Hekaya za Mlevi: Barabara zifuate kasi ya magari

Dar es Salaam. Maendeleo ni kutoka kwenye sehemu moja kwenda nyingine iliyo bora zaidi. Ili utoke kwenye sehemu ya mwanzo, ni lazima upate msukumo au haja ya kufanya hivyo. Kwa mfano ulikuwa ukilala kwenye kachumba kamoja peke yako.

Ukaona haja ya kuwa na mwenza, ukampata na mkajaaliwa watoto. Kale kachumba hakatakutosha tena, hivyo itakubidi uongeze chumba kingine au vingine kwa ajili ya watoto.

Hali hiyo ipo kuanzia mtu mmoja mmoja hadi ulimwengu mzima. Nchi yenye watu wachache haina mahitaji mengi au makubwa. Kuna vinchi vidogo kama Swaziland ambavyo havina njaa kabisa.

Wastani wa raslimali zao ni sawa tu na huku kwetu, lakini kwa uchache wao ni rahisi kumfikia kila mtu na kujua maendeleo au maanguko yake na kuyaratibu. Sio sisi ambao inatubidi kupanga bajeti ya matrilioni ili kufanya sensa.

Kule mtu mmoja akinunua gari anajulikana bila hata kutumia mifumo rasmi.  Mwingine akiiba hujulikana mara moja. Na wanapoona sasa magari yameongezeka, wanaweza kabisa kuimarisha miundombinu iweze kumudu wingi wa magari. Kuna tofauti kubwa na huku kwetu ambako ongezeko la magari huwezi kuliona kwenye mfumo wala kwa macho. Kwenye kundi la sisimizi ni vigumu kuwaona kumi walioongezeka.

Tatizo ni kwamba wabongo wana akili nyingi kama zilivyo shida zao. Waliwekewa mifumo ya utambuzi wa ongezeko la watu, wanyama, magari na majumba. Hiyo ingewasaidia kuratibu miundombinu katika maisha yao ya kawaida. Lakini kwa akili zao, wakaichakachua mifumo isome kinyumenyume ili waingize pesa kimyakimya. Sehemu kubwa ya mizigo inayopitishwa nchini kwenda nchi jirani huuzwa hapa bila mifumo kujua.

Matokeo yake kumekuwa na maingizo ya magari kama mvua. Hata tukizijenga barabara zetu kwa dharura hatuiwezi kuimudu kasi ya magari yanayoendelea kufurika mitaani. Foleni na ajali ndiyo sifa kubwa ya Majiji yetu yakiongozwa na Dar es Salaam (ingawa nasikia sasa sio Jiji). Wakati ule barabara zilipokuwa duni tulisema zinasababisha ajali. Sasa barabara ni za lami na ikeka isiyo na mashimo, ajali zimeongezeka maradufu. 

Kumbe tatizo si barabara, ni wingi wa magari. Wakati ule magari yalikuwa machache na ajali zikawa chache. Hivi sasa magari chekwachekwa hivyo lazima ajali zitaonekana nyingi. Hiyo ndiyo maana ya “kwenye nyingi nasaba kuna mingi misiba”. Mji wenye idadi kubwa ya watu unasifika kwa idadi ya wanaozaliwa na wanaokufa. Lakini unaweza kushindwa kwa wastani unapolinganishwa na miji yenye watu wachache.

Foleni za mjini ndio tatizo la kutisha kabisa. Utaligundua hilo baada ya kutumia saa tatu kutoka Moro mpaka kwenye kibao cha ‘Karibu Dar es Salaam’. Lakini si ajabu ukatumia saa nne au zaidi kwa basi hilo hilo kutoka Dar hadi Temeke, yaani kutoka kwenye kibao hicho mpaka nyumbani kwako. Ungetamani kuwapo na treni za SGR kutoka Mbezi zinazoelekea vitongojini.

Taa na askari wanaoongoza barabarani hawajafua dafu kwa utitiri wa magari, bajaji, guta, bodaboda, mikokoteni, baiskeli na waenda kwa miguu wanaotumia barabara hiyo hiyo. Wakati mwingine askari anaachia mdomo wazi kwani sarakasi anazooneshwa na watumiaji wa barabara sio za nchi hii. Askari wamesomea sheria za barabara, lakini wanakutana na bodaboda waliotumwa hela na sio kufuata sheria.

Askari hawana usaidizi wa kamera zinazorekodi matukio, hivyo huamua kesi kutokana na maelezo na ushahidi unaoonekana kwenye tukio. Gari lililogonga lenzie kwa nyuma huwa ndilo lenye makosa. Limeshindwa “kukip-distansi” na hata halikuzingatia taa za breki za lenzake. Lakini likiwa nyuma ya daladala litegemee lolote wakati wowote. Wenzao wana breki za ghafla wamapokula vichwa, yaani wanapookota abiria njiani. 

Wakati ukuta, usipoendana nao utaumia. Wakati huu tulitakiwa kuwa na barabara pana zenye kuyaachia madaladala na watumiaji wengine wajiachie. Kuwe na barabara za juu kwa malori na magari ya safari ndefu.

Usumbufu uliokuwapo unagandamiza sekta mojawapo kati ya hizo. Umeona jinsi mabasi ya mwendokasi yanavyoelemewa na mizigo ya wenzake hadi yanakufa kikondoo. Tatizo si barabara, ila mizigo ya daladala, wenye magari binafsi na watumizi wengine wa barabara.

Wakati tunajikongoja na barabara zetu za analojia, tunakutana na matajiri wanaonunua malori kwa mafungu. Tajiri mmoja anayesafirisha mizigo kwenda nchi jirani, anaingiza malori marefu kumi kwa wakati mmoja. Yote yanaanza safari pamoja kama vile mbwembwe au matangazo, lakini yanajenga foleni ya kutisha barabarani.

Jichukulie wewe upo na gari ndogo nyuma yao. Barabara inakuruhusu kwenda Kilometa 50 kwa saa, lakini haya malori yanakulazimisha kwenda chini ya hapo. Unaamua kuyapita yote kwa maana hakuna nafasi kati ya lori na lori. Ukiwa karibu na kuyamaliza, kule mbele yako unaona basi la abiria likikujia usoni kwa kasi. Kwa mwendo ule ni lazima mtakutana uso kwa uso.

Akili yako inafanya kazi haraka, unaamua kuongeza kasi hadi Kilometa 100 kwa saa kuepusha janga linalokufuata. Unafanya hivyo na kuyavuka malori salama, unaiepuka ajali hiyo mbaya. Lakini mwendo mfupi tu mbele unapigwa mkono na askari wa usalama barabarani. Mikononi ana tochi inayokusubiri usimame ili ianze kubonyezwa. Mimi sikusaidii, ila tafakari mwenyewe unafanyaje.