Mwijage azikwepa mbili na kutua KMC

BAADA ya kuhusishwa na Pamba Jiji na Mtibwa Sugar aliyekuwa winga wa Kagera Sugar iliyoshuka Ligi Kuu Bara msimu uliopita, Erick Mwijage amejiunga na KMC.

Winga huyo ambaye alikuwa anahusishwa kujiunga na Pamba Jiji na Mtibwa Sugar amefikia makubaliano ya kusaini mkataba wa kuitumikia KMC kwa mkataba wa miaka miwili.

Mwanaspoti limethibitishiwa na mmoja ya viongozi wa KMC kuwa tayari wamefikia makubaliano na winga huyo na wanaamini atakuwa chachu ya ushindani wa kikosi hicho msimu ujao huku akidai kuwa wameridhishwa na uwezo wake.

“Hiki ni kipindi cha usajili wachezaji wengi wazuri wanapata ofa nyingi, hivyo ni muda wetu kuongeza umakini na kuwa katika hali nzuri kiuchumi ili kukamilisha sajili ambazo zimependekezwa na benchi la ufundi,” alisema kiongozi huyo.

“Hatukuwa vizuri msimu ulioisha, tunahitaji kuboresha kikosi ili kuongeza ushindani msimu ujao. Nafikiri uwekezaji mzuri na kutumia ripoti tuliyopewa na kocha lengo likiwa ni kuweka timu sehemu nzuri msimu ujao.”

Kiongozi huyo alisema kwa asilimia kubwa wamefanikisha usajili uliotakiwa ili kuhakikisha wanafikia malengo msimu ujao.