Dar/Mikoani. Mzigo wa kuamua kina nani wanastahili kupigiwa kura za maoni kutafuta wa kupeperusha bendera ya Chama cha Mapinduzi (CCM) katika nafasi ya ubunge na uwakilishi umerejeshwa kwa wajumbe, baada ya chama hicho kufanya marekebisho madogo ya katiba yake.
Marekebisho hayo katika Ibara ya 103(7) f, sasa yanaipa kamati kuu wigo mpana wa kufikiria na kupendekeza idadi ya watiania kwa kadri itakavyoona inafaa, kwa ajili ya wajumbe kupiga kura za maoni, badala ya utaratibu wa awali uliokilazimu kikao hicho kupendekeza wagombea watatu pekee.
Hatua hiyo inapunguza hofu ya watiania kuhusu idadi ndogo ya majina yatakayorudi kutoka kamati kuu, huku ikiamsha wasiwasi mpya wa kuwashawishi wajumbe wapige kura zitakazomtosha mtiania kuonekana anafaa kupeperusha bendera ya CCM Oktoba 29, 2025.
Pamoja na mabadiliko hayo, watiania vijana wa nafasi mbalimbali za dola kwa tiketi ya CCM, wapo katika nafasi nzuri ya kupenya kwenye michakato hiyo kutokana na kile kilichoelezwa, kuwa ndilo kundi litakalopewa kipaumbele zaidi katika teuzi.
Kauli hiyo ya furaha kwa vijana, inaweza kuzima matumaini ya wale waliouvuka ujana, nab ado wanawania nafasi mbalimbali kupitia chama hicho.
Hayo yamefikiwa leo Jumamosi Julai 26, 2025 katika Mkutano Mkuu Maalumu wa CCM Taifa, uliofanyika kwa mara ya kwanza kwa njia ya mtandao, ukihudhuriwa na wajumbe 1,915 kutoka mikoa na wilaya zote za Tanzania Bara na Zanzibar.

Katika mkutano huo uliokuwa na ajenda moja ya marekebisho madogo ya katiba, Mwenyekiti wa CCM, Rais Samia Suluhu Hassan alishiriki kikao hicho akiwa pamoja na wajumbe wa Kamati Kuu na Halmashauri Kuu (NEC), katika ukumbi wa ‘White House’ makao makuu ya chama hicho, jijini Dodoma.
Wajumbe wa mkutano huo katika kila wilaya walishiriki kwa mtandao wa zoom wakiwa ofisi za wilaya za CCM. Wakati wa upigaji kura, makatibu wa wilaya walisimamia shughuli hiyo, na kisha kutoa matokeo kwa awamu.
Samia aliwaomba wajumbe waridhie mabadiliko hayo akisema ni kuruhusu katiba iipe kamati kuu mamlaka ya kufikiria na kupendekeza idadi ya watiania kwa kadri itakavyoona inafaa kwa ajili ya kupigiwa kura za maoni, badala ya majina matatu pekee kama ilivyokuwa awali.

Amesema wameamua kuomba mabadiliko hayo, kutokana na uhalisia wa idadi kubwa ya makada wa CCM waliojitokeza kuomba ridhaa ya nafasi mbalimbali, hivyo majina yatarudi zaidi ya matatu kwa namna kamati kuu itakavyoona inafaa.
“Kuna maeneo yana wagombea wengi hadi 3,940, kwa hiyo tumeona kwenda na watatu kati ya watu wengi hao si jambo la busara. Lakini papo hapo kamati kuu imebanwa na katiba, hatuwezi kuongeza majina,” amesema na kuongeza:
“Kwa hiyo, tumeamua kurudi kwenu kuomba ridhaa ya kubadilisha katiba kuongeza maneno… ‘kama kamati kuu itakavyoona inafaa’,” amesema.
“Tumerudi kwenu kuomba tuongeze maneno kwenye katiba kwamba kama kamati kuu itaona inafaa. Tumerudi kwenu kuomba ridhaa ya hilo na sasa tunataka jambo lijadiliwe,” amesema.
Baada ya ombi hilo, Rais Samia amewataka wajumbe wapige kura za maoni katika kila wilaya kisha zijumuishwe na kuhesabiwa, iwapo wamekubali au vinginevyo.
Katika kura hizo, wajumbe 1,912 sawa na asilimia 99.8 wa mkutano huo wamepiga kura ya ndiyo kukubaliana na utaratibu huo.
Katika kura hizo, tatu ziliharibika na wajumbe 16 hawakuhudhuria mkutano huo, hivyo kura za jumla zilizokubali marekebisho hayo ni 1,915 sawa na asilimia 99.8.
Awali, akizungumzia mabadiliko hayo, Katibu wa NEC, Oganaizesheni ya chama hicho, Issa Gavu amesema kwa mazingira maalumu chama hicho kinalazimika kufanya mabadiliko hayo madogo.

“Kwa mazingira maalumu yanayopelekea kusudio la kuleta majina zaidi ya matatu ya wagombea ubunge na ujumbe wa Baraza la Wawakilishi, chama kinalazimika kufanya mabadiliko madogo ya katiba katika ibara zinazohusika,” amesema.
Katika hitimisho la mkutano huo, Rais Samia amesema baada ya hatua hiyo, kamati ya usalama na maadili ya chama hicho itakaa kupitia majina yote na watajitahidi kuingiza vijana wengi zaidi kwa kadri inavyowezekana katika nafasi za ubunge na udiwani.
“Tutajitahidi kuingiza vijana wengi inavyowezekana, katika kutafuta nafasi za kuongoza nchi yetu katika ngazi za ubunge, lakini pia udiwani,” amesema.
Ingawa marekebisho hayo madogo ya katiba yamehusisha hata watiania wa udiwani, amesema utaratibu huo hautalihusu kundi hilo kwa kuwa tayari lenyewe mchakato wake umeshamalizika, hivyo hawatarudi nyuma.
“Kazi iliyotuweka leo (Julai 26) tumemaliza asanteni sana na Mungu akibariki chama chetu,” amesema Rais Samia huku wajumbe kutoka maeneo mbalimbali wakishangilia na kuimba: “Tuna imani na Samia, tuna imani na Samia.”
Rais Samia amesema baada ya mabadiliko hayo wanakwenda kuanza vikao vya uteuzi wa watiania vinavyofanyikia Dodoma, wakianza na kikao cha maadili Jumapili Julai 27 kisha kamati kuu Julai 28, 2025 ambacho kitafanya uteuzi wa majina hayo yatakayopigiwa ura za maoni.
Mmoja wa wabunge anayetetea nafasi hiyo kwa kipindi cha tatu aliyeomba hifadhi ya jina amesema: “Hilo la vijana kupewa kipaumbele kwa kweli linatia hofu sasa. Sijajua hata mimi kama nitarudi, lakini najiona kama bado kijanakijana hivi, ila wacha tusubiri.”
Mchambuzi wa siasa, Said Msonga amesema hatua ya CCM kufanya mkutano mkuu kwa mtandao ni mafanikio na kimeweka historia kwamba jambo hilo linawezekana.
“Wamedhihirisha kwamba wanakwenda kisasa na hili lisiwe kwa upande wa vyama vya siasa pekee, bali hata taasisi za Serikali ziige mfano ili kufikisha taarifa kwa haraka kwa watendaji wa chini wanaowahudumia Watanzania. CCM wameweka historia kubwa kwa kufanya mkutano mkuu kwa mtandao,” amesema.

Kuhusu mabadiliko yaliyofanyika Msonga amesema kwa hali ilivyokuwa awali, kamati za siasa za wilaya na mkoa zilikuwa na meno makubwa ambapo walikuwa wanapendekeza majina matatu kwenda kamati kuu baada ya kuyachakata.
“Kwa namna ilivyo ni kama vile kamati kuu ilifungwa, maana yenyewe pia ilikuwa inatakiwa kupendekeza majina matatu kwa kuzingatia pia ushauri wa kamati za siasa,” amesema.
“Ndio maana awali yalisikika malalamiko kwamba fulani amekatwa na kamati ya siasa, lakini CCM ikatoka hadharani ikasema hakuna aliyekatwa. Sasa kwa mapendekezo mapya kamati kuu itakuwa na uwanda mpana zaidi ya kuongeza majina,” amesema.
Msonga amesema kichofanywa na CCM ni mabadiliko ya msingi ili kuongeza demokrasia ndani ya chama hicho, ambayo yatawezesha kufanya mapendekezo ya ziada ya majina yatakayokwenda kwa wajumbe.
“Pamoja na mambo mengine mapendekezo hayo yatawezesha kupunguza vitendo vya rushwa vilivyoanza kulalamikiwa kwenye mchakato wa kura za maoni katika ngazi za awali,” amesema.
Kuhusu vijana kupewa kipaumbele katika mchakato huo, amesema kundi hilo ndilo kubwa kwa mujibu wa sensa, lakini pia ndio wanaokabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo ukosefu wa ajira.
“Rais Samia anaposema vijana watapewa nafasi maana yake ni fursa ya dhahabu kwa CCM na vijana wenyewe. Kuwa na kundi kubwa litakaloingia kwenye uongozi itasaidia CCM pia,” amesema.
“Lakini vijana watakaopata nafasi wasibweteke bali wajue kwamba wana dhamana kubwa ya kuwasaidia wenzao ili kuendesha gurudumu la kuchangia maendeleo ya Taifa,” amesema.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Faraja Kristomus amesema uamuzi huo unaweza kukigawa zaidi chama hicho na kutengeneza makundi kadhaa kutokana na matumizi makubwa yanayaodaiwa huwa yanafanyika kuwapata wajumbe.
“Ingawa una manufaa makubwa kwa chama endapo umakini mkubwa utatumika kuchunguza kilichofanyika kwenye kamati za siasa za wilaya. Kuna baadhi ya wagombea wameumizwa na kamati kutokana na tofauti za masilahi yao na za kisiasa.
“Kitendo cha mwenyekiti kuomba wapitishe majina ya wagombea vijana wengi kinaweza kutuma ujumbe kwa wabunge wakongwe majimboni kuwa huu ni muda wa wao kupumzika siasa na kuwapisha vijana,” amesema.
Amesema: “Kuna wabunge wamekaa majimboni miaka zaidi ya 20 watatakiwa kupumzika. Lakini pia kuna wagombea ambao wanaweza kuchinjwa kupitia utaratibu huu.”
Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM) wilayani Mbarali mkoani Mbeya, Medson Mwambapa amesema Rais Samia ameonyesha imani kubwa kwa vijana kwa hatua yake ya kutaka kundi hilo lipewe kipaumbele kwa ubunge na udiwani.
“Inaonyesha wazi mwenyekiti wetu bado anaendelea kuwaamini vijana, huu ni mwendelezo kwa sababu hakuanza jana wala juzi, bali tangu ashike madaraka amekuwa akiwapa nafasi,” amesema na kuongeza:
“Vijana ndio kundi kubwa la wapigakura, lakini pia ndio kundi linalotakiwa katika Serikali na CCM ili kuwasaidia na kuwasemea wenzao walioko nje kwa changamoto zinazowakabili, tunamshukuru Rais Samia kwa maono haya.”
Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM Taifa, kutoka wilayani Handeni, Mussa Mkombati amesema mabadiliko yaliyofanyika yatakuwa na faida kubwa kwa vijana na wagombea, hasa katika kuleta mshikamano.
Amempongeza Rais Samia kwa uamuzi huo kwani kuaminiwa kwa vijana kwenda kuchaguliwa kunafanya chama kisonge mbele kwa kuwa na jeshi kubwa.
“Kurudi majina zaidi ya matatu kutakuwa na faida zaidi kwa wanachama kwa sababu itawezesha kupunguza malalamiko na kuleta umoja,” amesema.
Mjumbe mwingine kutoka Simiyu, Lumen Mathias amesema uamuzi wa kuwapa nafasi vijana utaiimarisha CCM kwa sababu kundi hilo ndilo lina wapigakura, hivyo wakiteuliwa kuwania nafasi za ubunge na uwakilishi huenda wakafanya vizuri kutokana na kuja na mawazo mapya.
“Tunashukuru mwenyekiti kwa kutambua mchango wa vijana. Tunataka kuonyesha uwezo wetu, lakini pia tunahitaji usaidizi wa wale waliotutangulia,” amesema.
Jonathan Mnyela, mjumbe wa mkutano mkuu wa CCM Taifa wilayani Maswa amesema vijana wamepewa mwanga na kwamba, CCM ina maono makubwa ya kuangalia mbele.
“Vijana tumepewa nafasi katika kuwania nafasi hizi za ubunge na uwakilishi na tunaandaliwa kwa ajili ya uongozi wa kushika dola au kwenye chama, hivyo ni matumaini yangu majina mengi ya vijana yatarejeshwa,” amesema.
Kwa upande wake, Godlisten Kabarata amesema uamuzi huo ni mwanzo mzuri kwa vijana lakini bado wazee wana nafasi ya muhimu ya kushauri.
“Huu ni mwanzo mzuri kwa vijana, kwa muda mrefu tumekuwa tukisikia ahadi tu, sasa tunaona utekelezaji. Lakini wazee bado wana nafasi muhimu kama washauri,” amesema.
Katibu wa CCM, wilayani Kigamboni, Stanley Mkandawile amesema mabadiliko madogo yaliyofanyika katika katiba yataongeza tija na idadi ya watiania watakaorudishwa kwa wajumbe tofauti na iliyokuwa awali.
Mkandawile amesema uamuzi huo utaongeza tamaa kwa watiania ya kuamini kwamba lolote linaweza kutokea mbele ya safari katika mchakato wa kura za maoni.
Mjumbe wa mkutano huo kutoka Mbeya, Charles Mwakipesile amesema Julai 26 imekuwa siku ya kihistoria ya chama hicho kufanya mkutano kwa kidijitali.
“CCM inaweza kuwa mfano kwa Bara la Afrika kwa kupanga jambo na kulitekeleza, tumefurahia kuona uchaguzi wa kura za maoni unaenda kuwa wa huru na haki,” amesema Mwakipesile ambaye ni mtiania ya ubunge Mbeya Mjini.