Hekta 11,000 za mikoko zatoweka Pemba

Pemba. Wananchi ambao wanaishi maeneo ya pembezoni mwa Pwani ya Bahari ya Hindi katika Kisiwa cha Pemba, wametakiwa kuhakikisha wanatunza na kuhifadhi misitu ya mikoko ambapo kwa sasa kuna ongezeko la kukatwa na kuharibiwa kwa mazingira yake, jambo ambalo ni hatari kwao.

Akizungumza kwenye maadhimisho ya siku ya Mikoko Duniani iliyofanyika katika Shehia ya Shidi wilaya ya Mkoani Mkoa wa Kusini Pemba leo Jumamosi Julai 26, 2025 Afisa Mdhamini wa Wizara ya Kilimo, Umwagiliaji, Maliasiri na Mifugo Pemba, Mhandishi Idriss Hassan Abdullah amesema zaidi ya hekta 11,200 za misitu ya mikoko zimeharibiwa.

Amesema kwa eneo lote la Zanzibar ambalo lilikuwa na uhifadhi wa misitu ya mikoko ilikuwa ni zaidi ya asilimia nane, ila kwasasa hifadhi zinazidi kupungua hali ambayo inasababisha bahari kusogea kwenye makazi ya wananchi jambo ambalo lina madhara.

Mhandisi Idriss ameongeza kuwa wananchi ambao wanaishi pembeni ya hifadhi za misitu ya mikoko wanatakiwa kubadilika kwa kuilinda,kuacha kuvuna bila utaratibu lakini pia kujenga utamaduni wa kupambana kuilinda wakati wote ili hifadhi ziendelee kubakia.

“Kuna madhara makubwa ya kuendelea kuharibu hifadhi za misitu ya Mikoko kwenye jamiii mpaka sasa yapo mashamba ya mpunga yameshamezwa na maji ya bahari na hakuna shughuli inaendelea, hivyo kama hatutashirikiana katika kuhifadhi misitu hii ni hatari kwa maisha yetu sote kwani hali ni mbaya,” amesema Mhifadhi Idriss.

Amewataka masheha na viongozi wengine kuhakikisha wanakuwa walinzi kwenye maeneo yao kwa kulinda mikoko na mazao mengine ya bahari, ambayo yamekuwa yakisaidia katika uhifadhi wa mazingira lakini pia viumbe hai.

Ofisa Mkuu Idara ya Misitu Pemba, Samira Makame Juma amesema jumla ya miche 2,500 imepandwa katika Shehia ya Shadi katika maadhimisho hayo, na zoezi hilo litaendelea mara kwa mara ili kuhamasisha wananchi katika utunzaji wa mazingira ya bahari.

Amesema kwa Pemba kuna zaidi ya hekta 11,400 za hifadhi za miti aina mbalimbali ya baharini ikiwemo mikoko na wanaendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa kutunza pwani za bahari, kwani bila kufanya hivyo maji yataendelea kusogea kwa wananchi.

Ameitaka jamii kutoa taarifa kwenye kamati zinazosimamia uhifadhi wa mikoko endapo wataona yupo miongoni mwao anajihusisha na uvunaji wa mikoko, kwani kwa upande wa mkoani kwa mwaka mmoja hadi sasa wameshapanda miche 350,000 kwenye Shehia mbalimbali.

Afisa suluhisho za kiasili kutoka Shirika la Kimataifa linalojihusisha na Uhifadhi (IUCN) Suleiman Masoud Mohamed amesema ukataji mikoko una madhara kwenye jamii, kwani unasababisha ongezeko la joto, maji ya bahari kusogea nchi kavu na ongezeko la chumvi nchi kavu.

Hivyo kushauri wananchi badala ya kuvuna mikoko, wanaweza kuitumia katika ufugaji wa nyuki, kaa bahari na mazao mengine ambayo yatakuwa na faida kubwa kwao endapo watazalisha kwa wingi.

Afisa jinsia Mradi wa ReSea kutokea Mfuko wa Ruzuku kwa Wanawake Tanzania Grace Thomas ameshauri viongozi kuwashirikisha vijana na wanawake katika utunzaji wa mazingira ya bahari, kwani zipo faida mbalimbali watazipata kwa elimu hiyo.

Amesema wanawake ndio kundi kubwa ambalo linatumia nishati ya mkaa na kuni hivyo endapo watapewa elimu, itaweza kusaidia kupunguza uharibifu wa hifadhi za misitu bahari.

Dunia huadhimisha siku ya Mikoko kila mwaka Julai 26, mimea ambayo inapatikana zaidi katika fukwe za bahari na faida kubwa ni makazi ya samaki, kaa na viumbe wengine wa bahari ukiacha kulinda mazingira ya baharini.