SIMBA haipoi. Baada ya kudaiwa kunasa saini ya mmoja wa mabeki wa Mamelodi Sundowns, mara hii imerejea tena ikipambana kuchomoa mtu ndani ya timu hiyo ambaye katika mashindano ya Kombe la Dunia la Klabu kule Marekani ulimshuhudia akikipiga katika kikosi hicho.
Achana na Rushine De Reuck, beki unayeweza kumuona mitaa ya Msimbazi msimu ujao, lakini mara hii kocha wa timu hiyo, Fadlu Davids amepania kwelikweli kukisuka kikosi hicho ikielezwa kwamba jeuri ya bilionea wa Simba, Mohammed Dewji ‘Mo’ imetia mzuka kuhakikisha kwamba vyuma vya maana vinashushwa.
Hivi sasa Simba ipo katika mazungumzo na winga wa kushoto, Thapelo Maseko mwenye umri wa miaka 21 kutoka klabu ya Mamelodi Sundowns inayoshiriki Ligi Kuu ya Afrika Kusini.
Chanzo kutoka Simba kilisema zoezi hilo linasimamiwa vyema na kocha wa timu hiyo, Fadlu Davids ambaye ni mwenyeji wa Afrika Kusini anayetaka wachezaji wenye viwango vya juu watakaoisaidia kufanya vizuri michuano ya ndani na kimataifa ambayo msimu uliopita ilicheza fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya RS Berkane na kupoteza.
“Kocha ndiye aliyependekeza jina la Maseko na kama Simba ikimsainisha atakuwa mchezaji wa pili kutoka Mamelodi Sundowns baada ya kumalizana na beki Rushine De Reuck,” kilisema chanzo hicho na kuongeza.
“Kocha anahitaji zoezi la usajili likamilike mapema, ili wanapokwenda kufanya maandalizi ya msimu mpya awe na kikosi kamili.”
Maseko msimu uliopita katika Ligi Kuu ya Afrika Kusini, hakuwa mchezaji wa kikosi cha kwanza ambapo alicheza mechi nane, akafunga bao moja, huku upande wa Ligi ya Mabingwa Afrika akicheza mechi tatu. Upande wa MTN8 alicheza mechi moja sawa na Carling Knockout na Nedbank Cup.
“Ni mchezaji mzuri na mwenye kasi na nguvu, kikubwa ni dili lake kufanikiwa ili aje kuongeza nguvu katika harakati za kuwania ubingwa kwa msimu ujao,” kilibainisha chanzo hicho na kuongeza.
“Simba inafanya usajili wake kimyakimya, lengo la uongozi ni kuona inapata wachezaji ambao watarejesha furaha kwa kutwaa mataji ikiwemo Ligi Kuu Bara ambalo klabu haijachukua ndani ya misimu minne mfululizo.”
Kama Simba itafanikiwa kuinasa saini ya Maseko mwenye uwezo pia wa kucheza winga ya kulia, maana yake ni kwamba ataongeza wigo katika eneo la ushambuliaji ambapo taarifa zinabainisha klabu hiyo ipo hatua za mwisho kuwauza washambuliaji wake wawili, Leonel Ateba na Steven Mukwala, huku Kibu Denis naye akiwa kwenye hatua nzuri kusajiliwa na Nashville SC ya Marekani alipokwenda kufanya majaribio.
Hivi karibuni, Simba ilitajwa kuinasa saini ya beki wa kati, Rushine De Reuck ambaye alikuwa akicheza Mamelodi tangu Januari 2021, kabla ya Januari 2025 kutimkia Maccabi Petah Tikva ya Israel kwa mkopo uliomalizika mwisho wa msimu uliopita.
Pia inaelezwa kuwa kwenye mazungumzo ya kumsajili kiungo mshambuliaji, Neo Maema (29) kwa mkopo kutoka Mamelodi.
Nyota huyo mwenye uwezo pia wa kucheza winga ya kushoto na kulia, tangu amejiunga na Mamelodi kutoka Bloemfontein Celtic mwaka 2021, amecheza takribani mechi 120, akifunga mabao 13 na asisti 14, huku muda wote huo akishinda mataji manne ya ligi ndani ya timu hiyo.
Maseko na Maema, walikuwa sehemu ya kikosi cha wachezaji wa Mamelodi kilichoshiriki Kombe la Dunia la Klabu 2025 nchini Marekani ambapo timu hiyo safari yao iliishia hatua ya makundi ikishika nafasi ya tatu Kundi F ikikusanya pointi nne kufuatia kushinda mechi moja, sare moja na kupoteza moja.