Vikundi 440 vimepewa mkopo na Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam

Zaidi ya vikundi 440 kati ya vikundi 945 vilivyoomba mikopo ya asilimia kumi katika halmashauri ya jiji la Ilala, Mkoani Dar es salaam vyenye sifa vinatarajia kuanza kupokea fedha ndani ya siku saba.

Haya yamesemwa na Mkuu wa Wilaa ya Ilala, Edward Mpogolo, katika kongamano la Uelimishaji kwa vikundi juu ya mikopo ya asilimia kumi, kupitia mfumo jumuishi.

Akizungumza na vikundi mbalimbali vya wanawake wa kata 36, wilayani Ilala, Mpogolo amebainisha kuwa zaidi ya shilingi bilioni kumi na nane zinatolewa katika mikopo ya asilimia kumi ya Jiji kwa kundi la wanawake, vijana na walemavu.

Mpogolo, ameeleza kuwa utolewaji wa mikopo hiyo kwa vikundi hivyo utakuwa shirikishi na uwazi kwa waombaji na bank zinazotoa kulingana na utaratibu mpya mara baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kuruhusu mikopo hiyo kutolewa kwa utaratibu mzuri wa kuomba, kuhakikiwa na kukopeshwa mikopo hiyo.

Mkuu huyo wa wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo amewahakikishia vikundi vyote vilivyoomba vitapata mikopo kutoka na halmashauri hiyo ya jiji kuwa na mtaji wa kutosha wa kiasi cha shilingi bilioni 35 ambazo ziko katika mzunguko toka kuanza kutolewa kwa mikopo hiyo kwa awamu ya kwanza ya bilioni 17 na sasa ni bilioni 18.

Fedha ambazo zinatarajiwa kuongezeka hadi kufikia bilioni 60 kwa miaka miwili, kutokaba na marejesho ya mikopo iliyokatika mzunguko na kuyataka makundi hayo kutosita kuomba mikopo ya asilimia kumi ambayo haina riba na ni njia kuu ya kujikwamua kiuchumi.

Aidha kufuatia elimu iliyotolewa na taasisi za kibank zenye dhamana ya kukopesha mikopo hiyo, Mpogolo amewataka wanawake kuacha kwenda kukopa katika taasisi zenye ulaghai ambazo nyingi uwaingiza katika matatizo ya kiuchumi, familia na kuwaacha masikini.

Kwa upande wake Katibu tawala wilaya ya Ilala, Charangwa Suleiman amebainisha changamoto zilizojitokeza na kusababisha vikundi vingi kuchelewa kupata mikopo ni kutokana na dhana ya biashara ya kikundi kukosa uhalisia wa fedha wanazoomba, uzoefu wa biashara na ukweli.

Aidha katika kongamano ilo wanawake kutoka vikundi mbalimbali wamepongeza na kumshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kurudisha tena mikopo hiyo kwa makundi ya wanawake, vijana na walemavu.