Mmoja afariki, 11 wajeruhiwa wakitoka kwenye sherehe Kilimanjaro

Moshi. Mtu mmoja anayedaiwa kuwa ni mtawa wa Kanisa Katoliki, amefariki dunia huku wengine 11 wakijeruhiwa baada ya gari walilokuwa wakisafiria kuligonga gari jingine kwa nyuma wakati wakitoka kwenye sherehe.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa amethibitisha kutokea kwa ajali hiyo ambayo amesema ilitokea jana Julai 25, 2025 saa 1:20 usiku katika eneo la Kwa Frank, Kata ya Masama, Wilaya ya Hai, mkoani Kilimanjaro.

Kamanda Maigwa amesema chanzo cha ajali hiyo ni uzembe wa dereva ambaye alikuwa akiendesha gari hilo akiwa amelewa, ambapo kwa sasa anashikiliwa na Jeshi la Polisi.

“Jeshi la Polisi mkoani Kilimanjaro linamshikilia dereva aitwae Saimon Pauli (29) mkazi wa Emaus Sanya juu aliyekuwa akiendesha gari aina ya Toyota Haice, kwa kuligonga gari jingine kwa nyuma ambalo halijafahamika usajili wake na kusababisha kifo cha mtu mmoja na majeruhi 11,” amesema Kamanda Maigwa na kuongeza;

“Uchunguzi wa awali umebaini chanzo cha ajali hiyo ni uzembe wa dereva aliyekuwa akiendesha gari hilo akiwa amelewa, na kusababisha kupoteza umakini barabarani na matokeo yake kuligonga gari hilo kwa nyuma ambalo halijafahamika.”

Aidha, Kamanda Maigwa amesema majeruhi 10 wanaendelea na matibabu katika hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Kilimanjaro Mawenzi na majeruhi mmoja anatibiwa katika Hospitali ya Wilaya ya Hai.

Amesema mwili wa marehemu umetambuliwa na umehifadhiwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mawenzi kusubiri uchunguzi na taratibu nyingine za mazishi.

Ajali hiyo imetokea ikiwa zimepita siku 28 toka itokee ajali nyingine katika Wilaya ya Same iliyosababisha vifo vya watu 42 na majeruhi 28 baada ya basi kampuni ya Chanel One lililokuwa likitokea Moshi kwenda Tanga, kugongana uso kwa uso na basi dogo aina ya Coaster lililokuwa likitokea Same mjini kwenda Moshi na kuwaka moto wakati abiria wakiwa ndani ya magari hayo.