BAADA ya majadiliano ya ndani na tathmini ya kina, hatimaye klabu ya Simba imechagua Misri kuwa ngome ya maandalizi ya msimu ujao wa mashindano 2025-2026 ikiwa ni mkakati wa kujenga kikosi madhubuti kitakachopambana kwa ajili mataji ndani na nje ya nchi, huku siri ya kutimkia huko ikitajwa.
Kwa mujibu wa taarifa rasmi kutoka klabu hiyo yenye maskani yake Mtaa wa Msimbazi, kikosi kinatarajiwa kuondoka Jumatano ya wiki ijayo kuelekea moja kwa moja kwenye mji wa Ismailia ambao umewahi kuwa mwenyeji wa mechi za AFCON na kambi za timu mbalimbali barani Afrika kutokana na mazingira yake rafiki.
Simba imekuwa kwenye mjadala wa ndani kwa wiki kadhaa kuhusu wapi pa kuweka kambi, ikiwa na mapendekezo makubwa mawili mezani kutoka kwenye benchi lao la ufundi ambapo ni Misri au Uturuki.
Ingawa Uturuki ilikuwa chaguo lenye mvuto wa kimataifa na miundombinu ya hali ya juu, gharama na uhusiano wa karibu wa Simba na baadhi ya vituo vya mafunzo nchini Misri ulifanya uchaguzi kuwa mwepesi. Ikumbukwe kuwa msimu uliopita pia kikosi hicho kiliweka kambi eneo hilo.
“Kulikuwa na tathmini ya kina. Kocha Fadlu Davids na benchi lake waliweka vigezo kadhaa kwanza, mazingira ya hali ya hewa, pili ufanisi wa mazoezi, na tatu ukaribu wa kijiografia. Misri ikawa chaguo bora kwa vigezo vyote hivyo,” chanzo cha ndani kutoka Simba kililiambia Mwanaspoti.
Ismailia ni mji uliopo kando ya Mfereji wa Suez, wenye miundombinu ya kisasa ya michezo, hoteli bora, na viwanja vya mazoezi vya daraja la kwanza.
Pia una hali ya hewa ya joto ya wastani ambayo ni rafiki kwa maandalizi ya kimwili, hasa kwa timu kutoka ukanda wa Afrika Mashariki.
Hii ni mara nyingine tena Simba inakwenda Misri kuweka kambi ya maandalizi ya msimu mpya ikiwa na matumaini ya kufanya vizuri 2025-2026.
Msimu uliopita 2024-2025, Simba ilijichimbia katika mji wa Ismailia nchini Misri ikiwa chini ya Kocha Fadlu Davids.
Kabla ya hapo, Simba maandalizi ya msimu wa 2023-2024 ilipokuwa ikinolewa na Roberto Oliveira ‘Robertinho’ ilikwenda Uturuki, huku msimu wa 2022-2023 kambi yao ikiwa mji wa Ismailia nchini Misri wakati kocha akiwa Zoran Maki.
Kocha Didier Gomes katika maandalizi ya msimu wa 2021-2022, aliipeleka Simba kambini katika mji wa Rabat nchini Morocco.
Habari za uhakika ambazo Mwanaspoti imezipata kutoka kwa maofisa wa Simba zinasema kuwa wachezaji wapya kadhaa hawatasafiri na kikosi kutoka Dar es Salaam ambako kambi ya awali itaanza Jumatatu, badala yake wataungana moja kwa moja na timu nchini Misri.
“Baadhi yao walikuwa wakikamilisha masuala ya ruhusa kutoka klabu zao za zamani, wengine walikuwa likizo. Lakini wote wameelekezwa waelekee moja kwa moja Misri,” kilisema chanzo chetu.
Kwa kocha Fadlu Davids, huu ni msimu wa kuthibitisha ubora wake. Alipowasili Simba msimu uliopita, alikabidhiwa timu ikiwa kwenye kipindi cha mpito. Lakini alifanikiwa kuiimarisha na kuiweka kwenye ramani ya soka la kisasa ingawa hakuambulia kombe lolote.
Lakini kitendo cha kuifikisha timu hiyo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika ilikuwa ni mafanikio makubwa kwa kikosi ambacho kilikuwa kinajengwa upya chini ya kocha huyo.
Simba haijiandai kwa Ligi Kuu pekee. Kuna mashindano ya Kombe la Shirikisho la CAF, FA Cup, Ngao ya Jamii na pia mechi za kirafiki za kimataifa ambazo zitapangwa wakati wa kambi.
Uwepo wa baadhi ya wachezaji waliokuwepo msimu uliopita kama Elie Mpanzu, Charles Jean Ahoua, Joshua Mutale, pamoja na sajili mpya unatarajiwa kuleta ushindani mkubwa kambini.
Kambi hii ndiyo itatoa sura halisi ya kile ambacho Simba itakuwa nacho msimu wa 2025/26.