Dar es Salaam. Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), imeweka hadharani ratiba ya Uchaguzi Mkuu wa Rais, wabunge na madiwani utakaofanyika Oktoba 2025.
Katika ratiba hiyo, Agosti 9, 2025 hadi Agosti 27 utafanyika mchakato wa uchukuaji na ureshaji wa fomu za uteuzi wa wagombea Urais na Makamu wa Rais.
Ratiba hiyo, imewekwa hadharani leo Jumamosi Julai 26, 2025 na Mwenyekiti INEC Jaji wa Rufaa, Jacobs Mwambegele wakati akitoa taarifa za uzinduzi wa ratiba mpya ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025, hafla iliyofanyika jijini Dodoma na kuhudhuriwa na viongozi wa vyama mbalimbali wa vyama vya siasa.
Katika maelezo yake, Jaji Mwambegele amesema Agosti 14, 2025 hadi 27 itakuwa utoaji wa fomu za uteuzi wa wagombea ubunge na udiwani. Wakati Agosti 27, 2025 itakuwa siku ya uteuzi wa wagombea wa Urais na Makamu wa Rais, ubunge na udiwani.
“Agosti 28 hadi Oktoba 28 kampeni zitafanyika za uchaguzi kwa Tanzania bara. Agosti 28, 2025 hadi Oktoba 27 zitafanyika kampeni za uchaguzi Zanzibar ili kupisha kura ya mapema,” amesema.
“Oktoba 29, siku ya Jumatano, itakuwa siku ya uchaguzi mkuu,” amesema Jaji Mwambegele.
Jaji Mwambegele amesema INEC inatoa wito kwa wadau wote wa uchaguzi kujitokeza kushiriki uchaguzi kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu, miongozo na maelekezo yatakayotolewa.