NEMC NA MAZINGIRA PLUS WAFANIKISHA PROGRAMU YA TAKA SIFURI KWA SHULE YA SEKONDARI YA WASICHANA YA DAR ES SALAAM

Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) leo 25 Julai, 2025 kwa kushirikiana na Taasisi ya Mazingira Plus wamekabidhi Mradi wa Taka Sifuri kwa Shule ya Sekondari maalumu ya wasichana ya Dar es Salaam ambapo takribani wanafunzi 200 wamehitimu na kukabidhiwa vyeti vya mafunzo ya Mradi huo.

Hafla hiyo ya kukabidhi Mradi huo iliambatana na maonesho mbalimbali ya matokeo ya mafunzo hayo ikiwa ni pamoja na bustani za kioganiki zilizotengenezwa na wanafunzi, utengenezaji wa mbolea kupitia mabaki ya chakula, mabanda ya kuhifadhi na kutenganisha taka pamoja na sanaa ya vinyago vilivyoonesha namna viumbe hai wanavyoathirika na uharibifu wa Mazingira.

Akizungumza katika hafla ya kukabidhi Mradi huo, Meneja Uzingatiaji wa Sheria (NEMC) Bi. Amina Kibola amewapongeza wanafunzi hao kwa kuhitimu mafunzo hayo adhimu huku akiwasisitiza kuzingatia mafunzo hayo kwani yamebeba fursa za kiuchumi sambamba na Utunzaji wa Mazingira.

Aidha, Bi. Amina amewasisitiza kuzingatia dhana ya punguza, tumia tena na rejeleza ambayo ni msingi wa kudhibiti uchafuzi wa Mazingira na pia ni dhana ya kuibua fursa za kiuchumi kupitia urejelezaji wa taka na uchakataji wa taka kuwa malighafi kama vile mbolea.

Kwa upande wake Mratibu wa Programu ya Taka Sifuri mashuleni Bw. Suleman Mang’uro amewataka walimu wa Shule hiyo kusimamia na kuhakikisha Mradi huo unaendelea kwa manufaa ya kiuchumi na utunzaji wa Mazingira.