Arusha kinara matukio ya ukatili kwa watu wazima

Dar es Salaam. Mkoa wa kipolisi Arusha umetajwa kuongoza miongoni mwa mitano iliyoripotiwa kuwa na matukio mengi ya ukatili kwa watu wazima.

Hali hiyo ni kwa mujibu wa ripoti za uhalifu na usalama barabarani kuanzia Januari hadi Desemba 2024, iliyochapishwa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS). Kati ya matukio 23,782 yaliyorekodiwa mwaka 2024, mkoa huo una matukio 3,844.

Aina ya matukio ya ukatili yanayotajwa ni lugha chafu, kujeruhi, kushambulia mwili, shambulio la aibu na shambulio la kawaida.

Hali ikiwa hivyo, mkoa huo umeweka mikakati ya kukabiliana na matukio hayo, ikiwamo utekelezaji wa Mpango wa Pili wa kitaifa wa kutokomeza Ukatili wa kijinsia dhidi ya Wanawake na Watoto (Mtakuwa), kwa mujibu wa Ofisa Ustawi wa Jamii wa mkoa huo, Denis Mgiye.

Matukio hayo 23,782 ya ukatili kwa watu wazima mwaka 2024 nchini yameongezeka ikilinganishwa na mwaka 2023 yaliporekediwa 22,147. Ongezeko hilo ni sawa na asilimia 7.4.

Mbali ya Arusha, mkoa wa kipolisi Kinondoni unashika nafasi ya pili kwa matukio 3,466, Tanga 2,043, Temeke 1,892 na Ilala 1,761.

Mgiye anasema katika kukabiliana na matukio hayo wanahakikisha wanaunda, kuhuisha na kusimamia mpango wa Mtakuwa.
“Kamati zipo ngazi ya mtaa, kijiji, kata, wilaya na mkoa na tayari tumezijengea uwezo. Zimekuwa zikitusaidia kuibua na kupokea rufaa katika ngazi ya jamii na kupeleka kwenye vyombo husika,” amesema.

Vilevile amesema vyombo vya usalama husaidia kila anayefanya ukatili anachukuliwa hatua kali za kisheria. Ili kuwasaidia walioathiriwa na ukatili huo, amesema wameanzisha kituo katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Arusha.

“Tumeanzisha kituo cha mkono kwa mkono katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Arusha ya Mount Meru, ukienda pale utakutana na madaktari, wanasheria, wauguzi na polisi wote wakiwa kwenye eneo moja, muathirika wa ukatili atapewa msaada wote wa kisheria na matibabu,” amesema.

Mgiye amesema ukatili huo umechangiwa na mambo mengi, ikiwamo ukosefu wa maadili hasa la watu kutukanana hadharani.
Amesema si watoto pekee wenye changamoto ya maadili, bali hata watu wazima, akitaja ulevi na matumizi ya dawa za kulevya kuwa na mchango katika hali hiyo.

“Ukiangalia Arusha, uvutaji wa bangi ni kama kitu cha kawaida, mtu anakwambia amevuta cha Kisimiri, pia umasikini nao ni tatizo. Wanawake ni waathirika wa matukio ya ukahaba, ubakaji, ndoa za kulazimishwa na kupungua kwa uwajibikaji kwa watu waliopewa ulinzi kwenye jamii,” amesema.

Pia mila kandamizi huwaathiri wanawake, akitoa rai kwa jamii kuwa kufanya hivyo ni kwenda kinyume cha sheria.
“Tumejipanga kuhakikisha wanaofanya matukio haya wanachukuliwa hatua za kisheria na tutatoa taarifa kwa vyombo vya habari kuanzia mwenendo wa kesi na tutakwenda kwenye mtaa ambao mtu alitenda kosa kueleza hatua ambazo Serikali imechukua, hii itatusaidia watu kuacha kutenda makosa hayo,” amesema.

Akizungumzia hilo, Mtetezi wa haki za binadamu, Dk Hellen Kijo-Bisimba amesema matukio hayo yanatokana na watu kutotendeana mema.
Amesema watu wamekuwa wakiishi wakiwa na visasi, hivyo ni muhimu matukio yanayosababisha hali hiyo yamalizwe, ikiwamo watu kupoteza wapendwa wao katika mazingira ya kutatanisha.
“Mkoa wa Arusha unaonekana unaongoza kwa sababu watu wake wanaishi na visasi, ni lazima tuangalie mambo ambayo yanawaathiri, tuyatafutie suluhisho,” amesema.

Mchungaji wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Usharika wa Boay mkoani Manyara, Elieth Mtaita amesema chanzo cha matukio hayo ni watu kumuacha Mungu.
“Watu hawana hofu ya Mungu, hata utamaduni wetu tumeuacha, mzazi anaweza kupigana au kutukana mbele ya watoto, hilo linakwenda kuleta matokeo mabaya kwenye malezi ya watoto, sasa kama baba au mama anapigana au kutukana hadharani, mtoto itakuwaje?” amesema.

Amesema pamoja na kuwa ni katazo la Mungu watu kutenda uovu, kazi kubwa inahitajika kuendelea kueneza neno la Mungu, akisisitiza jamii ifanye wajibu wake kwenye malezi ya watoto.

Kwa upande wake Mtaalamu wa saikolojia, Edwick Mapalala amesema sababu ya kuongezeka kwa matukio ya ukatili kwa watu wazima ni changamoto ya afya ya akili.

“Mtu anapokuwa na msongo wa mawazo ni rahisi kutamka maneno au kufanya jambo linalomuumiza mtu mwingine bila kujali athari ya jambo hilo, ni muhimu kila mtu akifanya jambo atafakari matokeo yake ni nini,” amesema.

Anasema mtu akifanya jambo ili kuendana na mazingira aliyopo bila kuwa na uwezo nao, hivyo hujitengenezea mazingira magumu ya afya ya akili na baadaye kufanya matendo yasiyo sahihi.
“Ukiangalia upande wa ndoa, vijana hawana uvumilivu, wakigombana kidogo wanafikiria kupigana na kuachana, siyo kutatua tatizo, tunapaswa kutawaliwa na hofu ya Mungu na kufuata mila zetu za asili ili kuendelea kuheshimiana na kuoneana huruma,” amesema.

Kwa mujibu wa Shirika la Wanawake katika Sheria na Maendeleo Barani Afrika (WiLDAF) ukatili husababishwa na mambo mbalimbali ukiwamo umasikini, mfumo dume, maandiko ya vitabu vya dini, ulevi, ushirikina, imani potofu, mahari, mila mbovu, wivu wa kimapenzi, sheria mbovu, sera na elimu duni.