BAADA ya kumalizana na Singida Black Stars, Edward Charles anatajwa kujiunga na Mtibwa Sugar iliyopanda Ligi Kuu Bara msimu huu.
Manyama ambaye alishawahi kukipiga Azam FC aliitumikia Singida Black Stars kwa mkataba wa mwaka mmoja na alijiunga nayo akitokea Azam FC aliyoitumikia kwa misimu miwili.
Chanzo cha kuaminika kutoka Mtibwa Sugar kimeliambia Mwanaspoti kuwa mazungumzo baina ya pande zote mbili yanaendelea vizuri na muda wowote watakapofikia makubaliano beki huyo atasaini mkataba.
“Ni kweli tupo kwenye mazungumzo na mchezaji huyo. Bado hatujafikia makubaliano ya kusaini mkataba, lakini tumefikia hatua nzuri. Mambo yakienda kama tulivyopanga tutamalizana,” alisema mmoja wa watu wa ndani ya Mtibwa na kuongeza:
“Tunatambua umuhimu wa beki huyo kutokana na uzoefu alionao, tunaamini atakuwa sehemu ya mafanikio yetu baada ya kurejea Ligi Kuu. Mikakati yetu ni kuunda kikosi bora na cha ushindani.”
Chanzo ndani ya timu hiyo kinasema hadi sasa viongozi wamefanikiwa asilimia kubwa kuboresha kikosi na wanaamini kitaonyesha ushindani msimu ujao.
Mtibwa Sugar imerejea Ligi Kuu Bara baada ya kushuka daraja msimu wa 2023-24 ambapo imepanda daraja ikitwaa taji la Ligi ya Championship.