Afisa Elimu Dar ashangazwa na wanafunzi St Anne Marie Academy wanavyomudu kifaransa

Na Mwandishi Wetu

SERIKALI imeahidi kuendelea kushirikiana na sekta binafsi katika elimu huku ikiipongeza shule ya St Anne Marie Academy ya jijini Dar es Salaam kwa kufanya vizuri kwenye matokeo ya mitihani ya kitaifa.

Pongezi hizo zimetolewa leo jijini Dar es Salaam na Afisa Elimu wa Mkoa wa Dar es Salaam Gift Kyando wakati wa mahafali ya darasa la saba yaliyofanyika kwenye viwanja vya shule hiyo Mbezi Kimara kwa Msuguri.

Alisema amefurahishwa na mazingira mazuri ya shule baada ya kutembelea maeneo mbalimbali ya shule hiyo na kuridhishwa pia na namna maktaba zilivyoboreshwa na kuwekwa vitabu vya kila aina kuwawezesha wanafunzi kupata maarifa wanayotaka.

“Waswahili wanasema tembea uone, mimi leo nimejionea mwenyewe kwa macho yangu namna St Anne Marie Academy ilivyoboresha mazingira ya shule kwa kupanda miti ya kutosha, bustani za mboga mboga na matunda kiasi kwamba mnajitosheleza wenyewe kwa mboga mboga na matunda, naomba wengine nao waige kutoka kwenu,” alisema

Alimpongeza Mkurugenzi wa shule hizo, Dk Jasson Rweikiza kwa uwekezaji mkubwa alioufanya kwenye shule zake na kuajiri walimu na watumishi wengi hali ambayo imesaidia kupunguza tatizo la ajira nchini.

Alisema uwekezaji mkubwa unaofanywa na sekta binafsi kwenye elimu umekuwa na manufaa makubwa kwa serikali kwani haiwezi kuhudumia watanzania wote peke yake.

“Nimeambiwa pia kuwa hapa wanafunzi wanakula milo mitano, hili siyo jambo la kawaida na ndiyo maana hata ukiwaona watoto wanaosoma hapa wanasiha njema kabisa, “

Kyando aliziomba shule binafsi nchini ikiwemo St Anne Marie Academy kuendelea kutoa elimu bora lakini kwa kuwatoza ada himilivu watanzania ili watu wengi wenye kipato cha wastani nao wapate fursa ya kusomesha watoto wao na kuwa msaada kwa taifa.

“Rweikiza serikali inakupongeza sana, nimeelezwa kuhusu ufaulu wa shule yako nimevutiwa sana kwa namna mnavyofanya vizuri kwenye matokeo ya kuanzia wilaya, mkoa na kitaifa, nina miaka miwili tangu nije kufanya kazi Dar es Salaam na sijawaji kuhudhuria mahafali ya shule ya msingi yenu ni ya kwanza,” alisema

Vile vile Kyando alielezea kushangazwa kwake kwa namna wanafunzi wa shule hiyo wanavyomudu kuzungumza kwa ufasaha lugha ya kifaransa na namna walivyoielezea filamu ya Royal Tour iliyochezwa na Rais Samia Suluhu Hassan.

“Kwa dunia ya leo kadri mtu anavyojua lugha nyingi ndivyo anapokuwa na fursa nyingi sana za ajira maeneo mbalimbali duniani, nimesikia wanafunzi walivyoielezea Royal Tour kwa kifaransa imenivutia sana wazazi lazima mjipongeze kwa kuwaleta watoto sehemu sahihi,” alisema

Mkurugenzi wa shule hiyoo, Dk Jasson Rweikiza alisema ataendelea kuboresha mazingira ya shule hiyo ili kuwawezesha wanafunzi kuendelea kufanya vizuri kwenye mitihani yao ya kitaifa.

Alisema shule hiyo imekuwa ikifanya vizuri kwenye mitihani ya kitaifa kutokana na mkakati kabambe waliojiwekea ikiwemo kuwaondolea walimu jukumu la kutunga mitihani yao ya ndani.

Alisema wameunda bodi ya mitihani ambayo kazi yake ni kuhakikisha inatunga mitihani kulingana na silabasi na walimu wa shule hiyo wamebaki na kazi moja tu ya kufundisha.

Dk Rweikiza alisema mwanafunzi wa shule hiyo atakayefiwa na mzazi anayelipa ada hatasimamishwa masomo na badala yake ataendelea kusoma hadi atakapomaliza

“Kama atafiwa na mzazi akiwa darasa la kwanza basi ataendelea mpaka amalize darasa la saba na kama yuko kidato cha kwanza basi ataachwa amalize hadi kidato cha nne bila kulipa ada,” alisema Dk Rweikiza