Ramovic achomoa mtu Yanga | Mwanaspoti

Pale Yanga kuna watu wa maana kabisa, kwani kila kocha aliyeifundisha timu hiyo misimu ya karibuni na kuondoka, amesepa akiwa na vichwa ambavyo kokote atakakokwenda anatamani kupiga navyo kazi.

Alianza Nasrredine Nabi aliyepo Kaizer Chiefs kwa sasa, Miguel Gamondi yupo Singida Black Stars aliyefuatiwa na Sead Ramovic anayeinoa CR Belouizdad kisha Miloud Hamdi aliyepo Ismailia ya Misri akimpisha Romain Folz aliyetua hivi karibuni akitarajiwa kuinoa msimu ujao.

Lakini, kila kocha aliyesepa ameondoka na majina ya wachezaji au watalaamu wa benchi la ufundi ambao angetamani huko aliko apige nao kazi.

Taarifa ikufikie kwamba mkurugenzi wa ufundi wa Yanga, Abdihamid Moallin huenda akaachana na kikosi hicho, huku taarifa zikieleza mabosi wa Algeria, CR Belouizdad wanamuhitaji kwa lengo la kuungana tena na Mjerumani, Sead Ramovic.

Taarifa ambazo Mwanaspoti imezipata, zinaeleza Ramovic aliyejiunga na Yanga Novemba 15, 2024, kisha kuondoka Februari 4, 2025, kwa makubaliano ya pande mbili na kutua CR Belouizdad, amependekeza kufanya kazi Moallin katika kikosi hicho cha Algeria.

Sababu za kuondoka kwa Moallin ni kutokana na kile kinachoelezwa kocha mpya wa Yanga raia wa Ufaransa, Romain Folz anaunda upya benchi la ufundi la kikosi hicho, ambapo tayari mbadala wake inadaiwa ni Msauzi, Paul Matthews.

Matthews inadaiwa ameachana na SuperSport United ya kwao Afrika Kusini ambayo kwa sasa inajulikana kwa jina la Siwelele FC, ambapo taarifa zinaeleza ndiye anayekuja Yanga kwa ajili ya kuchukua nafasi ya Moallin anayeweza kuondoka kikosini.

Moallin aliyewahi kuifundisha Azam FC, alijiunga na Yanga Novemba 18, 2024, akitokea KMC aliyoachana nayo Novemba 11, 2024, kwa makubaliano ya pande mbili, baada ya kuiongoza katika mechi 11, za Ligi Kuu Bara kwa msimu uliopita 2024-2025.

Katika mechi hizo 11, ambazo Moallin aliiongoza KMC, alishinda nne, sare mbili na kupoteza tano akiiacha nafasi ya saba na pointi 14.

Kabla ya Moallin kushika nyadhifa hiyo ya Mkurugenzi wa Ufundi wa Yanga, mtu wa mwisho alikuwa ni Kocha Mholanzi, Hans Van Der Pluijm, wakati ikiwa inafundishwa na Mzambia George Lwandamina kipindi cha uongozi wa bilionea marehemu Yusuf Manji.

Moallin ni pendekezo la Ramovic katika kikosi cha CR Belouizdad, ambapo Mwanaspoti limedokezwa mazungumzo baina ya pande zote mbili kati yao yanaendelea na muda wowote kocha huyo anaweza kuondoka Yanga na kujiunga na miamba hiyo ya Algeria.