Dar es Salaam. Mwili wa Dk Hassy Kitine, aliyewahi kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Usalama wa Taifa (TISS) umezikwa, huku waombolezaji wakieleza watakayoyakumbuka kutoka kwake, ukiwamo uzalendo wake kwa Taifa.
Dk Kitine (82) aliyefariki dunia akiwa usingizini usiku wa kuamkia Julai 25, 2025 akiwa nyumbani kwake Oysterbay, amezikwa leo Julai 26 katika makaburi ya Kisutu, Dar es Salaam.
Waziri Mkuu wa zamani Jaji Joseph Warioba amemtaja Dk Kitine kama kiongozi mzalendo aliyesaidia Taifa kuvuka wakati mgumu kwa kuwezesha viongozi wa wakati huo kupata taarifa sahihi.

Amesema alisaidia Serikali na nchi kupata taarifa sahihi ili uamuzi sahihi ufanyike.
“Wakati anaongoza alikuwa na vijana wenzake wengi wametangulia mbele ya haki, wale vijana walifanya kazi vizuri kumsaidia Mwalimu (hayati Julius Nyerere) na Serikali kupata taarifa sahihi na uamuzi sahihi ufanyike,” amesema.
Katika uchaguzi wa mwaka 1995 inadaiwa siku chache kabla ya uteuzi wa mgombea urais kupitia CCM, Dk Kitine alimwendea Mwalimu Nyerere nyumbani kwake Msasani na kumweleza kuwa hakuna mgombea aliyestahili kutokana na migawanyiko ya makundi ndani ya chama.

Inadaiwa alipoombwa amtaje mtu anayemuona anabebeka, Dk Kitine alimtaja Benjamin Mkapa, aliyekuwa Waziri wa Sayansi, Teknolojia na Elimu ya Juu wakati huo, aliyemuona kuwa hakuwa na migawanyiko ya kikundi na alikuwa na historia safi, tofauti na wagombea wengine.
Jaji Warioba amesema Dk Kitine alikuwa mzalendo aliyeipenda nchi yake. Amesema walipozungumza naye kabla hajapata maradhi ya utu uzima alikuwa akimweleza anatamani warejee kwenye hali ya uzalendo na uaminifu kwa nchi.

Amesema Dk Kitine alitumikia nchi kwa uwezo wake wote, hivyo ni muhimu Watanzania kusherekea maisha yake duniani.
Mufti na Sheikh Mkuu wa Tanzania, Abubakary Zubeiry amesema wanadamu wanapaswa kufahamu dunia si pahala pa kufanyia mchezo bali kufanyia kazi.
“Tujenge amani, utulivu na kupendana, tuondoe chuki. Mtume (S.A.W) anasema watu wanapokuwa wamefanya jambo jema watakuwa watu wa peponi, watakapokuwa wanakwenda peponi milango inafunguka. Kwa wale ambao wanagombana milango itafunga,” amesema.
Amesema Dk Kitine kwa namna alivyoishi kila mtu anaweza kuelezea maisha yake mema duniani, akihimiza Watanzania wanapaswa kusherekea maisha yake mema aliyoishi.

Mwakilishi Ofisi ya Rais (hakutaka kutaja jina), amesema Dk Kitine alikuwa kiongozi mzalendo na alihudumu kama Mkurugenzi wa Idara ya Usalama wa Taifa katika wakati mgumu.
“1980 tunafahamu nchi yetu ilikuwa katika wakati gani, aliweza kushirikiana na taasisi zingine kuivusha nchi salama, alikuwa mzalendo na mchapakazi na alionyesha ushirikiano mkubwa kwa wafanyakazi wenzake,” amesema.
Ibrahimu Kitine mtoto wa Dk Kitine amesema wasifu wa baba yake akisema alizaliwa mwaka 1943, huku akieleza alikosoma ndani na nje ya na nchi hadi alipoteuliwa kushika wadhifa wa kuongoza TISS.