Ridhiwani aeleza tatizo la vijana kwenye mikopo

Dar es Salaam. Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Ridhiwani Kikwete amezitaka taasisi za kifedha kuwajengea uwezo vijana ili wawe na sifa ya kukopesheka, akisema tatizo la vijana wengi nchini ni kukosa nidhamu ya fedha.

Amesema kijana anapopata fedha hutumia nje ya malengo kusudiwa kutokana na kukosa nidhamu ya fedha hizo, na kama hawatapata elimu ya mikopo ni ngumu wakopaji wapya kuongezeka kwenye taasisi za fedha, badala yake watajirudia walewale wanaokopa kila wakati.

Waziri huyo ametoa kauli hiyo Julai 25, 2025 jijini Dar es Salaam wakati akizindua Jukwaa la Biashara na Maendeleo (NEDC), ambalo linalolenga kuunganisha nguvu ya sekta binafsi, vijana na Serikali katika kuchangamkia fursa zilizopo nchini.

“Taasisi za kifedha jaribuni kuangalia namna ya kuelekeza vijana namna ya kukopa, tunaweza kupiga kelele lakini watakaoendelea kwenda kukopa ni sisi. Hawa vijana waliopo mtaani wataendelea kuhangaika na kinachowakwamisha ni elimu ya namna gani wanaweza kujiandaa na kutoa maneno kwamba wanakopesheka,” amesema.

Waziri Kikwete amesema pamoja na elimu ndogo ya mikopo kwa vijana, riba zilizopo kwenye mikopo bado ni kikwazo kwa vijana kutomudu masharti yake huku Serikali kupitia Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi 2025-2030, imeweka mikakati ya kuwezesha vijana na wajasiriamali kupata mikopo kwa urahisi.

Mwanzilishi wa Jukwaa la NEDC, Jesse Madanda amesema moja ya programu ya umahiri ya  jukwaa hilo ni Bongo Fursa, ambayo inalenga kuvumbua, kulea na kuibua vipaji vya ubunifu.

“Kupitia Bongo Fursa tutazindua mashindano ya kitaifa, maonyesha ya kibiashara, warsha na mafunzo maalumu yatakayochochea kiwango cha ubunifu katika Taifa letu, programu hii inalenga kuvumbua vijana na kuwawezesha,”

Amesema kaulimbinu yao ni Kuunganisha Biashara, Wawekezaji na Serikali kwa Maendeleo Endelevu ikiwa ni dhamira yao kufikia vijana wengi kuwa na uchumi imara kama ilivyoainishwa kwenye Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB Foundation, Tully Mwambapa amesema katika juhudi za benki hiyo kuwezesha vijana wenye biashara changa, Sh7 bilioni zimetolewa katika uwezeshaji wa vijana.

Mwambapa amesema kabla ya kijana kupewa mkopo hufuatiliwa tabia yake na kama mtu ana historia ya kuchukua mkopo kwa muda mrefu bila kurejesha, anakosa sifa ya kukopesheka.

Kwa upande wake Edwin Urassa kutoka Taasisi ya Creditidiinfo Tanzania Limited  inayojishulisha na masuala ya mikopo amesema mikopo mingi inayokopwa na vijana ni midogo midogo.

Mikopo hiyo ni kuanzia Sh1 milioni kushuka chini na nyingi ni kupitia simu za mkononi na tangu 2017 hadi sasa vijana waliokopa mikopo ni milioni 13 kati yao milioni 10 walikopa mikopo midogo.

“Taarifa za mikopo ambazo tunahifadhi za mikopo benki yeyote inaweza kutumia kama historia ya mtu na tabia yake kwenye ukopaji, kama ni mrejeshaji mzuri anaweza kupata sifa ya juu ya kuendelea kukopa na kama mtu anasumbua kwenye marejesho anakosa sifa ya kukopesheka,” amesema.