Mtanzania Arjun Kaur Mittal ang’ara Duniani katika Tuzo ya Global Student Prize 2025

Na Seif Mangwangi, Arusha

Mwanafunzi Mtanzania Arjun Kaur Mittal ameweka historia kwa kuchaguliwa miongoni mwa wanafunzi 50 bora duniani wanaowania Tuzo ya Kimataifa ya Chegg.org Global Student Prize 2025, tuzo yenye hadhi ya kimataifa inayotolewa kwa wanafunzi wenye mchango mkubwa katika elimu, jamii na maendeleo ya kijamii.

Tuzo hiyo, inayotoa zawadi ya Dola 100,000 kwa mshindi (takribani Sh milioni 250 za Kitanzania), inatolewa kwa ushirikiano kati ya Chegg.org na Varkey Foundation kwa lengo la kutambua juhudi za kipekee za wanafunzi duniani kote.

Arjun, ambaye ni mwanafunzi wa North London Collegiate School ya Dubai, alichaguliwa kutoka kwa zaidi ya maombi 11,000 yaliyowasilishwa kutoka nchi 148 duniani akiwa anawakilisha Tanzania katika orodha hiyo adhimu pamoja na wanafunzi wengine wawili kutoka Dubai ambao ni Dalia Zidan anayesoma Al Mawakeb School Al Garhoud na Wiktoria Blazik anayesoma katika shule ya Jumeirah College.

Aidha Tuzo hiyo inalinganishwa na ile ya Global Teacher Prize ambayo hutolewa kwa walimu wanaofanya ubunifu lakini hii hulenga wanafunzi pekee. Tangu ianzishwe miaka mitano iliyopita, imekuwa jukwaa la kuwaibua vijana wanaoleta mabadiliko ndani na nje ya darasa.

Arjun amesifiwa kwa kutumia uwezo wake kuanzisha miradi mbalimbali ya kijamii ikiwemo tovuti, programu za simu na jukwaa la kijamii linalotoa msaada kwa vijana kuhusu afya ya akili, kujifunza kwa ufanisi na kujijengea kujiamini.

Kupitia blogu yake ya elimu na afya ya akili, Arjun amefikia wasomaji zaidi ya 12,000 duniani kote, huku jukwaa lake la Instagram likiwavutia zaidi ya watumiaji 130,000 kwa mwezi.

Aidha, mwanafunzi huyo ameanzisha mpango wa kufundisha mdahalo na uongozi kwa wanafunzi wa shule za umma zenye mahitaji maalumu nchini Tanzania, akilenga kusambaza maarifa ya kufikiri kwa kina na kuzungumza mbele ya hadhira na stadi muhimu kwa uongozi wa kisasa.

Katika mahojiano maalum, Arjun alisema: “Nikiwa Mtanzania, nimebeba maadili na misingi ya jamii yangu. Mafanikio haya si yangu peke yangu, bali ni ushahidi kuwa vijana wa Afrika wana nafasi ya kuibadilisha dunia.”

Mkurugenzi Mtendaji wa Chegg Inc., Nathan Schultz, aliwapongeza wanafunzi hao watatu waliotoka Dubai akisema: “Wameonyesha siyo tu ndoto za kubadili dunia, bali wameanza kuzitekeleza kwa vitendo.”

Naye mwanzilishi wa Varkey Foundation, Sunny Varkey, alisema: “Hadithi ya Arjun na wenzake ni ushahidi kuwa elimu ni silaha ya kutatua changamoto kubwa za dunia.”

Mbali na mafanikio ya kijamii, Arjun pia ni mwanafunzi bora kitaaluma. Amewahi kushiriki tafiti kuhusu afya ya akili, teknolojia na vijana, huku akipata usaidizi wa kitaalamu kutoka mashirika mbalimbali duniani ikiwemo familia yake kupitia kampuni ya Baba yake ya Mount Meru Millers Group Limited yenye makao yake makuu nchini Tanzania.

Katika hafla maalum iliyofanyika katika mji wa Ras Al Khaimah kusherehekea wanafunzi waliochaguliwa, Arjun alipewa heshima ya pekee kama mwakilishi wa Afrika Mashariki, na Tanzania kwa ujumla, katika jukwaa hilo la kimataifa.

Washindi 10 bora wa Tuzo ya Global Student Prize wanatarajiwa kutangazwa mwezi Agosti 2025, huku jina la mshindi mmoja likitarajiwa kutolewa mwishoni mwa mwaka huu na jopo la kimataifa la wataalam maarufu.

Tuzo hii iko wazi kwa wanafunzi wote wenye umri wa miaka 16 au zaidi, walioko katika taasisi rasmi za elimu au mafunzo ya stadi. Hata wanafunzi wanaosoma kwa kupitia njia ya mtandaoni wanaruhusiwa kushiriki.

Kwa sasa, macho ya Watanzania na jamii ya elimu duniani yako kwa Arjun Kaur Mittal, kijana Mtanzania anayethibitisha kuwa mipaka ya mafanikio haina nafasi kwa mtu mwenye dhamira, maarifa, na moyo wa kujitolea.