Mwanza. Wasomi kutoka vyuo vikuu, watafiti na wahadhiri wa kada mbalimbali nchini wamependekeza mageuzi ya kisera, maboresho ya elimu na kuimarishwa kwa tafiti kama nguzo kuu za kufanikisha Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050 kupitia ubia kati ya sekta ya umma na binafsi (PPP).
Mapendekezo hayo yametolewa katika kongamano lililoandaliwa na Kituo cha Ubia kati ya Sekta ya Umma na Binafsi (PPPC) kwa kushirikiana na Mpango wa Utafiti na Elimu ya Demokrasia Tanzania (Redet) lililofanyika leo Jumamosi Mei 26, 2025, Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustino (Saut) jijini Mwanza.
Katika mjadala huo, wasomi hao wamesisitiza umuhimu wa kujenga uchumi jumuishi unaotegemea utaalamu wa ndani, utafiti wa kina na mazingira ya biashara yanayovutia wawekezaji, hasa wazawa.
Elimu ya vitendo, sera na tafiti
Akizungumza katika kongamano hilo, Dk David Kafulila, Mkurugenzi Mtendaji wa PPPC, amesema sera na sheria ya ubia ina ushindani katika utekelezaji wa miradi hivyo wanazuoni wanapaswa kushirikiana kufanya tafiti ili kubaini changamoto hizo.
“Wanazuoni mnao wajibu wa kujua, kuelewa na zaidi kufanya tafiti ila hatuna chuo kinatoa digrii ya masuala ya ubia kwa sababu uwezo wa Serikali nyingi kumudu gharama ni mdogo na ndio maana deni la Serikali duniani kote linazidi kupaa ukilinganisha na uchumi kwa hiyo ni muda wa kuwakilisha wanazuoni kuendesha Dira ya Taifa,” amesema Kafulila.

Mkurugenzi Mtendaji wa PPPC, David Kafulila akizungumza katika kongamano la sekta binafsi lililokuwa na mada kuu nafasi ya ubia katika kufikia malengo ya dira ya maendeleo 2050. Picha na Timothy Lugoye
Aliyewahi kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Profesa Adelardus Kilangi amesema kuwa bado kuna pengo kubwa la uelewa na mawasiliano kati ya sekta binafsi na ya umma katika utekelezaji wa miradi ya ubia.
“Lugha inayozungumzwa na sekta hizi mbili bado haijaungana. Tunahitaji tafiti za kina kuhusu historia ya PPP, uhusiano wa siasa na sheria na namna sera zetu zinavyounga mkono au kudhoofisha ushirikiano huu,” amesema Profesa Kilangi.
Uboreshaji wa mitaala na uwekezaji kwa watu
Mhadhiri Mwandamizi katika Usimamizi wa Utalii katika Chuo Kikuu cha Saut, Dk Delphine Kessy amesisitiza haja ya kuwa na chombo huru cha kitaifa kitakachosimamia miradi ya ubia, kufanya tathmini ya maendeleo na kujifunza kutoka kwenye makosa ya nyuma.
“Chombo hicho kingeweza kutoa taarifa kila baada ya miaka mitano kipi kimefanikiwa, wapi tumejikwaa, na nini tuboreshe. Hii itasaidia PPPC kufanya kazi kwa ufanisi zaidi,” ameeleza.
Ameongeza kuwa” Kama sisi tukiweza kuwekeza vizuri na hatuna sehemu ya kuwekeza nzuri, na yakuuza vizuri itakuwa namna gani? Tunahitaji mtaji nje na hata watu wa nje wanatuhitaji.”
Katika mchango wake, Khadija Khamis, mwanafunzi wa kidato cha sita aliyehudhuria kongamano hilo, ametoa wito kwa Serikali kuboresha ufundishaji wa masomo ya uchumi na biashara katika shule za sekondari ili kuwajengea wanafunzi msingi imara wa kushiriki kwenye uchumi wa nchi.
“Tunahitaji elimu ya vitendo inayotufundisha namna ya kushiriki kwenye uchumi wa Taifa, siyo ya kujibia mitihani tu. Pia tunaomba walimu wa kutosha kwenye shule zetu,” amesema Khadija.
Sekta binafsi ya wazawa kupewa kipaumbele
Naye, Dk Ntui Ponsian, Mkuu wa Idara ya Uhasibu na Fedha Saut Mwanza, amesema kuwa sekta binafsi ya ndani ndiyo injini ya kweli ya maendeleo.
Amesema sera zilizopo hazijatosheleza kuilinda na kuikuza sekta hiyo kabla ya kuingia kwenye ubia na Serikali.
“Nimeona rasimu ya sera ya sekta binafsi ya mwaka 2013, lakini hatujaweka mkazo wa kutosha kwa sekta binafsi ya wazawa. Ikipewa msukumo na motisha, uchumi wa Taifa utakuwa imara zaidi na endelevu,” amesema Dk Ntui.
Ameongeza kuwa ili kufikia uchumi wa dola trilioni moja ifikapo 2050, taifa linahitaji kuwa na uchumi unaoweza kugharamia sekta zote, uwekezaji mkubwa katika rasilimali watu na elimu bora na mazingira ya biashara yenye utulivu wa kisera na kisheria.
“Hatutaki muwekezaji aweke fedha leo, halafu kesho mtu anaamka na kufunga biashara kwa amri ya ghafla. Tunahitaji sera zinazotabirika na mazingira yanayovutia wawekezaji wa ndani na nje,” amesema.