Kinshasa. Katika kile kinachoonekana kuwa ukurasa mpya katika historia ya siasa za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Mahakama ya Kijeshi mjini Kinshasa siku ya Ijumaa, Julai 25, 2025 ilifungua rasmi mashitaka ya uhaini dhidi ya Rais wa zamani wa nchi hiyo, Joseph Kabila.
Hii ni historia mpya nchini Congo, kwa kionhozi aliyewahi kuiongoza nchi hiyo kwa takriban miaka 18 kufutiwa kinga za kikatiba na kunguliwa mashitaka ambayo kwa mujibu wa sheria za nchi hiyo adhabu yake ni kifo.
Kabila anashtakiwa kwa makosa tisa yakiwemo uhaini, mauaji ya makusudi na mateso, huku pia akikabiliwa na tuhuma nzito za kushirikiana na kundi la waasi la M23, Muungano wenye historia ndefu ya uasi na vita mashariki mwa Kongo.
Kesi hiyo imefunguliwa katika mahakama ya Kijeshi jijini Kinshasa licha ya Kabila kutokuwepo mahakamani, hali inayoashiria mvutano unaoendelea kati ya Serikali ya sasa na mtandao wa kisiasa wa utawala uliopita.
Taarifa kutoka nchini humo zinaeleza kuwa, Kabila anadaiwa kuhusishwa na kundi la M23, ambalo tangu Januari mwaka huu limetekeleza operesheni za kijeshi zilizosababisha kutekwa kwa mji wa Goma na maeneo mengine muhimu mashariki mwa nchi hiyo.
Inadaiwa kuwa, Rais huyo wa zamani wa nchi hiyo, alitembelea mji huo Mei mwaka huu, hatua iliyozua maswali mengi, hasa ukizingatia kuwa ni ngome ya waasi kwa sasa.
Rais wa sasa Félix Tshisekedi anadaiwa kumtuhumu mtangulizi wake huyo, kuwa analifadhili kundi hilo.
Tuhuma hizo zimezua wasiwasi mkubwa wa kiusalama, katikati ya juhudi za kikanda na kidunia za kurejesha amani nchini humo.
Hatua ya mahakama imekuja siku chache tu baada ya Seneti ya DRC kumvua Kabila hadhi ya kuwa seneta wa maisha, nafasi aliyopewa kwa mujibu wa Katiba kama Rais mstaafu.
Wapinzani wake wanasema hilo ni pigo la moja kwa moja dhidi ya kinga zake za kisiasa na kisheria, linalomuweka wazi kushitakiwa bila kinga ya kisheria kama Mkuu mstaafu wa nchi.
Kwa upande wake, Kabila amekanusha mashitaka yote na kuitaja hatua hiyo kama mgogoro wa kisiasa unaotumiwa na Serikali ya sasa kuminya demokrasia na kuendeleza uhasama wa kisiasa nchini DRC.
Wakati jeshi likimfungulia kesi nzito aliyekuwa Rais wa nchi hiyo, hali ya kiusalama mashariki mwa nchi hiyo inaendelea kuwa ya hatari.
Katika wilaya ya Masisi, karibu na mji wa Goma, watu 11 wameripotiwa kuuawa katika mashambulizi ya kuzi.
Mashambulizi hayo mapya yaliripotiwa kuua watu 11 katika mji wa Luke, huku wengine 21 wakijeruhiwa vibaya.
Taarifa zinasema vituo vya afya na miundombinu mingine ya jamii vimeharibiwa kabisa na mapigano hayo.
Mkuu wa tarafa ya Banyungu, Alexandre Kipanda Mungo, amenukuliwa na vyanzo vya habari vya kimataifa nchini humo vikiwemo BBC na DW akitupia lawama kundi la M23 kwa mashambulizi hayo.
“M23 hawajaacha vita,” amenukuliwa kiongozi huyo huku akieleza kuwa waasi hao wamevamia pia maeneo ya Nyamabako na vijiji vya karibu.
Katika hali inayozua mshangao zaidi, hatua hii imefikiwa licha ya kutiwa saini kwa mkataba wa amani kati ya Serikali ya Congo na kundi la M23 wiki iliyopita mjini Doha, Qatar.
Wiki iliyopita, Serikali ya Congo ilifikia mwafaka na Waasi wa M23 kutua silaha chini kufuatia kutiwa saini azimio la kanuni lililopewa jina la Declaration of Principles na baadaye Mkutano wa Mawaziri kutoka nchi za SADC ulioketi jijini Dar es Salaam, Tanzania, kutoa wito wa kumalizwa kwa migogoro ya kisiasa nchini Congo.
Hata hivyo, msemaji wa M23, Lawrence Kanyuka, anadaiwa kukanusha madai hayo akisema kuwa ni wanajeshi wa Serikali waliovunja mkataba huo kwa kushambulia maeneo yao, akiwataja kama “watu wasiopenda amani” wakati huu mazungumzo yakiendelea.
Kwa zaidi ya miaka 30, mashariki mwa DRC imekuwa ikikumbwa na mzozo wa muda mrefu unaochochewa na makundi ya waasi, mvutano wa kikabila na maslahi ya kiuchumi.
Tangu mwaka 2021, kundi la M23 limeongeza kasi ya mashambulizi na kudhibiti maeneo yenye utajiri wa madini, hali inayozidi kuongeza ukinzani baina ya majeshi ya serikali na waasi hao.
Katika hali ya sasa nchini humo, kesi ya Kabila si tu inaweka rekodi katika historia ya nchi hiyo, bali pia inafungua ukurasa mpya juu ya mustakabali wa kufikiwa kwa amani ya kudumu nchini humo.