INEC yapuliza kipenga uchaguzi mkuu

Dodoma/Dar. Wakati Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), imeweka hadharani kalenda ya uchaguzi mkuu wa Rais, wabunge na madiwani kwa mwaka 2025, wadau wa siasa nchini wamesema ni muhimu ikafuatwa na kila chama kipewe haki kwa mujibu wa sheria.

Wamesema uwepo wa kalenda ya uchaguzi unawaweka katika nafasi nzuri ya kushiriki mchakato huo, kwani awali walifanya mambo pasipo kuwa na uhakika wa kipi kitafanyika lini.

Kwa mujibu wa ratiba ya Tume iliyowekwa hadharani leo Julai 26, Uchaguzi Mkuu utafanyika Jumatano Oktoba 29, 2025 ukiwashirikisha wapigakura 37,655,559.

Ratiba hiyo imetolewa jijini Dodoma na Mwenyekiti INEC, Jaji Jacobs Mwambegele mbele ya viongozi wa vyama 18 vya siasa vinavyoshiriki uchaguzi mkuu huo, isipokuwa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), ambacho kilishaweka wazi kuwa hakitashiriki bila kufanyika marekebisho ya mifumo ya uchaguzi.

Kwa mujibu wa ratiba hiyo mchakato wa uchukuaji na urejeshaji fomu za uteuzi wa wagombea Urais na Makamu wa Rais utafanyika Agosti 9, 2025 hadi Agosti 27.

Jaji Mwambegele amesema Agosti 14 hadi 27 Tume itatoa fomu za uteuzi wa wagombea ubunge na udiwani, wakati Agosti 27, 2025 itakuwa siku ya uteuzi wa wagombea wa Urais na Makamu wa Rais, ubunge na udiwani.

Jaji Mwambegele amesema: “Agosti 28 hadi Oktoba 28 kampeni za uchaguzi kwa Tanzania Bara zitafanyika. Agosti 28, 2025 hadi Oktoba 27 zitafanyika kampeni za uchaguzi Zanzibar ili kupisha kura ya mapema,” amesema na kuongeza:

“Oktoba 29, siku ya Jumatano, itakuwa siku ya uchaguzi mkuu.”

Jaji Mwambegele amesema INEC inatoa wito kwa wadau wote wa uchaguzi kujitokeza kushiriki uchaguzi kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu, miongozo na maelekezo yatakayotolewa.

INEC imesema jumla ya watu milioni 37.65 wamejiandikisha kupiga kura katika uchaguzi huo idadi yao ikiwa imeongezeka kwa asilimia 26.55 huku vituo vya kupigia kura vikipaa kwa asilimia 22.49

Tume imefafanua kati ya wapigakura hao, milioni 36.65 wapo Tanzania Bara na 1,004,627 wapo Zanzibar. Idadi hiyo ni sawa na ongezeko la asilimia 26.55 kutoka idadi ya wapigakura milioni 29.75 waliokuwa katika Daftari la Kudumu la Wapigakura mwaka 2020.

“Kati ya wapigakura milioni 37.65, wanawake ni milioni 18.94 sawa na asilimia 50.31 na wapigakura milioni 18.71 ni wanaume sawa na asilimia 49.69, wakati wapigakura 49,174 ni watu wenye ulemavu,” amesema.

Jaji Mwambegele amesema jumla ya vituo 99,911 vitatumika katika kupiga kura katika uchaguzi huo.

“Vituo 97,349 vitatumika kupigia kura Tanzania Bara na vituo 2,562 vitumika Zanzibar. Idadi hiyo ni sawa na ongezeko la asilimia 22.49 ya vituo 81,567 vilivyotumika katika uchaguzi mkuu wa 2020,” amesema.

Kuhusu wapigakura wapya amesema watu milioni 7.64 wamejiandikisha katika Daftari la Kudumu la Wapigakura.

Amesema idadi hiyo ni sawa na asilimia 136.79 ya makadirio ya awali ambayo yalikuwa ni kuandikisha watu milioni 5.58, sawa na asilimia 18.77 ya wapigakura wote walioandikishwa mwaka 2019/2020.

Vilevile amesema wapigakura milioni 4.29 wameboresha taarifa zao kwenye daftari hilo, sawa na asilimia 98.23 ya makadirio yaliyokuwa milioni 4.36 ya wapigakura wote walioandikishwa 2019/2020.

“Wapigakura 99,744 wameondolewa katika daftari kwa kupoteza sifa, sawa na asilimia 16.78 ya makadirio ya awali yaliyokuwa zaidi ya watu 500,000,” amesema.

Kibano waliojiandikisha zaidi

Mwenyekiti huyo amesema wapigakura 8,703 wamebainika kujiandikisha zaidi ya mara moja, akisema baada ya hafla hiyo, Mkurugenzi wa Uchaguzi, Ramadhani Kailima atakabidhi orodha hiyo kwa Jeshi la Polisi kwa hatua za kisheria, kwa mujibu wa kifungu cha 114 cha Sheria ya Uchaguzi wa Rais, wabunge na madiwani ya mwaka 2024.

Baadaye Kailima amekabidhi kwa Polisi nakala ngumu na nakala tete ya majina hayo akisema watu wa aina hiyo wamevunja sheria kwa mujibu wa miongozo.

Amesema Watanzania hao wamechukuliwa picha, alama za vidole, vituo walivyojiandikisha na namba za simu, jambo linalokwenda kuwarahisishia Polisi katika kuwatambua.

Mwakilishi wa Jeshi la Polisi makao makuu aliyehudhuria uzinduzi huo wa kalenda ya INEC, hakuwa tayari kueleza ni nini kitafuata kwa watu hao.

Katika uzinduzi huo uliobeba kaulimbiu: “Kura yako ni haki yako, jitokeze kupiga kura”, Jaji Mwambegele amesema maandalizi yote yamekamilika kwa asilimia 100 na kwamba, kila hatua na kila kilichofanyika kilihitaji fedha ambazo kwa asilimia 100 zimetolewa na Serikali ya Tanzania.

Katibu Mkuu wa Chama cha NCCR- Mageuzi, Evaline Munisi amesema uzinduzi wa kalenda hiyo unakwenda kuwaweka mahali pazuri, kwani walishindwa kuweka mipango yao sawa katika kuelekea ushindi kutokana na kutokujua lini wanatakiwa kufanya nini.

Munisi ameiomba INEC kusimamia kile walichokubaliana na kilichopangwa ili kutovuruga mchakato, kwani anayetakiwa kushinda anatakiwa kushinda kihalali na asiyestahili basi iwaache wananchi wamkatae.

“Kikubwa tunasisitiza suala la amani na utulivu katika kipindi hicho, wenzetu Tume tungewaomba wajali kalenda ya uchaguzi kama walivyoiwasilisha na kwa namna yoyote sisi hatuwezi kulalamika ikiwa kama tutakwenda kama walivyotupangia, kwani tumejipanga na karibu majimbo 200 tumeshamaliza kufanya uteuzi,” amesema.

Katibu Mkuu wa Chaumma, Salum Mwalimu amesema ndani ya saa 72 chama hicho kitakuwa kimetoa kalenda yake ya matukio, kwani hakikuweza kufanya hivyo awali kwa kuwa walikuwa wanasubiri kuona kalenda ya INEC ilivyo.

Mwalimu amesema hakuna shida yoyote kuhusu kalenda hiyo, wameona inawezekana na muda uliotolewa kwa chama kilichojipanga hakiwezi kushindwa kufanya mambo makubwa, wala kukuingia kwenye uchaguzi na kutoa ushindani wa kushinda majimbo na urais.

Amesisitiza uchaguzi ufuate kalenda na kila chama kipewe haki kwa mujibu wa sheria bila ya kuegemea upande.

Mwalimu amesema wanaunga mkono kwani kila jambo lililofanyika linaonekana kuwa na baraka za vyama ambavyo vilishirikishwa tangu mwanzo wa mchakato.

Katibu wa ACT-Wazalendo, Ado Shaibu amesema Agosti 6, 2025 chama hicho kinakwenda kukamilisha mpango na mkakati wake katika uchaguzi na kuwa watampata mgombea urais baada ya michakato mingine kuwa imekamilika.

Amesema kalenda ya uchaguzi ilikuwa muhimu kwao ili waweke mambo vizuri, na kuwa awali walikuwa wanakisia juu ya lini na nini kinakwenda kufanyika kwa wakati gani, ndiyo maana walikuwa wametulia na kuendelea na michakato ya chinichini.