JIJI la Mbeya linatarajia kusimama kwa muda kupisha sherehe ya wanachama na mashabiki wa Yanga watakapopokea makombe iliyochukua msimu uliopita, shughuli ambayo itafanyika katika fukwe za Matema (Matema Beach) wilayani Kyela mkoani hapa.
Katika msimu uliopita Yanga ilitwaa ubingwa ukiwa wa nne mfululizo, huku ikiweka rekodi tamu ya kubeba mataji matano ikiwa ni Ligi Kuu Bara, Kombe la Shirikisho (FA), Ngao ya Jamii, Mapinduzi na Toyota iliyobeba nchini Afrika Kusini.
Mratibu wa timu hiyo mkoani Mbeya, Said Komba ‘Kastera’ amesema tukio hilo linatarajiwa kufanyika Agosti 30, mwaka huu, ambapo viongozi wa juu wa timu hiyo wanatarajia kuwasili Mbeya wakiwa na makombe yote ya msimu uliopita.
Amesema lengo ni kuwafikia wanachama, mashabiki na wapenzi wa timu hiyo na kutoa shukrani kwa sapoti waliyoweka hadi timu hiyo kufanya vizuri na kuchagiza mshikamano katika msimu ujao.
“Hili litakuwa tukio la kihistoria kupokea makombe yote matano ya msimu uliopita, tukio ambalo litafanyika katika fukwe za Matema (Matema Beach), viongozi wa juu watakuwapo wote,” alisema Kastera.
Kigogo huyo aliongeza hadi sasa maandalizi yanakwenda vyema ambapo jana Jumamosi matawi yote ya Mkoa wa Mbeya yalitarajiwa kukutana katika kikao cha mipango na utekelezaji ili kuvunja rekodi ya mwaka jana.
Mwenyekiti wa Kamati ya Hamasa na Habari mkoani humo, Rajabu Mrisho alisema kikao kingetoa mwelekeo wa sherehe hiyo akiwaomba wanachama wa mikoa yote ya Nyanda za Juu Kusini kujitokeza.
“Itakuwa sherehe kubwa ambayo itaacha historia. Yeyote anayetaka awe upande wa mtani wetu Simba anakaribishwa kuyaona makombe yetu na kupiga nayo picha. Waliopo mikoa ya jirani wote wafike,” alisema Mrisho.