Morogoro. Mahakama Kuu Kanda ya Morogoro imewahukumu kunyongwa hadi kufa watu watatu, akiwemo dereva wa bodaboda baada ya kutiwa hatiani kwa kosa la mauaji.
Waliohukumiwa adhabu hiyo wametiwa hatiani kwa mauaji ya Christian Tungaraza, aliyekuwa mwalimu mkuu wa Shule ya Msingi Siginali, kwa kumkata na kitu chenye ncha kali sehemu mbalimbali za mwili akiwa nyumbani kwake Mang’ula, wilayani Kilombero.
Adhabu hiyo imetolewa kwa Jovina Mwekya, ambaye ni mke wa marehemu Tungaraza, dereva wa bodaboda, Mussa Mwakyoma na Thadei Mwinuka, mkazi wa Kitongoji cha Lukombe, Kata ya Ludewa mkoani Njombe.
Hukumu ilitolewa Julai 24, 2025 na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Morogoro, Rose Ebrahim baada ya kuridhishwa na ushahidi uliotolewa na upande wa Jamhuri ambao haukuacha shaka katika kuthibitisha shtaka lililokuwa likiwakabili.
Wakati wa usikilizwaji wa kesi, Jamhuri kupitia Wakili wa Serikali, Dastan William ilidai washtakiwa walitenda kosa hilo Juni mosi, 2023 usiku katika Kijiji cha Mang’ula, wilayani Kilombero.
Mshtakiwa wa kwanza katika kesi hiyo ambaye ni Mwekya anadaiwa kula njama na mshtakiwa wa pili (Mwakyoma) ya kumuua Tungaraza na baadaye walimkodi mshtakiwa wa tatu (Mwinuka) kutekeleza mauaji kwa gharama ya Sh500, 000.
Ilidaiwa mahakamani kuwa washtakiwa wa kwanza na wa pili walimpokea mshtakiwa wa tatu na kupanga chumba kwenye nyumba ya wageni, kabla ya usiku kuvamia nyumbani kwa Tungaraza na kumuua.
Baada ya mauaji ilidaiwa mshtakiwa wa tatu alitoroka akarejea Ludewa na baada ya upelelezi wa tukio, alikamatwa na kuunganishiwa kwenye shtaka hilo la mauaji.
Upande wa Jamhuri katika kesi hiyo ulikuwa na mashahidi 14 na vielelezo sita.
Baada ya hukumu kutolewa, Clavery Tungaraza ambaye ni mdogo wa marehemu amesema familia imeridhika na uamuzi wa mahakama.
Amesema maisha bila ya uwepo wa kaka yake yamejaa machungu, simanzi na huzuni ikizingatiwa aliacha watoto watatu.
Happy Sanga, aliyekuwa akifundisha pamoja na Tungaraza amesema hukumu ya mahakama imewapa faraja kwani kifo cha mwalimu huyo kiliacha pengo kwa shule aliyokuwa akifundisha.
Amesema mbali ya kuwa mwalimu alikuwa kama baba na mlezi wa walimu wengi aliowapokea kazini akiwa mwalimu mkuu.