BAADA ya msimu wa 2024/25 kukamilika patupu kwa Simba bila kutwaa taji lolote kubwa ndani na nje ya nchi, macho yote yakageuka kwa benchi la ufundi la timu hiyo chini ya Kocha Fadlu Davids kuona hatua gani inafuata katika mradi wake.
Kocha huyo kijana raia wa Afrika Kusini hakulaza damu. Alichora ramani ya namna ambavyo heshima ya klabu hiyo inaweza kurudi baada ya kutengeneza msingi katika msimu wake wa kwanza.
Pamoja na mambo mengine, Fadlu alitoa tathmini ya kiufundi ambayo ilionyesha kasoro katika maeneo kadhaa huku moja kati ya hayo likiwa ni lile la safu ya ushambuliaji, hasa nafasi ya mshambuliaji wa kati.
Ilibainika kuwa pamoja na Simba kuwa miongoni mwa timu zilizotengeneza nafasi nyingi zaidi katika Ligi Kuu Bara (asilimia 60 ya mashambulizi yakitokea katikati), lakini nafasi hizo hazikufanyiwa kazi kwa kiwango cha kuridhisha.
Huku akiwa na rungu la kufanya usajili wa wachezaji wote wa kigeni, Fadlu alitazama Kaskazini, Magharibi na Kusini mwa Afrika, lakini aliamua kutupa ndoano kwa Jonathan Sowah ambaye alikuwa nyumbani kwao Ghana kwa mapumziko. Na ndani siku chache dili hilo likajipa.
Sowah ambaye anatajwa kujiunga na Simba akitokea Singida Black Stars ni mshambuliaji wa kimataifa kutoka Ghana ambaye aliwahi pia kung’ara akiwa na Medeama ya nchini humo. Alijiunga na Singida Black Stars kwenye dirisha dogo la usajili Januari 2025 na kuanza kuonyesha ubora ndani ya dakika chache.
Katika mechi 11 alizocheza kwenye Ligi Kuu Bara msimu wa 2024/25, Sowah alifunga mabao 13 ikiwa ni wastani wa bao 1.18 kwa kila mechi – takwimu ambazo si rahisi kupatikana.
Katika soka kuna tofauti kati ya mchezaji anayejua kufunga na mfungaji wa asili. Sowah ni wa kundi la pili – yule ambaye hata ukimpa nafasi moja ataigeuza bao. Ana uwezo wa kufunga kwa mguu wa kushoto, kulia, kichwa na hata akitokea nje ya boksi.
Aina yake ya uchezaji ni ile ya mshambuliaji ambaye hasubiri huduma maalumu – anaweza kutengeneza nafasi kupitia presha kwa mabeki. Anajua kutumia mwili wake kuzuia mpira na ana uwezo wa kufunga hata akiwa chini ya ulinzi mkali wa mabeki.
Pia Sowah ni mchezaji anayependa kukimbia nyuma ya mabeki akitumia kasi yake kuvunja mitego ya kuotea na kuibuka kwenye nafasi nzuri ya kufunga.

Mojawapo ya changamoto kubwa ambazo Fadlu atalazimika kuzifanyia kazi kwa haraka ni nidhamu ya kiuchezaji ya mshambuliaji huyo. Ingawa mchezaji huyo ana rekodi nzuri ya kufumania nyavu bado kuna upungufu kwenye utulivu uwanjani, hasa pale anapowekewa presha na mabeki wa timu pinzani. Hilo linaweza kuwa tatizo kwa timu katika mechi muhimu na zenye ushindani mkubwa.
Katika fainali ya Kombe la FA msimu uliopita, Sowah alijikuta akitumbukia kwenye mtego wa kupaniki baada ya mabeki wa Yanga kumkaba kwa karibu. Badala ya kuonyesha ukomavu alionekana kukasirika kupita kiasi, hali iliyosababisha kuingia kwenye mabishano yasiyo ya lazima.
Matokeo yake alionyeshwa kadi ya pili ya njano kisha akatolewa nje kwa kadi nyekundu jambo ambalo lililodhoofisha timu yake wakati huo. Fadlu atalazimika kutumia muda mwingi kumjenga mshambuliaji huyo ili aweze kucheza kwa nidhamu na kuwa mtulivu hata pale mambo yanapokwenda ndivyo sivyo.
Simba ya Fadlu mara nyingi hutumia mfumo wa 4-2-3-1 ambapo mshambuliaji wa kati ndiye mlengwa wa mashambulizi mengi. Katika mfumo huo Sowah atakuwa na nafasi kubwa ya kung’ara kwa sababu ya aina ya wachezaji waliopo nyuma yake akiwamo Charles Ahoua, Joshua Mutale, Elie Mpanzu, na hata Kibu Denis.
Pia, ujio wa Sowah unaweza kuruhusu Simba kucheza mifumo mingine mipya kama 4-4-2 Diamond ambapo Sowah atashirikiana na mshambuliaji mwingine, huku viungo wakitoa pasi za uhakika kutoka nyuma. Mwingine ni 3-5-2 ambapo atapata msaada wa mabeki wanaopanda kama Shomary Kapombe.
Kwa vyovyote vile, Sowah ni mchezaji ambaye haishii kwenye mfumo mmoja anaweza kucheza katika staili yoyote ya kisasa.
Msimu uliopita, Ahoua alikuwa kila kitu kwa Simba. Mbali na kuwa kiungo mshambuliaji, alilazimika pia kuchukua jukumu la kufunga. Kuwa na Sowah kutampa nafasi Ahoua kupumua na kujiweka zaidi katika nafasi ya mtengenezaji wa mabao.
Pia itamsaidia Ahoua kupunguza ‘uwezekano wa hata kuumia’ kwa sababu hatalazimika kufunga kila mechi au kuingia kwenye boksi kila wakati kazi hiyo sasa ni ya Sowah. Kwa mantiki hiyo, Sowah si tu mshambuliaji, bali ni sehemu ya suluhisho la matatizo ya kiufundi yaliyokuwa yakiiandama Simba kwa muda.
Habari kutoka ndani ya Msimbazi zinasema kuwa Simba ipo tayari kuwaaga washambuliaji wake wawili Mukwala na Ateba.
Uamuzi wa kuwaachia ni wa kimkakati Simba haitaki kuwa na wachezaji wengi wa nafasi moja ambao hawapati muda wa kutosha uwanjani. Pia ni nafasi ya timu kuingiza mapato na kuwekeza katika maeneo mengine.
Usajili wa Sowah ni sehemu ya mpango mpana wa kuhakikisha Simba inarudi kuwa timu tishio kuanzia katika ligi ya ndani na kuendelea kufanya vizuri katika michuano ya CAF. Timu inayotaka mataji ni lazima iwe na mfungaji anayefunga mabao hata wakati timu haichezi vizuri.
Simba haitaki kuwa timu inayomiliki mpira bila matokeo. Wanataka mabao, wanataka ushindi, na wanataka ubingwa Sowah ni sehemu ya silaha mpya kuelekea huko.
Akimzungumzia mchezaji huyo, nyota wa zamani wa Yanga, Said Maulidi ‘SMG’ anasema namba zinambeba Sowah kwani ameonyesha uwezo mkubwa ndani ya muda mfupi huku akitaja nidhamu kuwa ndio shida inayomuangusha akimfananisha na Mario Balotelli – nyota wa zamani wa Liverpool, Inter Milan, AC Milan na Manchester City.
“Ubora aliouonyesha unaweza ukawa ni uwezo wake binafsi au amebeba na timu anayoichezea. Nafikiri ni mtu sahihi, lakini watafute mtu wa kukaa naye ili kumjenga apunguze hasira au nidhamu mbovu inayosababisha kuiangusha timu kutokana na adhabu zake za mara kwa mara za kadi nyekundu,” anasema.
Mchezaji wa zamani wa Simba na Yanga ambaye sasa ni meneja wa Singida Black Stars, Amissi Tambwe ambaye aliwahi kuwa mfungaji bora wa Ligi Kuu Bara kwa vipindi tofauti akiwa na Simba, anasema Sowah ana akili kubwa ya mpira na kila kocha anatamani kuwa na mchezaji wa aina hiyo.
“Amefunga mabao 13 ndani ya mechi chache, unajiuliza angeanza msimu angekuwa na mabao mangapi. Anajua kucheza na akili za mabeki, lakini pia analijua goli,” anasema.
Mwandishi wa Makala hii ni mshindi wa Tuzo ya Umahiri wa Uandishi wa Habari Tanzania (EJAT) 2023 katika kipengele cha Uandishi wa Takwimu kwa Vyombo vya Habari vya Chapisho (Print Media).