Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), Jaji wa Rufaa Jacobs Mwambegele amesema jumla ya wapigakura wapya milioni 7.64 wamejiandikisha katika daftari la kudumu la wapigakura.
Amefafanua kuwa idadi hiyo ni sawa na asilimia 136.79 ya makadirio ya awali ambayo yalikuwa ni kuandikisha watu milioni 5.58 sawa na asilimia 18.77 ya wapigakura wote walioandikishwa mwaka 2019/2020.
Jaji Mwambegele ameeleza hayo leo Jumamosi Julai 26, 2025 wakati akitoa taarifa uzinduzi wa ratiba mpya ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025, hafla iliyofanyika jijini Dodoma na kuhudhuriwa na viongozi wa vyama mbalimbali vya siasa.
Mbali na hilo, Jaji Mwambegele amesema jumla ya wapigakura milioni 4.29 wameboresha taarifa zao kwenye daftari hilo, sawa na asilimia 98.23 ya makadirio yaliyokuwa milioni 4.36 ya wapigakura wote walioandikishwa 2019/2020.
“Wapiga kura 99,744 wameondolewa katika daftari kwa kupoteza sifa, sawa na asilimia 16.78 ya makadirio ya awali yaliyokuwa zaidi ya 500,000 ya walioandikishwa 2019/2020,”
Pia, amesema wapigakura 8,703 wamebainika kujiandikisha zaidi ya mara moja, akisema baada ya hafla hiyo, Mkurugenzi wa INEC, Ramadhani Kailima atakabidhi orodha hiyo kwa Jeshi la Polisi kwa hatua za kisheria kwa mujibu wa kifungu cha 114 cha Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani ya mwaka 2024.