Ofisi za TPA kuanzishwa jijini Kigali

Dar es Salaam. Serikali imesaini makubaliano ya uanzishwaji wa Ofisi ya Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari ya Tanzania (TPA) jijini Kigali, nchini Rwanda, kama sehemu ya hatua za kuimarisha uhusiano wa karibu na kukuza maendeleo ya pamoja baina ya Tanzania na Rwanda.

Kuanzishwa kwa ofisi ya TPA jijini Kigali kunalenga kurahisisha upatikanaji wa huduma za bandari nchini Rwanda, kupunguza gharama za bidhaa, kuimarisha na kuongeza matumizi ya bandari za Tanzania kama lango kuu la kupitisha mizigo na shehena za Rwanda.

Mbali na kuanzishwa kwa ofisi hiyo, pia kumesainiwa makubaliano ya ushirikiano kwenye sekta ya kilimo kati ya nchi hizo za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).

Hayo yote yamejiri baada ya Mkutano wa 16 wa Tume ya Kudumu ya Pamoja ya Ushirikiano (JPC) kati ya Tanzania na Rwanda kufungwa rasmi jijini Kigali, Julai 26, 2025, ambapo mawaziri wa pande zote mbili wamesaini hati hizo mbili za makubaliano ya ushirikiano.

Hati hizo zimesainiwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wa Tanzania, Balozi Mahmoud Kombo, na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Rwanda, Balozi Olivier Nduhungirehe.

Kwa mujibu wa Wizara ya Mambo ya Nje, lengo la makubaliano hayo ni kuimarisha ushirikiano wa kimkakati kati ya Tanzania na Rwanda kwa manufaa ya wananchi wa mataifa hayo.

Ikifafanuliwa zaidi kupitia makubaliano ya sekta ya kilimo, pande zote zimekusudia kubadilishana uzoefu, teknolojia, utaalamu na taarifa muhimu ili kuongeza uzalishaji, usalama wa chakula, na fursa za biashara ya mazao ya kilimo.

Akizungumza wakati wa hafla ya kufunga mkutano, Waziri Kombo amesisitiza umuhimu wa utekelezaji wa makubaliano yote yaliyoafikiwa katika mkutano huo.

“Niwatake wataalamu na viongozi wa Serikali kuhakikisha kuwa mipango na maazimio ya JPC yanatekelezwa kwa wakati,” amesema.

Kwa upande wake, Waziri Nduhungirehe ameipongeza Tanzania kwa ushirikiano mzuri na kusisitiza kuwa Rwanda itaendelea kushirikiana kwa karibu na nchi jirani ili kuhakikisha maridhiano ya kweli yanapatikana kupitia utekelezaji wa maazimio yaliyofikiwa.

“Makubaliano kama haya ni nyenzo muhimu ya kukuza uchumi, kuboresha usalama wa chakula, na kuimarisha mshikamano wa kidiplomasia na kijamii kati ya mataifa haya mawili,” amesema.

Aidha, Mkutano wa 16 wa JPC umejadili masuala mbalimbali ya ushirikiano ikiwemo biashara, ulinzi na usalama, miundombinu, afya, elimu, nishati na kilimo.

Mazungumzo hayo yamekuwa na tija na yamefanikisha hatua za pamoja za kuendeleza mahusiano ya kidiplomasia na kiuchumi baina ya Tanzania na Rwanda.

Akizungumza alipotafutwa na Mwananchi, Mtaalamu wa Biashara na Uchumi, Dk Donath Olomi, amesema faida yake inaongeza uhakika wa soko la Rwanda kutumia mfumo wa usafirishaji wa Tanzania.

“Tukumbuke Rwanda wanaweza kutumia Mombasa pia, kwa hiyo soko la Rwanda ni la nchi kama Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) pia, kwa hiyo kitendo hicho kinaongeza wepesi wa Rwanda kutumia bandari yetu na pia kukamata soko la nchi zinazokua.

Amesema uchumi wa Tanzania na nchi za jirani unakua na ni fursa kubwa kwa nchi yetu sasa. Ikiwa kuna uhusiano mzuri, maana yake tunaendelea kupata uhakika wa soko sambamba na kuimarisha uhusiano.