‘Mzee wa Ubwabwa’ awatangulia viongozi vyama vya siasa uzinduzi kalenda ya uchaguzi

Dodoma. Viongozi wa vyama vya siasa wameanza kuwasili katika viwanja vya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi unakofanyika uzinduzi wa kalenda ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.

Leo Jumamosi Julai 26, 2025 Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi wanafanya uzinduzi wa kalenda ya uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 ambapo viongozi wa vyama vya siasa wamealikwa.

Wa kwanza kuingia alikuwa Mwenyekiti waChama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma), Hashimu Rungwe maarufu Mzee wa Ubwabwa  ambaye ameingia saa 2.05 asubuhi akivalia suti ya rangi ya bluu, shati jeupe na tai nyekundu

Moja kwa moja kiongozi alielekezwa mahali palipoandaliwa viongozi hao kukaa na kukabidhiwa ratiba ya shughuli za leo.

Ilipofika saa 2.11 asubuhi ameingia Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba ambaye aliingia akiwa amevalia shati ambalo rangi yake huvaliwa na wanachama wa chama hicho.

Profesa Lipumba ameelekezwa mahali alipokaa Hashimu Rungwe na baada ya kusalimiana walikaa kwenye viti na muda mwingi Rungwe ameonekana akiangalia simu yake, huku Profesa Lipumba akiwa na Kitabu kikubwa aliendelea kusoma.