Dar es Salaam. Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), imesema jumla ya watu milioni 37.65 wamejiandikisha kupiga kura katika Uchaguzi Mkuu wa Rais, wabunge na madiwani utakaofanyika Oktoba mwaka huu.
INEC imefafanua kuwa kati ya wapigakura hao, milioni 36.65 wapo Tanzania Bara na 1,004,627 wapo Zanzibar. Idadi hiyo ni sawa na ongezeko la asilimia 26.55 kutoka idadi ya wapigakura milioni 29.75 waliokuwa katika daftari la mwaka 2020.
Takwimu hizo zimetolewa leo Jumamosi Julai 26, 2025 na Mwenyekiti INEC, Jaji Jacobs Mwambegele wakati akitoa taarifa uzinduzi wa ratiba mpya ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025, hafla iliyofanyika jijini Dodoma na kuhudhuriwa na viongozi wa vyama mbalimbali vya siasa.
Katika hafla hiyo, Jaji Mwambegela amefafanua kuwa “kati ya wapigakura milioni 37.65, wanawake ni milioni 18.94 sawa na asilimia 50.31 na wapigakura 18.71 ni wanaume sawa na asilimia 49.69, wakati wapigakura 49,174 ni watu wenye ulemavu,” ameeleza Jaji Mwambegele.
Mbali na hilo, bosi huyo wa INEC amesema wapigakura 725,876 wapo katika Daftari la Wapigakura la Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC).
Katika hatua nyingine, Jaji Mwambegele amesema jumla ya vituo 99,911 vitatumika katika kupiga kura katika uchaguzi huo.
“Vituo 97,349 vitatumika kupigia kura Tanzania bara na vituo 2,562 vitumika Zanzibar. Idadi hiyo ni sawa na ongezeko la asilimia 22.49 ya vituo 81,567 vilivyotumika katika uchaguzi mkuu wa 2020,” amefafanua.