Dar/Dodoma. Ndani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) bado hakujapoa. Ndivyo unavyoweza kueleza kutokana na yanayoendelea kugonga vichwa vya wadau wa siasa ndani na nje ya chama hicho kikongwe nchini.
Leo Julai 26, 2025 CCM itafanya mkutano mkuu wa dharura, ikiwa mara ya kwanza katika historia kutaendeshwa kwa staili tofauti.
Mkutano huo ambao utafanyika kwa njia ya mtandao utatanguliwa na vikao vya Kamati Kuu (CC) na Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC), vyote vitafanyika kesho kwa mtindo huohuo wa kidijitali.
Mkutano huo ambao umeitishwa ghafla, haukuwa kwenye kalenda kwa kuwa ni miezi miwili tu imepita tangu chama hicho tawala kifanye mkutano mkuu uliopitisha Ilani ya Uchaguzi Mkuu ya mwaka 2025-2030 jijini Dodoma na kufanya marekebisho ya katiba.
Mengi yanazungumzwa kwenye korido za siasa nchini, huku ikielezwa huenda vikao hivyo, vikatoka na uamuzi mgumu ikiwemo hatima ya makada wake akiwemo Mjumbe wa NEC, Askofu Josephat Gwajima na Katibu wa zamani wa NEC, Itikadi na Uenezi, Balozi Humphrey Polepole.
Mamlaka ya nidhamu kwa viongozi wa hadhi hiyo ni halmashauri kuu.
Taarifa za awali kutoka kwenye vyanzo vyetu mbalimbali zinaeleza kuna mikakati ya kuwafukuza uanachama kwa kile kilichoelezwa na makada ndani ya CCM kuwa wamekwenda kinyume cha maadili na kinachodaiwa kupotosha uamuzi uliofanywa na mkutano mkuu.
Siku za hivi karibuni makada hao wamekuwa wakitoa kauli zinazoonyesha mitazamo tofauti kuhusu uamuzi uliofanywa na vikao vya chama hicho, hasa Balozi Polepole akikosoa mchakato uliompitisha Rais Samia Suluhu Hassan kuwa mgombea urais kwa tiketi ya CCM.
Licha ya kuwa ni kipindi cha kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2025, hofu imetanda zaidi kutokana na ukweli kuwa, tayari CCM imeshafanya mikutano mikuu minne ndani ya miaka minne chini ya uenyekiti wa Rais Samia, zaidi ya ilivyoelezwa katika kalenda kwa mujibu wa Ibara ya 100(3) ya Katiba ya CCM inayosema:
“Mkutano Mkuu wa CCM wa Taifa utafanya mikutano yake ya kawaida mara tatu katika kipindi cha miaka mitano. Mikutano miwili kati ya hiyo itakuwa ya uchaguzi na mmoja utakuwa wa kazi. Kalenda ya vikao vya chama itaonyesha ni lini mikutano hiyo mitatu itafanyika.
“Lakini mkutano usiokuwa wa kawaida unaweza kufanyika wakati wowote ukiitishwa na Mwenyekiti wa CCM au ukiombwa na theluthi mbili ya wajumbe wote wa Halmashauri Kuu ya CCM ya Taifa.”
Mkutano huo umetangazwa ghafla takribani wiki moja tangu CCM ilipobadilisha tarehe ya uteuzi wa wagombea ubunge, ubunge wa viti maalumu na uwakilishi kwa upande wa Zanzibar.
Kikao cha Kamati Kuu ya CCM kwa ajili ya uteuzi kilipangwa kufanyika Julai 19, 2025 lakini siku hiyohiyo, Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM, Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Amos Makalla akautangazia umma kwamba kikao hicho kimeahirishwa hadi Julai 28, mwaka huu.
Makalla akasema kabla ya kikao hicho kitafanyika kikao cha NEC Julai 26 (leo) ambacho kitatanguliwa kamati kuu na vyote vitaongozwa na Rais Samia. Siku hiyo hakusema kama kungekuwa na mkutano mkuu.
Hata hivyo, siku moja kabla ya kikao hicho cha NEC kufanyika kama ilivyotangazwa awali, Makalla akaeleza umeitishwa mkutano mkuu wa dhararu tena kwa njia ya mtandao.
Vikao hivyo vinaitishwa huku kukiwa na vuguvugu la watiania wa udiwani, ubunge wa viti maalumu na wa jimbo wakisubiri uteuzi kabla ya kwenda kukutana na wajumbe kusaka ridhaa ya kupeperusha bendera ya CCM kwenye Uchaguzi Mkuu wa Oktoba, 2025.
Baadhi ya wajumbe wamethibitisha kupokea mialiko ya kushiriki mkutano huo utakaofanyika kwa mtandao, lakini utaratibu huo mpya ni kama umewavuga wakionyesha ugumu wa baadhi ya mambo kujadiliwa kwa njia ya mtandao.
Mmoja wa wajumbe aliyeomba hifadhi ya jina lake, amesema mkutano mkuu wa chama hicho una wajumbe zaidi ya 2,000 itawezekanaje wote washiriki, lakini kama kutahitajika kupiga kura za kuamua jambo itafanyikaje.
“Kuna wajumbe hawajui kabisa kuhusu masuala ya mitandao, itakuwaje kwao. Mkutano mkuu mara zote ni kikao cha uamuzi, unahitaji maoni ya wengi, tutapigaje kura na mambo mengine,” amehoji mjumbe huyo.
Hata hivyo, hatua ya CCM kufanya mkutano huo kidijitali ni sehemu ya utekelezaji wa Ibara ya 99(2) ya Katiba yake, iliyorerekebishwa Mei 2025 na kupitisha kipengele cha mikutano kufanyika kidijitali panapo ulazima kutokana na kukua kwa teknolojia.
Wakati wakipitisha marekebisho hayo katika mkutano mkuu wa Mei, 2025, Mwenyekiti wa chama hicho, Rais Samia alisema: “Tumefunga mitambo ya kuwasiliana mikoa kwa mikoa au wilaya kwa wilaya ili kurahisisha utendaji wa kazi, hatua iliyopendekezwa na idara ya oganaizesheni, kikao cha kwanza ni sekretarieti ya wilaya, kamati ya siasa ya wilaya, sekretarieti ya mkoa kamati ya siasa ya mkoa.”
Polepole, Gwajima watajwa
Taarifa za ndani kutoka kwa makada wa CCM zinaeleza kuna uwezekano mkubwa kwa makada hao kuchukuliwa hatua.
Kauli ambazo zimekuwa zikitolewa na Polepole zimetajwa kuwasukuma makada wengine ndani ya CCM na kutaka hatua zichukuliwe dhidi yake.
“Huyu si mwenzetu kabisa, ana nia ya kuvuruga mambo kwa sababu mkutano mkuu wa Januari 18-19, 2025 ulifuata taratibu zote kwa mujibu wa katiba na kanuni za CCM.
“Polepole akasome katiba ili afahamu kuwa mkutano mkuu una mamlaka ya kuelekeza kikao chochote kifanye uamuzi. Na kwa mujibu wa kanuni, mkutano mkuu unaweza kuitwa na mwenyekiti au theluthi mbili ya wajumbe wa NEC,” amesema Hamis Mgeja, ambaye aliwahi kuwa Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga na kuongeza:
“Kilichofanywa na Polepole ni usaliti kwa kupingana na uamuzi wa vikao halali na hilo ni kosa na kanuni inaelekeza afutwe uanachama na tunaomba hilo lifanyike.”
Hata hivyo, Polepole alipoulizwa iwapo suala lake litajitokeza kwenye vikao hivyo na pengine kufukuzwa uanachama, alisema ni haki ya chama kuchukua hatua kwa mwanachama yeyote, lakini kuna utaratibu wa kufuatwa ikiwemo kupewa haki ya kusikilizwa.
Alisema yeye bado yuko CCM na kwamba, kila binadamu anastahili heshima na anastahili kuhojiwa na kusikilizwa kabla ya kuchukuliwa hatua.
“Mimi sijaitwa na chama hadi muda huu, kwamba nitachukuliwa hatua lakini nitakapoitwa kwenye chama nitajenga msimamo na si mara ya kwanza. Nilishaitwa hadi kamati ya maadili ya chama mwaka 2021,” alisema Polepole alipozungumza na Mwananchi jana.
Kwa upande wake, Mchambuzi wa siasa, Kiama Mwaimu amesema kuitishwa mkutano wa dharura ni jambo halali na katiba ya CCM inaruhusu, lakini lazima kuwepo sababu nzito inayohitaji hadhi ya udharura huo.
“Kwa muktadha huo na mazingira yaliyopo ya kisiasa juu ya mienendo ya baadhi ya makada wa CCM kuwepo na mitizamo tofauti kuhusu taratibu mbalimbali, ikiwemo namna ya kumpata mgombea urais huenda imechangia kuitishwa kwa mkutano huu,” amesema.
“Hilo linaweza kutafsiriwa kwa kubashiri kuwa mkutano huo utakaohusisha na kuwajadili waliotoa maoni kinzani. Jambo jingine kumekuwa na malalamiko kutoka kwa wagombea ubunge na udiwani kuhusu mchakato wa uchaguzi,” amesema Mwaimu na kuongeza: “Kama hayo hayatakuwa basi tusubiri huo udharura utakuwa wa aina gani?”
Kwa upande wake, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Aviti Mushi amesema huenda kutakuwa na kitu mahususi au muhimu ndiyo maana kumeitishwa mkutano huo.
“Sijajua hasa kitakachojadiliwa, maana mgombea urais ameshapatikana au kuthibitishwa tangu Januari 19, 2025 sasa tusubiri tuone hiyo kesho,” amesema.
Jitihada za kumpata Askofu Gwajima ambaye pia ni Mbunge wa Kawe anayemaliza muda wake kuzungumzia kuwapo kwa taarifa hizo hazikuzaa matunda na juhudi zinaendelea.
Julai 13, 2025, Polepole alimwandikia barua Rais Samia ya kujiuzulu wadhifa aliokuwa nao wa Balozi wa Tanzania nchini Cuba kwa sababu mbalimbali ikiwemo ya kutoridhishwa na mwenendo wa mkutano mkuu wa Januari 18-19, 2025 kumpitisha Rais Samia kuwa mgombea urais.
Hata hivyo, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mahmoud Thabit Kombo alipoulizwa hivi karibuni kuhusu suala hilo alisema: “Suala lile lina masuala ya kisheria, kanuni na masuala ya utumishi wa umma na lina taratibu zake, zikikamilika kwa utumishi wa umma taarifa za kina zitatolewa.”
Licha ya mitazamo hiyo, katika mkutano wake na waandishi wa habari jana Ijumaa, Julai 25, 2025, makao makuu ya CCM, jijini Dodoma, Makalla amesema mkutano huo utakuwa na ajenda moja ya kufanya marekebisho madogo ya katiba.
“Ajenda ya mkutano mkuu huu maalumu ni moja tu, marekebisho madogo ya katiba ya CCM. Maandalizi yamekamilika katika wilaya na mikoa yote na kwamba utafanyika kama ulivyoandaliwa,” amesema.
Kwa nini unafanyika kidijitali, amesema Ibara ya 99(2) ya katiba ya chama hicho, inatoa nafasi hiyo, hivyo wanatekeleza matakwa ya kisheria ya CCM.
“Dunia inabadilika na chama hiki kinathibitisha ukubwa wake kwa kuendana na teknolojia,” amesema.
Makatibu wa wilaya na mikoa wamepewa jukumu la kusimamia wajumbe wa mkutano huo kwa maana maandalizi ya ukumbi, uandikishaji, ukaaji ukumbini na uhakiki wa akidi.
“Siyo kwamba huu mkutano utatumiwa ‘link ya zoom’ la hasha, kuna kumbi maalumu ambazo tumekwisha kuziandaa kila eneo. Wajumbe watakuwa hapo. Kazi hii inasimamiwa na makatibu wetu wa wilaya na mikoa,” amesema mmoja wa wajumbe wa sekretarieti aliyeomba hifadhi ya jina.