Suza, APRM kushirikiana tafiti kuimarisha utawala bora

Unguja. Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (Suza) kimesaini makubaliano ya ushirikiano na Taasisi ya Mpango wa Hiari wa Kujitathmini kwa vigezo vya Utawala Bora Tanzania (APRM), wenye lengo la kuimarisha tafiti zinazolenga kukuza utawala bora nchini.

Akizungumza leo Jumamosi Julai 26, 2025 Makamu Mkuu wa chuo hicho, Profesa Moh’d Makame Haji amesema chuo hicho kina hazina ya wataalamu waliobobea katika nyanja mbalimbali ambao wanaweza kutoa mchango katika utekelezaji wa malengo ya maendeleo ya Taifa.

Amesema tafiti zitakazofanywa kupitia ushirikiano huo zitazingatia masuala ya soko la ajira, ustawi wa wananchi kwa kulingana na Dira ya Maendeleo ya Taifa ya 2050.

“Elimu na tafiti ni silaha muhimu katika kufanikisha malengo ya Taifa, hivyo Suza itaendelea kupanua wigo wa ushirikiano wake na taasisi mbalimbali ili kuhakikisha inatoa mchango chanya nchini,” amesema.

Kwa upande wake, Katibu Mtendaji wa Taasisi ya APRM Tanzania, Lamau Mpolo amesema imejipanga kuhamasisha utawala bora kwa kushirikiana na taasisi za elimu ya juu, ikiwamo chuo hicho.

Amesema ushirikiano huo utahakikisha tafiti zinazofanyika zinakuwa na tija na kuendana na maeneo yenye uhitaji mkubwa wa kijamii na kiuchumi na wanaamini matokeo ya tafiti hizo yatakuwa yenye kuchochea maendeleo.

“Naupongeza uongozi wa chuo kwa ushirikiano mliouonyesha kwetu, hasa katika mchakato wa maandalizi ya kitabu kinachoangazia mafanikio ya Serikali ya awamu ya sita na ya  nane, kwa JMT na SMZ mtawalia, kwa kuonyesha dhamira ya kweli na mshikamano ambao umesaidia kufanikisha kazi hii,” amesema.

Mpolo amesema kupitia ushirikiano huo, Suza na APRM wanatarajia kuanzisha miradi ya utafiti, warsha na mijadala ya kitaaluma itakayosaidia kuchambua changamoto za kijamii na kiuchumi, pia kubuni sera madhubuti kwa maendeleo ya Taifa.

Utiaji saini makubaliano hayo umetokana na kikao kilichofanyika Machi 27, 2025 katika ofisi za Suza ambao viongozi kutoka taasisi hizo mbili walijadili namna ya kuimarisha ushirikiano katika nyanja za tafiti, elimu na utawala bora.