Kukithiri matumizi nishati chafu yatajwa chanzo kupukutisha misitu

Kilolo. Katika kuhakikisha misitu ya asili ya safu ya milima ya Udzungwa inahifadhiwa kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho, Serikali kwa kushirikiana na mashirika yasiyo ya kiserikali imeanza kutoa elimu kwa wananchi wa Wilaya ya Kilolo mkoani Iringa ili kuwawezesha kutambua thamani ya rasilimali za misitu na umuhimu wa kuacha shughuli zinazoathiri mazingira kama ukataji miti hovyo na kilimo kisicho endelevu.

‎Mashirika yaliyoungana na Serikali kuendesha mpango huo wa Udzungwa Landscape Strategy (ULS) ni Alliance for Community Conservation (MACCO), Southern Tanzania Elephant Program (STEP).

‎Akizungumza na Mwananchi Digital Julai 25, 2025 katika viwanja vya Ipalamwa Wilayani Kilolo mkoani Iringa, Ofisa Misitu Msaidizi wa Kilombero Nature Forest Reserve (KNFR), Francis Rugemalira amesema kuwa asilimia 70 ya hifadhi hiyo ipo mkoani Iringa, huku asilimia 30 iliyobaki ikiwa katika Mkoa wa Morogoro.

‎”Misitu yetu iko hatarini kutokana na uharibifu wa mazingira unaotokana na ukataji miti hovyo na shughuli nyingine za kibinadamu ndiyo maana tumeona michezo kama njia bora ya kufikisha ujumbe,” amesema Rugemalira.

‎Rugemalira ameeleza kuwa Serikali kwa kushirikiana na mashirika yasiyo ya kiserikali yameona kuwa njia bora ya kuwafikia wananchi wa kawaida ni kupitia midahalo ya kijamii inayoambatana na mashindano ya michezo, ambapo watu hukusanyika kwa furaha na shauku kubwa.

‎Rugemalira ameongeza kuwa katika mazingira hayo, ujumbe wa uhifadhi unapenya kwa urahisi na unakumbukwa zaidi tofauti na mikutano ya kawaida ambayo huwakusanya watu wachache na mara nyingine wasio na motisha.

‎”Elimu ya mazingira inayotolewa kupitia michezo kama “Misitu Cup” inatoa nafasi ya kuzungumzia masuala nyeti kama mabadiliko ya tabianchi, uharibifu wa vyanzo vya maji, ukataji miti ovyo na matumizi ya nishati mbadala kwa lugha nyepesi na rafiki kwa jamii,” amesema Rugemalira.

‎”Kupitia burudani, vijana wanashirikishwa kikamilifu katika juhudi za kulinda mazingira, jambo linalowajengea uzalendo na kuwafanya kuwa mabalozi wa uhifadhi katika maeneo yao,” amesema.

‎Kwa upande wake, Frank Lihwa, Mkurugenzi wa STEP amesema mashindano hayo yamelenga kuvutia jamii kushiriki katika kulinda mazingira hasa kwa vijiji vinavyozunguka safu ya milima ya Udzungwa.

‎”Mashindano haya hayalengi burudani tu bali ni chombo cha elimu na tunatamani fursa hii ya kuwahamasisha wananchi kuhusu athari za uharibifu wa mazingira na mbinu mbadala za kuhifadhi misitu,” amesema Lihwa na kuongeza kuwa

‎Lihwa ameongeza kuwa kila mwaka Wananchi wa Kilolo watapata fursa ya elimu ya uhifadhi kwa lengo la kuunganisha elimu na burudani katika kupambana na uharibifu wa mazingira.

‎Akizungumzia mafanikio ya kampeni hiyo, Lihwa ameeleza kuwa katika vijiji vinavyoshiriki mashindano hayo, miradi ya maendeleo kama vikundi vya hisa na vikoba, pamoja na matumizi ya majiko banifu yanayopunguza matumizi ya kuni na mkaa, imeanzishwa.

‎”Tunasisitiza matumizi ya nishati mbadala, ili kupunguza utegemezi wa misitu kwa mahitaji ya kila siku. Tunawawezesha wananchi kuwa na njia mbadala za kujikimu kiuchumi,” amesema.

‎Vilevile Ofisa Mazingira wa Wilaya ya Kilolo, Rhoida Kilangi amesema kuwa matumizi ya michezo kama jukwaa la kuelimisha jamii kuhusu utunzaji wa mazingira ni hatua chanya na ya kisasa inayoweza kuleta matokeo ya haraka na ya kudumu.

‎”Kwa muda mrefu changamoto ya uelewa mdogo kuhusu umuhimu wa misitu na mazingira imesababisha shughuli nyingi za kibinadamu kuhatarisha uhai wa rasilimali hizo muhimu, lakini sasa elimu hiyo inaanza kuenea kirahisi kupitia burudani kama michezo,” amesema Rhoida.

‎Rhoida ameahidi kuwa ofisi yake itaendelea kushirikiana na mashirika na jamii kuhakikisha elimu ya mazingira inawafikia wananchi wote wa Kilolo kwa njia shirikishi na bunifu kama michezo.

‎Amina Ngwata, mkazi wa Kijiji cha Udekwa Wilayani Kilolo amesema kuwa sasa elimu hiyo ataitumia silaha katika misitu ili kuhakikisha kuwa mazingira hayaharibiwi.

‎”Sasa najua umuhimu wa kutokata miti hovyo na kutumia majiko yanayotunza mazingira,” amesema.