahidi wanane.

Jaji Mugasha katika hukumu ya jopo hilo amesema wanakubaliana na hoja ya mawakili wa pande zote mbili kuwa amri ya uhamisho wa kesi ya msingi chini ya kifungu 45(2) cha MCA, haikutoa mamlaka kwa Hakimu Mkazi mwenye mamlaka ya nyongeza kusikiliza kesi ya mauaji.

Awali, mtoto wa marehemu, Godfrey Lyimo, (shahidi wa kwanza) aliieleza mahakama kuwa usiku wa Desemba 16, 2018 alisikia sauti ya watu watatu miongoni mwao akidai alikuwa mjomba wake (mrufani), akimwita baba yake atoke nje ya nyumba.

Alieleza aliitambua sauti ya mjomba wake aliyekuwa akifahamiana naye na kwamba, alimsikia baba yake akitoka ndani ya nyumba akiwafuata waliokuwa nje na kusikia hatua zake kuelekea msitu wa KDF.

Hata hivyo, akihojiwa na wakili wa mrufani, shahidi huyo alidai baba yake hakurejea nyumbani na baada ya siku tatu alimtaarifu babu yake, William Lyimo (shahidi wa pili).

Pia Agripina Lyimo, mke wa marehemu (shahidi wa sita) aliripoti suala hilo polisi na alikana kumfahamu mrufani.

Hata hivyo, shahidi wa sita anakumbuka mume wake alitoweka na Desemba 29, 2018 alipokea simu kutoka kwa Hillary Lyimo, aliyemweleza anapaswa kwenda Tarakea kuungana na wengine kutambua mwili wa marehemu uliokutwa msituni.

Alieleza mwili huo uliokutwa ukiwa na kisu, ulikuwa umefungwa na mfuko wa salfeti, huku ushahidi wa daktari aliyeufanyia uchunguzi mwili huo akieleza chanzo cha kifo ni jeraha kubwa kichwani na kutokwa na damu ndani nyingi.

Shahidi wa nane, H1010 Koplo Kailan aliyechunguza mauaji hayo alieleza mrufani na mwenzake walituhumiwa kutenda kosa hilo Desemba 16, 2018 na walionekana msituni wakichimba shimo ambalo mwili huo ulikutwa.

Kwa mujibu wa shahidi huyo, mrufani na mwezake walikiri kumuua na maelezo yao ya onyo yalirekodiwa ila hayakuwahi kuwasilishwa mahakamani kama vielelezo wakati wa usikilizwaji wa kesi hiyo.

Baada ya usikilizwaji wa kesi, Abelly aliachiwa huru kwa kuwa ushahidi haukumuhusisha na mauaji, huku Ludan akitiwa hatiani na kuhukumiwa adhabu ya kunyongwa hadi kufa.

Hakuridhishwa na uamuzi wa Mahakama Kuu, akakata rufaa Mahakama ya Rufaa akitoa sababu 11. Aliwakilishwa na mawakili wawili, huku Jamhuri ikiwakilishwa na mawakili wawili wakiongozwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Rose Sulle.

Majaji kabla ya kuendelea kusikiliza rufaa walitaka kujiridhisha iwapo mahakama ya mwanzo ilipewa mamlaka ya kusikiliza kesi ya mauaji kwa kuzingatia amri ya uhamisho ilitolewa chini ya masharti ya kifungu cha 45 (2) cha Sheria ya (MCA).

Wakijibu hoja hiyo mawakili wa pande zote mbili walikubaliana amri ya uhamisho haikutoa mamlaka kwa Hakimu Mkazi mwenye mamlaka ya nyongeza ya kusikiliza kesi ya mauaji.

Walieleza uhamishaji sahihi wa amri ulipaswa kufanywa chini ya masharti ya kifungu cha 256 A cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA), hivyo kuomba mahakama kubatilisha mwenendo na hukumu iliyokuwa imetolewa.

Katika hoja zao mawakili walidai kusikilizwa upya kwa shauri hilo la mauaji haifai kwani udhaifu wa ushahidi wa mashtaka hauwezi kuendeleza hukumu ya mrufani.

Wakili wa mrufani alieleza ushahidi wa upande wa mashtaka unadhoofishwa na ushahidi wa ajabu wa shahidi wa kwanza wa kutochukua hatua kuripoti kutoweka, kutokutolewa maelezo ya onyo ya mrufani na kushindwa kuwapo mashahidi waliodai kuopoa mwili huo msituni. Aliiomba mahakama imuachie huru mteja wake.

Mahakama iliangalia amri ya uhamisho ya Novemba 25, 2020 kesi hiyo ilihamishiwa  Mahakama ya Hakimu Mkazi Moshi kwa Hakimu aliyeongezewa mamlaka.

Jopo la majaji limesema rekodi iko kimya kuhusu jinsi jalada hilo lilihama kwani hakukuwa na mari yoyote ya uhamisho iliyoamuru kesi kuhama.

“Katika hali hiyo, kwa sababu ya upungufu ulioainishwa, kwa kawaida tungeamuru kesi irudiwe tena, hata hivyo, hatufikirii kama kusikilizwa upya kunastahili kutokana na ushahidi dhaifu wa mashtaka ambao hauwezi kuendeleza hukumu ya mrufani, tutatoa sababu zetu,” amesema.

Jaji Mugasha amesema inashangaza hakukuwa na ushahidi wa moja kwa moja juu ya mauaji na inaweza kutambulika kuwa, hukumu  ilitegemea utambulisho wa mrufani kwa sauti kulingana na ushahidi wa shahidi wa kwanza.

Amesema wameanza kwa kupitia ushahidi wa mashtaka ambao awali shahidi wa kwanza alikiri kumtambua mrufani kwa sababu alikuwa anamfahamu, hata hivyo, wakati wa kuhojiwa alikataa kumfahamu.

Amesema ushahidi wa mashtaka unadhoofishwa na kutokuwepo Hillary William na Pudenciana Epimarck ambao kwa mujibu wa rekodi walitoa taarifa muhimu zilizosababisha kupatikana kwa mwili wa marehemu.

Amesema mashahidi hao wangeweza kufafanua kwa mahakama kuhusu nani, wapi na lini (marehemu) aliuawa na kuzikwa katika msitu wa KDF.

Jopo limesema masuala hayo yameacha mambo mengi na kutilia shaka kesi ya mashtaka.

“Hata hivyo, inashangaza kwamba, upande wa mashtaka haukuonyesha maelezo ya ungamo ya mrufani anayedaiwa kukiri kumuua (marehemu), hapana sababu zilitolewa kwa kushindwa kuonyesha maelezo ya ungamo ya mrufani ambayo kwa hakika yalikuwa na maana,” amesema Jaji Mugasha katika hukumu.

Amesema hakuna ushahidi wa kumuunganisha mrufani na kesi hiyo, akikubaliana na mawakili wa mrufani kwamba kesi haifai kusikilizwa tena kwani itampa fursa mjibu rufaa kujaza mapengo ya ushahidi ambao haukuwepo awali.

“Tunabatilisha mwenendo wa kesi kwa sababu mahakama ya awali haikuwa na mamlaka ya kusikiliza kesi ya mauaji, na hukumu inabatilishwa na kuwekwa kando. Tunaamuru kuachiliwa mara moja kwa mrufani isipokuwa kama kutakuwa na sababu nyingine halali,” amesema.