Dar es Salaam. Wajumbe wa halmashauri kuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Kinondoni leo wamejitokeza katika Mkutano Mkuu wa Taifa kwa njia ya mtandao, katika ukumbi maalumu uliounganishwa na mfumo wa mawasiliano ya kidijitali.
Wajumbe hao wamekutana katika ofisi ya CCM Wilaya ya Kinondoni iliyopo Mkwajuni, Dar es Salaam, mapema asubuhi.
Miongoni mwa viongozi na wanachama mashuhuri, walioonekana ni Mama Salma Kikwete pamoja na wabunge wanaowakilisha majimbo ndani ya wilaya hiyo.
Katibu wa UVCCM wilaya hiyo, Amosi Simon amesema ukumbi wa ofisi hiyo umeandaliwa kwa ustadi ambapo runinga kubwa yenye uwezo wa mawasiliano ya moja kwa moja kwa njia ya video imewekwa kuwaunganisha wajumbe waliokuwa kwenye kikao cha mtandao na Dodoma.

Kwenye kikao hicho, Mbunge wa Kawe, Askofu Josephat Gwajima, ambaye ni mjumbe hakuhudhuria kikao hicho.
Taarifa kutoka ndani ya chama zinasema kuwa huenda Gwajima alikuwa katika kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM kilichokuwa kikiendelea jijini Dodoma, ambacho yeye ni mjumbe pia.
“Gwajima ni mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa, na leo Halmashauri Kuu ina kikao cha dharura kule Dodoma. Huenda hiyo ni sababu ya kutohudhuria kwake hapa Kinondoni,” amesema Katibu wa CCM wa wilaya hiyo, Jacob Siayi.