WAZIRI KOMBO APONGEZA UJUMBE WA TANZANIA KATIKA MKUTANO WA JPC RWANDA, AHIMIZA KUCHANGAMKIA FURSA ZA USHIRIKIANO

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo (Mb.), amewapongeza wajumbe wa Tanzania waliowasili jijini Kigali, Rwanda kwa ajili ya kushiriki Mkutano wa 16 wa Tume ya Kudumu ya Pamoja ya Ushirikiano (JPC) kati ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Jamhuri ya Rwanda.

Akizungumza katika kikao kilichofanyika katika Ubalozi wa Tanzania jijini Kigali, Waziri Kombo ameeleza kuridhishwa na ushiriki wa ujumbe huo, akisema hatua yao ya kuwasili mapema ni uthibitisho wa uzalendo, uwajibikaji na dhamira ya dhati ya kulitumikia taifa.

Aidha, Waziri Kombo ameeleza kuwa hatua hiyo imewezesha wajumbe kufanya maandalizi ya kina kwa ajili ya majadiliano yenye tija, kwa kuzingatia masuala muhimu ya kipaumbele yatakayowasilishwa katika mkutano huo.

Katika hotuba yake, Waziri Kombo amesisitiza umuhimu wa kutumia kikamilifu fursa zinazojitokeza kupitia ushirikiano kati ya Tanzania na Rwanda. Ametoa wito kwa wajumbe kuwa na mikakati madhubuti ya kuzitumia ipasavyo fursa hizo kwa ajili ya maendeleo ya nchi na ustawi wa wananchi.

Vilevile, amewahimiza wajumbe kuendelea kusimamia maslahi ya taifa katika majadiliano yote, akisisitiza kuwa wao ni wawakilishi wa Watanzania na wanapaswa kuhakikisha kuwa Tanzania inanufaika kikamilifu na makubaliano yatakayofikiwa.

Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Said Shaib Mussa, ameeleza kuwa mkutano huo una ajenda mahsusi zilizoandaliwa na wataalamu kutoka pande zote mbili, zikilenga kuimarisha ushirikiano katika nyanja za uchumi, biashara, miundombinu, afya, elimu na usalama wa mipaka.

Mkutano wa 16 wa JPC unatarajiwa kuhitimishwa tarehe 26 Julai 2025 kwa ngazi ya Mawaziri, ambapo viongozi hao watapitisha maazimio ya pamoja na kuweka mikakati ya utekelezaji, ikiwa ni sehemu ya kuimarisha uhusiano wa kidugu kati ya Tanzania na Rwanda na kufungua kurasa mpya za ushirikiano wa kimkakati.


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo (Mb.)

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Said Shaib Mussa

Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Rwanda Mhe. Dkt Habib Kambanga