Kigogo Prisons afichua mtoko mpya

“PRISONS mpya inakuja.” Ni kauli ya ofisa mtendaji mpya wa Tanzania Prisons, Godfrey Madegwa akieleza namna anavyokwenda kuisuka timu hiyo kwa ajili ya msimu ujao, huku akiwatoa hofu wadau na mashabiki juu ya presha iliyojitokeza msimu uliopita.

Msimu uliopita maafande hao waliponea chupuchupu kushuka Ligi Kuu Bara kufuatia matokeo ya jumla ya mtoano baada ya kushinda mabao 4-2 dhidi ya Fountain Gate na sasa wanajipanga upya na msimu ujao.

Timu hiyo ya Jeshi la Magereza hivi karibuni ilifanya mabadiliko ya uongozi ambapo Madegwa alikabidhiwa nafasi ya katibu mtendaji akirithi mikoba ya John Matei. Kwa upande wa nafasi ya Meneja Oraph Mwamlima alikabidhiwa kiti hicho kilichokuwa chini ya Laurian Mpalile, huku katika benchi la ufundi akipewa Mkenya Zedekiah Otieno kuwa kocha mkuu.

Otieno atasadiwa na Shaaban Mtupa na Dickson Osward aliyekuwa timu ya vijana chini ya miaka 17 na timu hiyo inatarajia kuingia kambini Agosti Mosi, mwaka huu.

Madegwa ameliambia Mwanaspoti kuwa, baada ya kuaminiwa kukabidhiwa nafasi hiyo anakwenda kuibadili timu hiyo na kuondoa presha za kusubiri matokeo dakika za mwisho.

Alisema anafahamu baadhi ya changamoto hasa za uendashaji akieleza kuwa kwa mipango ya mkuu wa jeshi hilo upo mwelekeo mzuri wa kuibadili Prisons kuwa timu yenye ushindani na tishio.

“Kimsingi tunakwenda kushirikiana na wenzetu nje na ndani ya timu kutafuta udhamini na kikubwa ni kuona uendeshaji wa timu unakuwa wa hapahapa Mbeya badala ya kusubiri kila kitu makao makuu Dodoma,” alisema Madegwa na kuongeza:

“Mkuu wa Jeshi nchini ameonyesha dhamira ya kutaka mabadiliko kwa timu hii na sisi tulioaminiwa tunataka kuona ufanisi zaidi. Tutaanza usajili haraka kwa kuzingatia ubora wa mchezaji na mahitaji yetu.”

Kigogo huyo ameongeza kuwa baada ya kumpata kocha mkuu hivi sasa nguvu inaelekezwa kwa wachezaji na ni lazima kuwapo na mabadiliko.

“Wapo wachezaji waliomaliza mikataba tutakaobaki nao lakini wapo tutakaowaacha. Tutafanya usajili mkubwa wenye kukidhi mahitaji ya timu. Tunahitaji Prisons mpya isiyo ya presha,” alisema.

Kuhusu kambi na maandalizi ya msimu ujao kiongozi huyo alisema wanatarajia kuingia kambini Agosti Mosi huko Kiwira au sehemu nyingine itakayopendekezwa na benchi la ufundi.