Mrithi wa Shomary huyu hapa!

UONGOZI wa KMC FC, uko katika mazungumzo ya kuipata saini ya beki wa kushoto wa kikosi cha Tanzania Prisons, Samson Mwaituka, kwa lengo la kuchukua nafasi ya Rahim Shomary aliyejiunga na Ghazl El Mahalla ya Misri.

Samson alionyesha uwezo mkubwa na timu hiyo ya maafande kwa msimu wa 2024-2025, baada ya kuaminiwa kikosi cha kwanza na aliyekuwa Kocha, Mbwana Makata na baadaye Amani Josiah, ambapo kwa sasa amekuwa lulu sokoni na kuanza mazungumzo na KMC.

Beki huyo amemaliza mkataba na Prisons na hadi sasa hakuna mazungumzo ya kuongeza mwingine, baada ya kuweka wazi yupo tayari kwa changamoto mpya, huku ikielezwa viongozi wa KMC wanamuona ni beki sahihi atakayezipa vyema nafasi ya, Rahim.

Rahim ni miongoni mwa nyota walioonyesha uwezo mkubwa akiwa na kikosi cha KMC, huku msimu wa 2023-2024 wa Ligi Kuu Bara, akichaguliwa kuwa mchezaji bora chipukizi katika Ligi Kuu Bara, akiwashinda Semfuko Charles wa Coastal Union na Constantine Malimi wa Geita Gold.

Akizungumza na Mwanaspoti, Ofisa Mtendaji Mkuu wa KMC, Daniel Mwakasungula alisema tayari wamekamilisha baadhi ya sajili kwa ajili ya msimu ujao, ingawa sio muda muafaka kuwatangaza, hadi pale watakapokamilisha taratibu zilizobaki.

“Tutaanza kuwatambulisha pale tutakapoona ni muda sahihi wa kuwatangaza, ni kweli tumekamilisha baadhi na tunaendelea na wengine kutokana na mapendekezo ya benchi letu la ufundi, hivyo mashabiki wetu wawe tu na subra,” alisema Mwakasungula.

KMC itakayonolewa msimu ujao na aliyekuwa Kocha wa Yanga na timu ya taifa ya Tanzania, Mbrazili Marcio Maximo, tayari inaendelea na maboresho makubwa ya kikosi hicho ambapo hadi sasa imemsajili winga, Erick Mwijage kutokea Kagera Sugar.