Kyombo ajiandaa kutua Mbeya City

MABOSI wa Mbeya City wanasuka kikosi chao kimyakimya kwa ajili ya kuleta ushindani msimu ujao wa 2025-2026 na kwa sasa wako hatua za mwisho za kukamilisha uhamisho wa aliyekuwa mshambuliaji nyota wa Pamba Jiji, Habib Kyombo.

Nyota huyo aliyejiunga na Pamba kwa mkopo dirisha dogo la Januari 2025, akitokea Singida Black Stars, alivunja mkataba wake na kikosi hicho, hivyo kwa sasa ni mchezaji huru, jambo linalowavutia Mbeya City kutokana na uzoefu wake.

Taarifa ambazo Mwanaspoti imezipata, zinaeleza viongozi wa Mbeya City wameanza mazungumzo ya kina na kambi ya mchezaji huyo kwa ajili ya kuipata saini yake msimu ujao na hadi sasa kila kitu kinaenda vizuri baina ya pande zote mbili.

Akizungumza na Mwanaspoti, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Mbeya City, Ally Nnunduma alisema mipango ya kukisuka kikosi hicho kwa ajili ya msimu ujao imeanza japo ni mapema sana kuweka wazi ni mchezaji gani wanayemhitaji dirisha hili.

“Tutakapokamilisha taratibu zote za uhamisho wa kila mchezaji tutaziweka wazi, ila itoshe kusema kwa sasa tunaendelea na mazungumzo na baadhi yao ingawa siyo muda sahihi kwetu wa kutoa taarifa hadi pale tutakapoona inafaa,” alisema Nnunduma.

Kyombo ni miongoni mwa nyota wazoefu na mbali na kuzichezea Singida na Pamba, pia alicheza Simba kisha baadaye kujiunga na Fountain Gate na sasa anakaribia kutua Mbeya City inayopambana kuweka heshima msimu ujao.

Mbeya City ilimaliza Ligi ya Championship ikiwa nafasi ya pili na pointi 68 baada ya kushinda mechi 20, sare nane na kupoteza mbili nyuma ya Mtibwa Sugar iliyoibuka mabingwa wapya msimu huu na pointi zake 71.

Timu hiyo inayonolewa na Malale Hamsini aliyerithi mikoba ya Salum Mayanga aliyetua Mashujaa, ameirejesha tena Ligi Kuu baada ya kushuka msimu wa 2022-2023, ikianza mawindo ya nyota wapya kwa ajili ya msimu ujao ili kuongeza ushindani.