Dar es Salaam. Wakati taifa linapoelekea katika kipindi cha uchaguzi, waumini wa Kanisa la Evangelistic Assemblies of God Tanzania (EAGT) Temeke kwa kushirikiana na viongozi wengine wa kiroho wameandaa mkutano wa injili ukiwa na lengo la kuwaombea Watanzania amani, mshikamano, na uongozi wenye maadili kuelekea uchaguzi ujao.
Maombi hayo yanatarajiwa kuanza kesho Julai 27, 2025 katika viwanja vya Mwembe Yanga, Wilaya ya Temeke jijini Dar es Salaam.
EAGT wakieleza kuhusu maombi hayo Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) leo Julai 26, 2025 kupitia mwenyekiti wake Jaji wa Rufaa, Jacob Mwambegele amesema ratiba ya uchaguzi wa Rais, wabunge na madiwani itatakuwa Oktoba 29, 2025.
Akizungumza na vyombo vya habari leo Julai 27, 2025 Mchungaji Kiongozi wa EAGT Temeke, Christomoo Ngowi amesema unalenga kusambaza upendo, matumaini na kuondoa hofu ambayo baadhi ya wananchi wanayo kuelekea uchaguzi.
“Bwana Yesu alituagiza tufanye mataifa kuwa wanafunzi. Hili ni jukumu letu kama watumishi wa Mungu. Na katika kipindi hiki tunapoelekea uchaguzi, tunaliona hili kama fursa ya kipekee ya kuwaombea Watanzania wote,” alisema Mchungaji Kingowi.
Amesema katika wakati huu ambapo nchi inaelekea katika uchaguzi, watu wanahitaji neno la faraja ndiyo sababu ya mkutano huo ambao umebeba maombi ya kitaifa kwa ajili ya uchaguzi ulio wa amani na kuepuka chokochoko au uchochezi wa kisiasa kwani maombi ni silaha kuu.
Kwa mujibu wa Mchungaji Kingowi, mkutano huo pia utakuwa jukwaa la watu kuungana kwa maombi dhidi ya roho za chuki, uchochezi, na hofu ambazo zinaweza kuathiri kampeni na uchaguzi kwa ujumla.
“Kama kuna roho chafu za kishetani, tunamuomba Mungu atushindie tuwe na uchaguzi wa amani,” amesema Mchungaji Kingowi huku akisisitiza kuwa mkutano huo utakuwa ni sehemu ya mabadiliko ya kiroho kwa taifa.
Wito huo umeungwa mkono na Mchungaji wa kanisa hilo kutoka Mwanza, Diana Dionizi akisema mkutano huo hautakuwa wa kawaida bali ni wa kipekee kwa sababu unaambatana na maombi mahsusi kwa ajili ya uchaguzi.
“Asikose mtu na asiwe mchoyo, akamwalika na jirani yake. Watu wenye mahitaji mbalimbali afya, ajira, ndoa, na hata maamuzi ya maisha Mungu yupo tayari kuwatendea kupitia mkutano huu,”
Mzee kiongozi wa kanisa hilo, Joseph Mwinura amesema wamekamilisha maandalizi yote muhimu na sasa wanakaribisha wananchi kutoka maeneo mbalimbali kushiriki katika mkutano huo wa kiroho utakaoanza Jumapili hadi Agosti 3, mwaka huu.