Dar es Salaam. Hakuna adui na tatizo kwenye ndoa kama vile kutojiamini, kuamini wengine kama vile vigagula na wachunaji waitwao waombaji na ushirikina.
Baadhi ya wanandoa wamevunja ndoa hasa kina mama kutokana na ujinga na uzwazwa huu. Hii ni kutokana na mfumo dume ambao humhukumu mwanamke linapokuja suala la kuwajibika katika ndoa.
Leo kutokana na uzoefu, tutadurusu kadhia hii na kwa kuangazia vyanzo vya tatizo. Zifuatazo ni sababu za ndoa nyingi kuvunjika linapokuja suala la imani iwe ni ya mhusika, vitu, au watu wengine.
Mosi, dhana ya imani inajulikana. Haihitaji tafsiri. Imani katika maisha yawe ya binafsi, jamii, au taasisi ni jambo la muhimu. Inaweza kuleta faida au hasara kulingana na inavyoeleweka na inavyotumika.
Mfano, kupitia imani, watu hujenga utamaduni usiobadilika kirahisi. Wakati mwingine, imani haina tofauti na kasumba au uraibu.
Pili, wengi hushindwa kutatua matatizo kutokana na kutojiamini iwe ni kwa wote au mmoja wao. Unaposhindwa kujiamini, utawaamini wengine au vitu vingine kama vile waganga na tunguli zao, wachungaji au wanaojitia kukuombea na upuuzi kama upako au vitambaa,wakikuhadaa kuwa wanaweza kutenda miujiza na kumaliza tatizo lako hata bila kujua mzizi kuwa ni wewe mwenyewe.
Tushadurusu mambo mengi yanavyovunja ndoa kama vile kutotunza siri, malezi mabaya, tamaa, na mengine mengi. Hivyo, wanandoa wanapaswa kujiamini na si kuamini wengine.
Hata hao wanaowaamini na kuwapelekea matatizo yao ya ndoa wanayo matatizo yao tena makubwa kuliko yao. Isitoshe, wengi hutumia fursa hii kuwanyonya, kuwadhalilisha, hata kuwaibia waathirika.
Usishangae kwanini waathirika hawajiamini ila wanawaamini wengine tena wasioaminika ambao nao hawaamini hawa waaminio. Wote wawili wanajua uovyo na kutoaminika kwao.
Huwezi kumsaliti mwenzako kutokana na kutojiamini na ushirikina ukaaminika wakati hajiamini wala kuaminika? Je, anayemhadaa na kumtumia huyu mwathirika naye anaaminika? Kimsingi, wawili hawa wanahitaji msaada.
Tatu, kutojua tatizo linapotokea ni tatizo kubwa kwa wanandoa wengi ambao ndoa zao zinayumba hata kuvunjika. Je, hili linaingilianaje na imani?
Linapotokea tatizo, wengi, badala ya kulitafuta tatizo na kulijua ili walishughulikie kisayansi, hutafuta sababu na visingizio kama vile kurogwa, laana, na upuuzi mwingine ambavyo ni matokeo ya kile wanachoamini. Badala ya kutafuta suluhu, wengi huamini kuna mkono wa mtu hata kama ni mkono wao wenyewe.
Kimsingi, unaposhindwa kujua tatizo na kuamini kuwa limetengenezwa, huwezi kulitatua kwa sababu hutajua hata namna ya kufanya hivyo. Badala ya kutumia muda kulidurusu na kulitafutia suluhu mujarabu, utapoteza fursa ya kulitatua.
Hapa, ndipo imani inapoingia. Badala ya kuelewa tatizo, mhusika anaanza kuamini vitu hata visivyoingia akilini kiasi cha kuzidisha ukubwa na hata ugumu wa tatizo.
Je, wanandoa wafanyaje katika hali hii? Tunashauri wafanye kama madaktari wafanyavyo wanapoletewa wagonjwa. Madaktari hawawezi kumtibu mgonjwa bila kujua aina ya ugonjwa ili waweze kutoa aina ya dawa na dozi vinavyotakiwa.
Hivyo, ni muhimu kulijua tatizo, sababu zake, na ukubwa wake ili kuweza kulishughulikia kisayansi.
Tatu, unaweza kulijua tatizo lakini ukagoma au kushindwa kutumia njia mujarabu kwa vile unaamini katika kutengenezwa kwa tatizo na siyo wewe au nyinyi. Mnatengeneza au kujenga au kusababisha mazingira ya kulitengeneza siyo kulitatua.
Hapa, tatizo siyo kutojua tatizo bali kukubali kuwa lipo, na hivyo, kulitafututia jawabu. Tunashauri wanandoa watafute chanzo cha tatizo ili kupata namna ya kulitatua kisayansi na siyo kiimani.
Nne, wapo wanaovunja ndoa kutokana na kutafuta majibu ya haraka na mepesi ama kwa sababu ya ujinga au ukosefu wa subira au hofu ya kukosa au kushindwa.
Linapotokea tatizo, wanandoa wajipe muda si kulisoma tatizo tu bali hata kutafakari na kufanya utafiti kabla ya kutoka nje kutafuta misaada ambayo inaweza kuwa chanzo cha kuvunjika ndoa.
Mwisho, ni vizuri wanandoa wakajiamini na kuaminiana na kutafuta chanzo cha tatizo au matatizo badala ya kuamini katika njia rahisi na za mkato ambazo mwishowe huleta maangamizi ya ndoa kutokana na imani potofu na za kishirikina kuwa wengine wanaweza kutatua matatizo yao. Mliooana ni nyinyi na siyo hao mnaowaamini tena wasioaminika. Jiamini na aminianeni mdumishe ndoa yenu.