Bibi aangua kilio mjukuu akirejesha ndoto kuendelea na masomo

Mbeya. Ikiwa zimepita siku 17 tangu kijana Nature  Wilson (18) kukwama na kukata tamaa ya  kuendelea na masomo ya  kidato cha tano  hatimaye  amerejeshewa tabasamu  na kuondolewa katika malezi duni na kuanza safari ya elimu katika Shule ya Sekondari  ya Wavulana ya Uwata iliyopo jijini hapa.

Tabasamu hilo halijaishia kwa kijana Nature, pia mdogo wake Patrick Wilson (8) ameonyesha furaha baada ya kupata fursa ya kuanza elimu ya awali hadi darasa la saba katika Shule ya Msingi Uwata, jambo ambalo limevuta hisia kwa bibi mlezi Lucia Kapangala (65) kushindwa kujizuia na kuangua kilio.

Kilio cha Lucia kilivuta hisia ya mambo mawili ikiwepo upweka atakaopata baada ya wajukuu zake kuanza safari ya masomo,  sambamba na kutuliwa mzigo wa  malezi na makuzi ya watoto hao.

Imeelezwa watoto hao tangu  wazaliwe  hawamjui baba yao, huku mama yao Mzazi Lida Kapangala (34) ni mlemavu wa kusikia  na hata uwezo wa kutambua  chochote katika maisha ya kila siku.

Leo Ijumaa Julai 25, 2025 na Meneja wa Taasisi ya Tulia Trust  Jackline Boaz chini ya Mkurugenzi  wake Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson imefika nyumbani kwa watoto Nature (18) na Patrick (8) katika Mtaa wa Mwasote Kata ya Itezi jijini hapa na kuwachukua tayari kwa kaunza safari ya elimu.

Hatua hiyo imefuatia  mwanzoni mwa  Julai mwaka huu, Spika wa Bunge, Dk TuliaAckson  kuliombwa na  wananchi wa Mtaa wa Mwasote  Kata ya Itezi kubebe jukumu la kuwasaidia  kuuwasomesha watoto hao na kuitunza familia ya bibi yao Lucia Kapangala (65) ambao wanaishi mazingira  magumu.

Awali, ilielezwa kijana Nature  alihitimu elimu ya kidato cha nne Shule ya Sekondari  Itezi na kuchaguliwa  kujiunga kidato cha tano  Shule ya Sekondari  Rungwe Wilaya ya Rungwe,  mkoani hapa ambapo alikwama kutokana  na kukosa mahitaji.

Hatua hiyo ilipelekea kukaa nyumbani kwa siku kadhaa huku akikata tamaa ya kupata elimu sambamba na mdogo  wake Patrick  ambaye alikuwa anasoma  darasa la kwaza Shule ya Msingi  Mwasote.

Lucia anasema licha ya watoto Nature  na Patrick  kuchukuliwa kuendelea  na masomo kupitia Taasisi ya Tulia Trust  bado yuko kaka yao ambaye yuko moja na Mkoa nchini akipambania maisha.

“Nimewalea kwa shida sana napika na kuuza pombe ili kumudu kutunza familia ya watoto wawili na Mama yao ,Lida Kapangala (34) ambaye ni Mlemavu  wa kusikia na ajiwezi kwa chochote, “amesema.

Lucia amesema kimsingi wanaishi maisha duni  na kuna wakati walala njaa kutokana na mfumo wa maisha ya kila siku.

Anasema kitendo cha Dk Tulia kuwachuka na kuwaendeleza kielimu ni cha kiungwana na kuwaombea safari yao ya elimu  ikawe njema, lakini amewapa husia  wakihitimu wakumbe kugusa jamii yenye uhitaji.

“Lakini nalia machozi ya furaha na huzuni kimsingi nitabaki mkiwa nilizoea kuishi na wajuku zangu sasa ni kama naanza safari mpya ya maisha,”amesema.

Akizungumza  hatua ya kuwaendeleza  kielimu, Meneja wa Taasisi ya Trust, Jackline Boazi amesema ni kufuatia maisha duni wanayopitia kwa kukosa chakula na mahitaji  mengine hali  inayopelekea kukosa utulivu wa kupata elimu.

Amesema hatua hiyo ni maelekezo  ya Spika wa Bunge  Dk Tulia Ackson  ambaye ni Mkurugenzi  wa Taasisi hiyo,kama  muendelezo  wa programu  ya kusaidia wahitaji katika sekta ya elimu na kubainisha  watakuwa chini ya uangalizi wa Taasisi hiyo.

“Kimsingi kama mlivyoona kijana, Nature  (18) ameanza masomo Shule ya Sekondari  ya Wavulana Uwata, lakini mdogo wake tumempeleka Shule ya Msingi  Uwata ataanza elimu ya awali hadi darasa la saba,”amesema.

Katika hatua nyingine Jackline amesema kama Taasisi wametumia zaidi ya Sh5.8 milioni  kwa ajili ya mahitaji  mbalimbali  zikiwepo sare za shule.

Kaimu Mkuu wa Shule ya Sekondari  ya Wavulana  Uwata, Patrick  Lalawima amesema ni jambo la kuishukuru  taasisi hiyo na  watahakikisha anafanya vizuri katika masomo.

“Kuna programu mbalimbali  za masomo tutampitisha lengo ni kuona anatimiza ndoto zake za kupata elimu, lakini kupitia Dk Tulia siyo mwanafunzi wa kwanza kumleta shuleni hapa,” amesema.

Kwa upande wake kijana Nature  amesema matarajio yake ni kufanya vizuri katika masomo  na kuja kusaidia wahitaji  wengine  kwani kwake ni kama ndoto.