UONGOZI wa Mbeya City uko katika hatua nzuri za kumsajili winga wa FC San Pedro ya Ivory Coast, Aboubakar Karamoko baada ya mabosi wa kikosi hicho kilichopanda kushiriki Ligi Kuu Bara 2025-2026 kuvutiwa sana na uwezo mkubwa wa nyota huyo aliouonyesha.
Nyota huyo raia wa Ivory Coast aliyezaliwa Oktoba 15, 1999, alijiunga na San Pedro Agosti 2, 2024, akiwa mchezaji huru baada ya kuachana na FK Auda ya Latvia aliyojiunga nayo akitokea United FC (UAE) ya Falme za Kiarabu iliyopo huko Dubai.
Taarifa ambazo Mwanaspoti imezipata, zinaeleza winga huyo tayari amefanya mazungumzo na Mbeya City, huku akiwataka kabla ya kufanya jambo lolote wamtumie mkataba kwa njia ya mtandao, kisha baada ya hapo ndipo atafanya uamuzi wake wa mwisho.
“Alituomba mkataba tumtumie kwa njia ya mtandao na sisi tumefanya hivyo, tunasubiria ausome na kama atakubaliana na kile tulichokipanga kwa maana ya makubaliano, basi atausaini akiwa Ivory Coast kabla ya kuja nchini,” kilisema chanzo hicho.
Nyota huyo mwenye uzoefu, alianza kucheza soka katika akademi ya Aspire iliyopo Qatar, akaichezea Atletico Malagueno ya Hispania, Septemvri Sofia (Bulgaria) kisha Doxa Katokopias, Digenis Akritas Morfou na Ermis Aradippou zote za Cyprus.
Baada ya hapo, nyota huyo aliyezaliwa Abidjan akiwa na uwezo wa kucheza winga zote mbili kwa ufasaha kwa maana ya kulia na kushoto, akazichezea pia FK Auda na Riga FC zote kutoka Latvia, jambo ambalo Mbeya City wanaamini ana uzoefu mkubwa.
Mbeya City iliyorejea Ligi Kuu Bara baada ya kushuka daraja msimu wa 2022-2023, tayari imeanza mawindo ya nyota wa kuwaongezea nguvu, ambapo hadi sasa imekamilisha usajili wa aliyekuwa beki wa kati wa Mashujaa FC, Ibrahim Ame.